Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Tuesday, June 30, 2020

Nyumba isiyokalika katika 'Bwawa la Damu' kwa Mangi Horombo

Baadhi ya wasomi wamezigawanya ndoto katika katika makundi makuu matatu, kundi la kwanza wanasema ni zile ndoto zinazotokana na Mungu, kundi la pili ni zile zinazotokana na shetani na kundi la tatu ni ndoto zinazotokana na mtu mwenyewe.

Kundi hili la tatu linatafsiriwa kuwa ndizo zinazochukua sehemu kubwa ya ndoto tunazoziota karibu kila siku kwenye maisha yetu. Wanachambua kwa kina kuwa aina hii ya tatu huwa inakuja kutokana na shughuli zetu tunazozifanya kila siku au mazingira yanayotuzunguka kila siku.

Wakati mwingine unaweza ukaota umefiwa na mzazi, au kaka au dada, au mtu wako wa karibu. Na ndoto hizi huwa zinakuja kwa uzito sana, kiasi kwamba unaposhtuka huamini kama kweli ilikuwa ni ndoto, kwasababu unaona kama tukio hilo lilikuwa ni halisi kabisa, unabaki kuishia kumshukuru Mungu na kusema asante  kwa kuwa ilikuwa ni ndoto tu huku ukihema kwa nguvu.

Kuna wakati unaota ukiwa utupu, halafu unakatiza barabara hususani maeneo ya mjini. Ukiwa ndani ya ndoto  unajiona na kuanza kutafuta namna ya kujificha, unajibanza katika vichochoro kisha unavizia watu wapungue ili ukimbilie upande mwingine. Wakati ukiyafanya hayo unakimbia na kurudi nyumbani ukidhani kwamba hujaonekana na wengi.

Muda kidogo wanakuja marafiki zako wa kike na kukuuliza mbona kuna picha zako zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii zikikuonyesha ukikatiza barabara ukiwa utupu na wakati wewe ni wa kiume, sasa linageuka songombingo ndani ya ndoto unaishiwa nguvu, unajiona ukipata fedheha ya milele isiyoweza kufutika unatamani kama ardhi ipasuke ikufukie.

Pia wakati mwingine unaota unapaa na watu usiowajua na wanakupeleka usipojua, au unaenda sehemu za kutisha, na unapoamka unakuwa huna amani umejawa na hofu na wasiwasi mwingi. Ndoto kama hizi huwa zinawapata watu wengi. Hata hivyo inakuwa ni vigumu kutoa jibu la moja kwa moja kuhusu ndoto hizo na vyanzo vyake ama Mungu au Shetani au mtu mwenyewe.

Sasa basi hitimisho kubwa hubaki katika kipengele kinaitwa mitholojia. Inavyoaminika ndoto huja kuelezea jambo moja kwa moja kama lilivyo au kinyume chake au huelezea kwa njia ya mifano na wakati mwingine huja kama fumbo.

Katika makala haya tutaangazia namna ambavyo nyumba iliyojengwa katika milki ya zamani ya Mangi Horombo huko Rombo mkoani Kilimanjaro ilivyozua tafrani na kusababisha watu kuiacha ukiwa, kutokana na ndoto na mauzauza kibao kwa waliokuwa wakiikaa hapo.

Mtunzaji wa eneo hilo Melania Peter Urio (65) anasema hakubahatika kumwona Mangi Horombo isipokuwa alikutana na taarifa mbalimbali zinazomhusu mangi huyo, miongoni mwa hizo ni eneo hilo linalofahamika kama ‘Bwawa la Damu’.

SABABU ZA KUITWA BWAWA LA DAMU

Sababu kuu za kuitwa Bwawa la Damu ilikuwa ni mauaji yaliyokuwa yakifanyika katika eneo hilo la Milki ya Mangi Horombo wakati wa vita vya koo zilikuwa zikipingana na kujiunga na utawala wa Mangi huyo.

Bi Melania anasema kuwa eneo hilo lilikuwa la maoteoni wakati wa vita inapokuwa kali walikuwa wakijificha na mara maadui walipokuwa wakiingia hapo walivamiwa na kuuawa.

“Mangi Horombo alilitengeneza kwa ajili ya ulinzi, maadui walipokuwa wakija waliwapitisha kwenye upenyo uliokuwa wazi huku wenyewe wakiangalia kutoka juu wakiingia hapo wanawaulia na kuwachoma moto,” anasema Bi. Melania.

