Wednesday, February 19, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Sadeq al Sadr ni nani?


Februari 19, 1999 alifariki dunia kiongozi wa juu wa Waislamu wa Kishia nchinio Iraki; Ayatollah Mohammed Mohammed Sadeq al-Sadr. 

Kiongozi huyo wa Washia aliuawa na majeshi ya Saddam Husseim kutokana na kutofautiana katika mtazamo.  

Al Sadr alianza kuonekana katika siasa za Iraki hususani mwanzoni mwa vita vya Ghuba.

Itakumbukwa vita ya Ghuba ilianza  Agosti 2, 1990 – 28 Februari 28, 1991 baina ya Marekani na washirika wake akali ya mataifa 35 enzi za utawala wa George Herbert Bush na Saddam Hussein aliyekuwa akiiongoza Iraki.  

Al Sadr alionyesha upinzani wa wazi kwa Saddam Hussein. Alifikia hatua akaanzisha mji wa kimaskini wa Washia wa Sadr City. 

Hapo awali ulikuwa ukifahamika kama Al-Thawra au Saddam City. 

Pia Al Sadr alionyesha upinza huo sio tu kwa Saddam Hussein pia hata kwa chama chake cha Baath. 

Al Sadr alipata uungwaji mkono na Washia hatua iliyomwezesha kuwafikia Washia wengi waliokuwa vijijini  na kutoa huduma ambayo haikuwa inafanywa na utawala wa Saddam Hussein. 

Miaka ya mwanzoni ya 1990 Saddam Hussein alianza kujipenyeza kwa Washia na kuwapa nafasi ili aweze kupata uungwaji mkono kwa ajili ya kuongoza taifa hilo. 

Kabla ya hapo Saddam Hussein aliwahi kufanya jaribio lililoshindikana la mauaji ya Washia mnamo mwaka 1982 mjini Dujail. 

Watoto, wanawake na wasiojiweza walitupwa jela. Saddam Hussein alikuwa wa Waislamu wa Kisunni.  

Wakati fulani kabla ya kifo chake, Al Sadr aliwahi kufunguka na kuambiwa kwamba Saddam Hussein amefikia mwisho katika kumvumilia. 

Cha kustaajabisha Al Sadr alijua kuwa muda wake umewadia lakini aliona bora afe kuliko kumwacha Saddam Hussein aendelee na dharau zake kwa Washia. 

Katika hotuba yake siku ya Ijumaa aliwaonyesha Washia kwamba hawezi kuvumilia uonevu wa Saddam Hussein alihubiri ukweli hata kwa kufa. 

Hatimaye baada ya kuisha kwa mahubiri yake aliuawa wakati akitoka katika msikiti mjini Najaf. 

Watoto wake wawili waliuawa papo hapo kwa shambulio la risasi wakati akiendesha gari mjini hapo. Al Sadr mwenyewe alijeruhiwa vibaya katika shambulio hilo. 

Alikata roho saa chache baadaye baada ya kufikishwa hospitalini. 

Inaelezwa na Washia walioko Iraki na Waangalizi wa Kimataifa kuwa serikali ya Saddam Hussein iliyokuwa chini ya Chama cha Baath cha Iraki walihusika na shambulio hilo. 

Hasira ililipuka miongoni mwa Washia na kusababisha Kuibuka kwa Mapigano mwaka 1999 maarufu kama '1999 Shia Uprising in Iraq.'  

Maeneo ya jirani ya mji mkuu wa Iraki, Baghdad pia miji ya kusini mwa Iraki inayokaliwa na Washia wengi ya Karbala, Nasiriyah, Kufa, Najaf na Basra ililipuka kwa vurugu na maandamano ambayo zaidi ya watu 200 waliuawa na maelfu kujeruhiwa na wengine kukamatwa. 

Baada ya kuanguka kwa Baghdad, kitongoji maarufu nchini humo cha Saddam City, kilibadilishwa jina na kuitwa Sadr City. 

Tukio hilo la kubadilishwa kutoka Saddam City na kuwa Sadr City sio rasmi  licha ya kwamba wengi wa Washia walifanya hivyo kwa ajili ya kuonyesha kumkumbuka kiongozi wao Sadeq al-Sadr. 

Aidha Sadr City kilikuwa ni eneo la kwanza kabisa katika Baghdad kuvamia Chama cha Baath 2003. 
Mtoto wa Al Sadr aliyefahamika kwa jina la Muqtada al-Sadr ndiye kiongozi wa sasa wa Washia hao waliokuwa wakifuata nyayo na maelekezo ya Al Sadr. 

Muqtada aliwaongoza Washia katika mapambano dhidi ya Serikali mpya ya Iraki kati ya mwaka 2004 hadi 2008.

Al Sadr alipenda kuandika ambapo alifanya kazi yake ya Utumishi wa Waislamu hao wa Kishia  alipoandika kitabu cha Al-Islam wal-Mithaq al-Alimiyah lil-Huquq al-Insan  (Uislamu na Makubaliano ya Kimataifa kuhusu Haki za Binadamu); Ma Wara al-Fiqh (Kilichopo nyuma ya Sheria) na Fiqh al-Asha'ir (Sheria za Kimila)

Alizaliwa Machi 23, 1943 mjini Al Kazimiya kaskazini mwa Baghdad nchini Iraki, ambapo baba yake alifahamika kwa jina la Mohammad Sadeq Al-Sadr (1906–1986) kutoka katika familia yenye asili ya Lebanon.

Wakati akianza kung'ara Al Sadr alikuwa akipokea upinzani kutoka kwa viongozi wengine wa Shia akiwamo Ayatollah Mohammed Baqir al-Hakim. 

Al Hakim alipoona hawezi aliikimbia nchi ya Iraki na kwenda kuishi uhamisho kwa miaka 20.  Al Hakim alifariki dunia Agosti 29, 2003 akiwa na umri wa miaka 63 kwa kulipuliwa na bomu mjini Najaf. 

Inaelezwa kuwa kuuawa kwake kulitengenezwa na wanachama wa cham cha Baath kilichokuwa kimeshika serikali wakati huo. 

Al Hakim aliuawa kwa bomu wakati akitoka katika kaburi la Imam Ali, ambapo mlipuko huo uliuwa na wengine 75.

0 Comments:

Post a Comment