Bi Melania anasisitiza kuwa askari wa Mangi Horombo walikuwa wakitumia mbinu ya kushtukiza kuzivamia koo fulani fulani na kujifanya kama wamezidiwa hivyo kuanza kukimbia, pindi wanapokimbia hukimbilia katika uelekeo ulipo upenyo ambao lazima maadui watawafuata kwenye mtego huo.

“Mara zote mtego huu uliwanasa maadui wengi na waliuawa wa kutosha, kwasababu maaskari wengine walikuwa wamejificha juu, …” anasema Bi. Melania.

Kwa upande wake Afisa Utamaduni  wa wilaya ya Rombo Florentine Henrico Langu, anasema kuwapo kwa Bwawa la Damu ni miongoni mwa vivutio vya utalii wa utamaduni katika wilaya hiyo ambao unaweza kukuza utalii wa ndani kutokana na wilaya hiyo kuwa na vivutio vingi vya asili.

UWEPO WA NYUMBA YENYE MAUZAUZA

Baada ya miaka mingi kupita, na eneo hilo kuanza kupotea palionekana kama tambarare nzuri ambayo inafaa kujengwa, ndipo baadhi ya wana ukoo wa Mangi Horombo waliamua kujenga nyumba hapo kwa ajili ya kuishi.

Nyumba hiyo ilikamilika na wahusika hawakukaa sana wakaondoka lakini inaelezwa kuwa hakuna mtu yeyote anayetaka kukaa humo kutokana na hofu inayojitokeza wakati wa usiku kwani ndoto ndoto za ajabu haziishi.

Bi Melania anasema wenye nyumba baada ya kumaliza ujenzi huo walienda zao Dar es Salaam, lakini waliamua kuwaacha watu wa kuilinda lakini baadaye watu hao waliondoka kutokana na mauzauza hayo.

“Mwenyewe unaiona nyumba, ilivyo nzuri lakini hakuna anayetaka kukaa, hata wa kupanga hawataki kila mmoja anahofia usalama wake ndoto za ajabu zinawajia,nyumba inaota nyasi tu,” anasema Bi. Melania.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu sababu za mauzauza hayo ni kwamba huenda kutokana na damu iliyomwagika hapo hasa kutokana na Mangi Horombo ambaye alikuwa mbabe na mwenye nguvu zote za kimwili na kiroho.

“Huyu Mangi Horombo alikuwa kama wachifu wengi ambao walikuwa wakimiliki maeneo na kuzishinda koo nyingine hata kwa uchawi, inawezekana hata kuwateketeza kwenye eneo hili kulitokana na kuwapumbaza kichawi,” anaongeza Bi. Melania.

Mangi Horombo alifariki dunia akiwa na miaka 82 mnamo mwaka 1802. Katika mkoa wa Kilimanjaro Mangi Horombo ndiye pekee aliyeenziwa kwa jina lake kusalia katika ukumbusho wa vizazi hata vizazi.

Kwasababu mkoa wa Kilimanjaro una wilaya za Hai, Same, Mwanga, Moshi na Rombo. Wilaya ya Rombo pekee katika kupewa jina hilo ilichaguliwa kutokana na Mangi Horombo.

Pia wakati unapopanda mlima Kilimanjaro kwa njia ya Marangu kuna kituo kinafahamika kwa jina la Horombo hiyo ni kwasababu ya umarufu wa Mangi Horombo aliyekuwa mtawala wa eneo ambalo kwa sasa ni Rombo.

Historia yake ni ndefu lakini sifa yake ya ubabe kwa wakorofi na mpatanishi kwa waliogombana vilimfanya ajichotee umaarufu katika kuteka koo mbalimbali.

Alifariki dunia wakati vita na koo moja upande wa Kenya. Inaelezwa alipigwa mshale wenye sumu kali na kupoteza maisha. Jina lake halisi alilopewa wakati anazaliwa ni Maingudu.

MAKTABA YA JAIZMELA: Kaisari Nepotianus ni nani?

Juni 30, 350 alifariki dunia mtawala wa Rumi mwite Kaisari Nepotianus. Kaisari huyu alifariki dunia kwa kuuawa baada ya kukalia kiti cha kuliongoza taifa hilo kwa siku 28 tu.

Jina lake halisi ni Flavius Julius Popilius Nepotianus Constantinus. Nepotianus alikuwa ni wa ukoo wa Constantino ambaye alitawala isivyo halali baada ya kuchukua nafasi hiyo kimabavu. Waliofanikisha jaribio la kummaliza kiongozi huyo walikuwa ni kundi jingine lililokuwa na tamaa ya kushikilia usukani wa kuliongoza taifa hilo.

Mauaji hayo yalifanywa na Jenerali Marcellinus wa kikosi au wafuasi wa Magnentius. Baada ya kufanya mauaji hayo Magnentius alishika utawala huo hadi mwaka 353.

Siku ya kukalia kiti hicho ilikuwa Juni 3, 350 ambapo Nepotianus aliingia jijini Rome akiwa na bendi ya waliokuwa wakimuunga mkono. Kwa kawaida kila mji wakati huo ulikuwa na kiongozi alitekuwa akifahamika kama Praefectus urbi.

Sasa wakati Nepotianus alipokuwa akiingia jijini humo Praefectus urbi wa wakati  huo alikuwa Titianus (Anicius) ambaye alishindwa kumzuia Nepotianus. Pia inaelezwa Titianus alikuwa mfuasi wa Magnentius , hivyo kuona mambo yameharibika alikimbia mji na Nepotianus akashikilia mahali pale.

Magnentius kwa haraka sana akajibu mapigo hayo kwa kumpeleka mtu aliyekuwa akiijua sharia vizuri na aliyemwamini Marcellinus huko jijini Rome.

Kwa mujibu wa mwanahistoria wa Rumi aliyefahamika kwa jina la Eutropius alisema, Nepotianus aliuawa wakati akipambana Juni 30, 350 na kichwa chake kilitundikwa katika fimbo ndefu na ikatembezwa katika viunga vya jiji la Rome ili watu wajionee.

Mama wa mwanahistoria huyo pia aliuawa wakati akibishana na wafuasi wa Nepotianus ambao wengi wao walikuwa maseneta. 

EU yasema ipo tayari kwa uangalizi uchaguzi mkuu Tanzania 2020 ikipewa mwaliko

Umoja wa Ulaya (EU) umesema upo tayari kuwa mwangalizi wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2020 nchini Tanzania, endapo watapata ridhaa kutoka katika mamlaka husika.

Balozi wa Umoja wa Ulaya kwa nchi za Afrika Mashariki Manfredo Fanti alisema hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika baina ya taifa hilo la Afrika mashariki pamoja na jumuiya hizo ya kimataifa kuhusiana na suala la uchaguzi, ijapokuwa upo tayari kufanya uangalizi wa uchaguzi huo ambao utawaweka mamlakani, madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha Balozi Fanti alisema taifa lina jukumu la kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi huru, haki na amani katika kipindi chote cha uchaguzi, huku akisisitiza kuwa umoja huo hauna mamlaka ya kuangalia uchaguzi bila mamalaka husika kutoa idhini.

Itakumbukwa kuwa sehemu ya kanuni za uchaguzi zinaeleza kuwa, Tume inaweza kutuma mwaliko kwa waangalizi wa kimataifa, jambo ambalo lilitoa wasiwasi kwa vyama vya siasa hasa upinzani kwamba huenda NEC isitoe fursa hiyo kwa jumuia za kimataifa kufuatilia kwa ukaribu zoezi hilo la kidemocrasia kama ilivyofanyika kwa chaguzi zilizopita.

CHANZO: DW


Monday, June 29, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Moise Tshombe ni nani?

Juni 29, 1969 alifariki dunia mwanasiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Moise Tshombe. 

Mwanasiasa huyo alikuwa Rais wa kwanza wa jimbo lililotaka kujitenga Lenye utajiri wa madini ya shaba la Katanga huko DRC. Pia alikuja kuwa Waziri Mkuu wa DRC.

Alifariki dunia jijini Algiers, Algeria akiwa na umri wa miaka 49.  Mnamo mwaka 1967, Tshombe alihuhukumiwa kifo bila yeye mwenyewe kuwepo (in absentia).

Juni 30, 1967 akiwa nadani ya ndege ya Hawker Siddeley ambayo ilitekwa na Francis Bodenan ambaye alikuwa wakala wa ujasusi wa SDECE ya Ufaransa. Kwa mujibu wa taarifa za serikali ya DRC wakati huo zilisema kuwa, Tshombe alikuwa akienda Afrika.

Tshombe alipelekwa Algeria ambako alitupwa jela na kuwekwa chini ya ulinzi mkali. Marubani wa ndege Britons Trevor Coppleston na David Taylor waliachiliwa na walirudi zao nchini Uingereza.

Serikali ya DRC ilikuwa ikitaka arudishwe nchini mwake lakini ilishindikana kutokana na waungaji mkono wake wa Kimagharibi walikataa kuachiliwa kwake. Algeria nao walikataa maombi yote mawili ya DRC na waungaji mkono wa Kimagharibi.

Kamati maalumu ya Tshombe iliyokuwa nchini Marekani ikiongozwa na Marvin Liebman na William F. Buckley walianza harakati za kushinikiza Tshombe kuachiliwa na kupelekwa nchini Hispania.

Rafiki mkubwa na mtoaji wa misaada wa Tshombe aliyefahamika kwa jina la Michel Struelens alisafiri katika miji tofauti barani Ulaya ili kupata uungwaji mkono wa sehemu ya kumweka Tshombe lakini hakupata msaada.

Tshombe alifariki dunia kwa kile kilichoelezwa mshtuko wa moyo huko Algiers. Tshombe alizikwa katika makaburi ya Etterbeek karibu na Brussels nchini Ubelgiji.

Tshombe kama alivyokuwa Patrice Lumumba amekuwa akichukuliwa kuwa alama muhimu katika mapambano dhidi ya uzalendo wa Mwafrika.

Mwanadiplomasia wa DRC Thomas Kanza mnamo mwaka 1972 alikaririwa akimwelezea Tshombe alikaribia kuwa mkombozi wa DRC. “Moise Tshombe alikaribia kuwa mwokozi wa Congo wakati akirudi kutoka uhamishoni. Lakini historia iliamua vinginevyo na watu wa Congo walijikuta wakiwa chini ya uongozi wa Mobutu.”

Jina lake halisi ni Moise-Kapenda Tshombe. Alizaliwa Novemba 10, 1919 katika mji mdogo wa Musumba katika ardhi ya DRC wakati huo ikiitwa Belgian Congo. Aliamua kujitenga na kuwa kiongozi wa jimbo la Katanga mnamo mwaka 1960.

Alipata nguvu ya kujitenga kutokana na nguvu za kijeshi kutoka kwa washirika wake. Kwa miaka mitatu alifanikiwa kuisimamia ardhi huru ya Katanga akiungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Tshombe alikuwa mwanasiasa mwenye akili katika siasa za DRC enzi za uhai wake.

Mnamo mwaka 1963 majeshi ya UN yaliivamia Katanga na kumwondoa Tshombe ambaye alikimbia uhamishoni Northern Rhodesia (Zambia) na baadaye alikwenda Hispania.

Mnamo Julai 1964 alirudi nchini DRC ambako alihudumu kama Waziri Mkuu wa serikali mpya ya Muungano. Baraza lake liliapishwa Julai 10.

Tshombe alikuwa akiungwa mkono na wanasiasa wa majimbo ya DRC, machifu na wenye fedha kutoka nje.

Aliposhika nafasi hiyo jambo la kwanza alilolifanya ni kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa 600 akiwamo Antoine Gizenga na aliamuru wanajeshi wa Katanga waliokimbilia Angola kurudi DRC na kuungana na jeshi la taifa hilo.

Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya mnamo mwaka 1965, Tshombe alikataa kuungana na Waasi wa Simba ambao walikuwa wafuasi wa Lumumba.

Aliondolewa katika Uwaziri Mkuu wa DRC mnamo Oktoba 1965 na Rais Joseph Kasavubu. Mwezi Novemba ikiwa ni mwezi mmoja baada ya kuondolewa katika nafasi hiyo Jenerali Mobutu Sese Seko alifanya jaribio lililofanikiwa na kumwondoa madarakani Kasavubu.

Pia Mobutu alipeleka mashtaka ya uhaini dhidi ya Tshombe ambaye kwa mara nyingine alilikimbia taifa hilo na kwenda uhamishoni nchini Hispania wakati huo ikiwa mikononi mwa dikteta Francisco Franco na ndio ukawa mwanzo wa safari ndefu ya taifa hilo mikononi mwa Mobutu.

Lazarus Chakwera: Rais wa kwanza Mlokole nchini Malawi

Nchini Malawi kumeshuhudiwa Kiongozi wa chama cha upinzani cha Malawi Congress (MCP) Lazarus Chakwera, akiapishwa jana (Juni 28, 2020) kama rais mpya wa nchi hiyo baada ya kuibuka mshindi kwa asilimia 58.7 za kura.

Katika sherehe hiyo ya kuapishwa katika mji mkuu wa Lilongwe, Chakwera aliapa kufanya majukumu yake vyema, kuilinda na kuitetea katiba ya nchi hiyo. Chakwera pia alitoa hakikisho kwa wafuasi wa rais wa sasa aliyeshindwa katika uchaguzi huo Peter Mutharika kwamba hawapaswi kuwa na hofu na kwamba Malawi mpya ni nchi yao pia.

Tume ya uchaguzi nchini humo jana usiku ilimtangaza kiongozi huyo kuwa rais mteule wa sita wa taifa hilo baada ya kumshinda rais wa sasa Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progressive Party.

Uchaguzi huo mpya uliandaliwa baada ya mahakama kuu nchini humo kufutilia mbali ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2019 kutokana na dosari nyingi zilizobainika ikiwemo kutumika kwa wino wa kufanya marekebisho katika karatasi za matokeo. Juni 27, 2020 Mutharika aliutaja uchaguzi huo uliofanywa Juni 23 kuwa mbaya zaidi katika historia ya nchi hiyo.

LAZARUS CHAKWERA NI NANI? 

Jina lake halisi ni Lazarus McCarthy Chakwera. Alizaliwa Aprili 5, 1955 jijini Lilongwe ambao ni mji mkuu wa Malawi. Wakati huo taifa hilo lililikuwa mikononi mwa utawala wa Uingereza.

Familia yake ilikuwa ni ya wakulima katika viunga vya jiji hilo. Kaka zake wawili waliozaliwa kabla yake walifariki dunia wakiwa bado wadogo. Baba yake alipozaliwa mwanaye huyo akampa jina lake Lazarus (Lazaro) ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu kwa mujibu wa maandiko ya Biblia.

Baba yake hakuwa na tumaini tena kutokana na watoto wake kufariki dunia. Lazarus alimwoa Monica na wawili hao wamefanikiwa kuzaa watoto wanne na wana wajukuu. Chakwera ni mwanasiasa mbapo kabla hajaiingia katika siasa alikuwa mwanatheolojia.

Alikuwa kiongozi wa MCP tangu mwaka 2013 na zamani walikuwa kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa nguvu zote alipinga uchaguzi uliojawa na mkanganyiko wa Mei 21, 2019 ambao ulipigwa chini na Mahakama ya Katiba. Alikuwa Rais wa Kanisa la Malawi Assemblies of God kutoka mwaka 1989 hadi Mei 14, 2013.  

Alihitimu masomo ya Sanaa (Falsafa) katika Chuo Kikuu cha Malawi mnamo mwaka 1977. Alisoma masomo ya theolojia na kutunukiwa shahada yake katika Chuo Kikuu cha North nchini Afrika Kusini. Pia alipata shahada ya uzamili (MTh) katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini mnamo mwaka 1991.

Pia mnamo mwaka 2000 alitunukiwa shahada ya uzamivu nchini Marekani katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Trinity kilichopo Deerfield huko Illinois. Alitunukiwa Uprofesa katika Pan-Africa Theological Seminary mnamo mwaka 2005.

Chakwera aliwahi kuhudumu kama Mwalimu katika shule za Kitheolojia za Assembilies of God kutoka mwaka 1983 hadi 2000 ambako alikuja kuwa Principal mnamo mwaka 1996. Pia alikuwa instructor na lecturer katika All Nation Theological Seminary.

Tangu Aprili 14, 2013 aliustaajabisha ulimwenguni hususani kanisa lake la Assemblies of God  alipotangaza kwamba ataongoza upinzani nchini humo wakati huo akiwa Rais wa Assemblies of God hatimaye alifanikiwa na sasa ni Rais wa taifa la Malawi.

Ifahamu historia ya Mji wa Moshi

Historia ni somo kuhusu maisha ya binadamu na utamaduni wao wakati uliopita. Mara nyingi neno historia pia lina maana ya maarifa yoyote kuhusu wakati uliopita, yawe au yasiwe maarifa ya watu (kwa mfano "historia ya ulimwengu").

Wanahistoria wanapata maarifa yao kutoka maandishi ya zamani (hasa kwa Historia andishi), kutoka fasihi simulizi na kutoka akiolojia (hasa kwa Historia ya awali).

Kwa mfano historia ya neno Kilimanjaro; Umaarufu wa jina hili umetokana na mlima mrefu uliosimama pekee unaoitwa Mlima Kilimanjaro, upatikanao kaskazini mwa Tanzania.

Asili ya neno hili ni makosa ya kisarufi yaliyofanywa na wageni kutoka ng'ambo ambao waliwasili eneo hilo karne ya 18 na kuwakuta wazawa  wakiishi maeneo hayo kuuzunguka mlima huo.

Inasemekana kuwa wazawa wa eneo hilo yaani wachaga waliuita mlima huo 'kilimakyarooo', wakimaanisha kilima kirefu.

Lakini kutokana na kushindwa kutamka hilo neno 'wazungu' walitamka kwa namna yao na kuuita huo mlima Kilimanjaro, ambalo ndilo neno litumikalo hadi hivi sasa kutokana na kwamba wao waliweza kuhifadhi hilo jina kwa njia ya maandishi na kulitangaza kote duniani.

Neno ‘Kilimanjaro limetumika pia kuutaja mkoa wa Kilimanjaro ambao una wilaya zipatazo saba za Same, Mwanga, Rombo, Moshi Vijijini, Moshi Mjini, Hai na Siha

Katika makala haya tutaangazia mji wa Moshi, sababu ya kuitwa jina hilo.

Mji wa Moshi ulianzia katika eneo la Old Moshi, Tsudunyi upande wa milimani ambako sehemu hiyo ilikuwa ikiitwa Moshi hapo kabla.

Wakati wa ujio wa wageni mbalimbali kutoka nje ya bara la Afrika katika ardhi ya Uchagani  miaka ya katikati ya karne 19 kwa ajili ya kufanya biashara na upelelezi wa upatikanaji wa mali ghafi walikutana na jamii zenye nguvu.

Wakitokea maeneo Ya Pwani, Ulaya, Asia na Uarabuni waliikuta Old Moshi ukiwa ndio mji mkubwa zaidi kibiashara katika ardhi ya uchagani ikiwa mikononi mwa kiongozi shupavu Mangi Mkuu Rindi Makindara.

Mangi Mkuu aliingia mikataba mbalimbali ya kibiashara na mahusiano ya kidiplomasia na serikali za Waingereza, Wajerumani na hata Zanzibar.

Baada ya Mangi Rindi Mandara Kufariki, Wajerumani ambao walikuwa wameshajipanga walibadilika na kuanza kuwa wababe wakati huo Gavana wa Wajerumani Kilimanjaro akiwa Dkt. Karl Peters na walijenga kituo cha kijeshi Old Moshi, hiyo ikiwa ni mwishoni mwa mwaka 1891.

Huo ndio ukawa mwanzo wa utawala wao Kilimanjaro. Hata hivyo Umangi wa Old Moshi ulikuwa umerithiwa na Mangi Meli Mandara mtoto wa Mangi Rindi Mandara ambaye alikuwa jeuri na mwenye kujiamini sana na hakutaka kuwa chini ya utawala wa Wajerumani.

Mangi Meli hivyo hakukuwa na maelewano mazuri kati yake na Wajerumani na hata watu wa Old Moshi kwa ujumla walikuwa wajeuri sana dhidi ya ubabe wa wajerumani.

Wakati huo huo Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu aliimarisha mahusiano yake na Dr. Karl Peters kiasi cha kumzawadia binti mrembo aliyeitwa Ndekocha.

Kitendo hicho kilimfanya  Dkt. Karl Peters ahamishe Ofisi za Utawala za Wajerumani Kilimanjaro Kutoka Old Moshi, Tsudunyi hadi Marangu, Lyamrakana mnamo mwaka 1892.

Lakini Karl Peters alifanya ukatili mwingi sana pamoja na mauaji katika ardhi ya Uchagani hususan Marangu kiasi cha kuimarisha sana ulinzi wake binafsi na hakuchukua muda mrefu aliondoka Kilimanjaro.

Gavana mpya Aliyekuja Kilimanjaro Von Bulow hakuwa na maelewano hata na Mangi Ndegoruo Marealle mwenyewe licha ya kuishi Marangu na alitumia mabavu kujaribu kulazimisha kila kitu.

Ubabe wake ulipelekea Von Bulow kuingia katika mzozo na Mangi Meli, wakati huo ofisi za utawala wa Wajerumani zikiwa Marangu alikozihamishia Karl Peters.

Von Bulow aliamua kuivamia tena Old Moshi kupambana na Mangi Meli ambaye alionekana ni jeuri sana na asiyetishika.

Von Bulow alikusanya majeshi yake pamoja na askari mamluki wa Kinubi kutoka Sudan na wengine wa Kizulu kutoka Afrika Kusini.

Mashushushu wa Mangi Meli Walikuwa Makini Kufuatilia nyendo zao na mnamo Juni mwaka 1892, waliivamia old moshi.

Jeshi imara la Mangi meli lililojumuisha askari kutoka Old Moshi, Uru na Kilema walijibu mapigo kwa ustadi mkubwa na askari wa Von Bulow waliuawa kwa wingi sana na kuzidiwa.

Von Bulow alikimbia lakini alitafutwa na askari wa Mangi Meli akapatikana akiwa amejificha huko Kahe naye akauawa huko huko.

Baada ya Von Bulow kuuawa Wajerumani wote Kilimanjaro walikimbia na hawakuthubutu kurudi Kilimanjaro kwa karibu mwaka na nusu, mpaka waliposhawishiwa sana kurudi na taasisi za kidini.

Baada ya kushawishiwa sana, Wajerumani walirudi Kilimanjaro mwaka 1893 mwishoni wakiwa na silaha nzuri za kisasa kwa wakati huo za kivita na jeshi imara sana kupambana na majeshi ya Wachaga.

Waliingia Old Moshi usiku na kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwenye ngome ya Mangi meli.

Vita ilipiganwa siku mbili usiku na mchana na Mangi Meli na majeshi yake walizidiwa na kuamua kujisalimisha ili kuepusha mauaji zaidi.

Mangi Meli alipewa masharti ya kutoa malighafi na nguvu kazi ya kutosha kujenga kituo kipya cha kijeshi cha Wajerumani Old Moshi na Ofisi za utawala wa Wajerumani.

Baada ya vita ya pili kati ya Wachaga na Wajerumani gavana mpya wa wajerumani kilimanjaro kapteni Johannes aliamua kurudisha Old Moshi ofisi za utawala wa wajerumani kilimanjaro ambazo Karl Peters alikuwa amezihamishia Marangu.

Kapteni Johannes alizirudisha lli aweze kuidhibiti Old Moshi. Hapo ndipo mji wa Moshi ukarudi upya eneo hilo la Tsudunyi na Ofisi za Utawala Kilimanjaro kuanzia Mwaka 1893 - 1919.

Mwaka 1912 reli lliyokuwa inajengwa ikitokea Tanga Kuelekea Kilimanjaro ilifika katika tambarare za Moshi na taratibu ukaanza mji mpya ambao uliitwa "The New Moshi" Yaani Mji Mpya wa Moshi kwasababu mji wa Moshi wenyewe ulikuwa kule mlimani.

Mwaka 1919 Ofisi za Utawala Kilimanjaro pamoja na taasisi zake kama Hospitali Ya Mawenzi, Mahakama n.k. vilivyokuwa Old Moshi, zilihamishiwa huku chini kwenye tambarare ambapo palikuwa bado ni mapori na hakuna hali nzuri sana ya hewa.

Baadaye ule mji kule juu mlimani ukapewa jina jipya "The Old Moshi" na Mpaka Leo panaitwa Old Moshi. Majengo yaliyokuwa ofisi za utawala kule Old Moshi sasa hivi ndio Majengo ya Halmashauri ya Wilaya Ya Moshi Vijijini.

Baadaye Jina La "The New Moshi" au Kwa Kijerumani "Neu Moschi" Lilikufa na Kuitwa ‘Moshi’ mpaka leo. 

Sunday, June 28, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: James Madison Jr. ni nani?

Juni 28, 1836 alifariki dunia mwanasiasa, mwanadiplomasia, mwanafalsafa na mwanzilishi wa taifa la Marekani James Madison Jr. 

Huyu alikuwa Rais wa nne Marekani kutoka mwaka 1809 hadi 1817. Anachukuliwa kuwa mtu muhimu sana katika uandishi wa katiba ya Marekani.

Madison amekuliwa akichukuliwa kuwa ‘Baba wa Katiba’ kutokana na mchango wake mkubwa katika uandishi wa mwongozo wa taifa hilo na muswada wa haki za Marekani. 

Madison alikuwa mwandishi wa Magazeti ya Federalist pia miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha Democratic-Republican. Madison alianzisha chama hicho akiwa na Thomas Jefferson.

Pia katika utumishi wake nchini Marekani alikuwa Katibu Mkuu wa Tano wa taifa hilo kwa miaka minane kutoka mwaka 1801 hadi 1809. 

Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 85. Madison hakuwa na umbo kubwa, pia alikuwa na macho ya bluu ya kung’aa, alikuwa na msimamo imara, alikuwa akifahamika kwa uchangamfu akiwa na mikusanyiko midogo.

Aliugua sana wakati wa uhai wake kutokana na msongo wa mawazo. Hata hivyo alifariki dunia kutokana na kupatwa na hofu ya kuogopa kuumwa (hypochondriac) inaelezwa kuwa Madison alikuwa anaogopa sana kuumwa. Alipoumwa msongo wa mawazo uliofanya afya yake iteteleke.

Madison alizaliwa Machi 16, 1751 katika mashamba ya Belle Grove karibu na Port Conway, Virginia, kwa wazazi Madison Sr. na mama yake Nelly Conway. Familia yao iliishi huko Virginia tangu miaka ya 1600. 

Madison alikuwa mtoto wa kwanza kati ya 12 wa Mzee Madison Sr. alikuwa na kaka zake saba na dada sita. Kati ya hao ni sita tu waliofika utu uzima.

Baba yake alikuwa mkulima wa tumbaku katika mashamba ambako sasa kunafahamika kama Mount Pleasant. Alikuwa na watumwa 100 katika ekari 5,000. Madison Sr. alikuwa mmiliki mkubwa wa ardhi na alikuwa akiongoza huko Piedmont.

Babu wa upande wa mama yake mzee Madison Sr. alikuwa mkulima mahiri na mfanyabiashara maarufu wa tumbaku. Mapema mnamo mwaka 1760 familia ya Madison ilihamia katika nyumba mpya waliyojenga na kuipa jina la Montpelier. 

Zifahamu mbinu za kupunguza Kitambi

Kitambi ni mafuta ya ziada yanayojikusanya katika sehemu ya tumbo. Hii inatokana na kula chakula kingi na kisicho na ubora, pia kuishi maisha ya kibwanyenye yanayokunyima fursa ya kufanya mazoezi. Mafuta yanayofanya kitambi huweza kujengeka chini ya ngozi, au ndani kabisa ya tumbo yakizunguka viungo kama tumbo, utumbo na ini.

Mafuta haya, hususan yale yaliyo ndani ya tumbo ni hatari kwa afya zetu. Ikumbukwe pia kwamba, kitambi huwa na mwonekano wake kutokana na misuli ya tumbo kuwa legelege. Hii husababisha mafuta yaliyo tumboni kuusukuma ukuta wa tumbo kiurahisi hivyo kutengeneza shepu ya mbinuko.

PUNGUZA SUKARI NA VYAKULA VYA WANGA: Kutokula vyakula vya wanga kunasaidia kupunguza njaa hivyo kunafanya upunguze kiasi cha chakula unachokula. Kwasababu miili yetu hutumia wanga kutengeneza nguvu ya kujikimu na shughuli zote za mwili, uhaba wa fungu hili la chakula mwilini husababisha miili yetu kutafuta mbadala wa kutengenezea hii nguvu kwa ajili ya uhai. Kwa hiyo miili yetu huamua kutumia glycogen na mafuta ambayo yanakuwa yametunzwa mwilini ambayo yanatufanya tuonekane wanene ili kutengeneza nguvu kwa ajili yetu. 

Mafuta yanapotumika kutengeneza nguvu badala ya wanga ndipo tutaona mabadiliko ya kupungua mwili.  Pia kupunguza vyakula vya wanga kunaleta kupungua kwa hormone ya insulin. Hii inasababisha figo kuondoa chumvi na maji mwilini hivyo kama tumbo limejaa linapungua haraka sana. Mara nyingi watu wanapata tumbo kujaa na wanadhani ni gesi tu inasababisha lakini kula vyakula vingi vya wanga na chumvi nyingi kunasababisha mwili ujae maji hivyo tumbo linakuwa limechomoza sana.

KULA PROTINI, MBOGA MBOGA NA MAFUTA YA MIMEA: Hakikisha kila mlo wako una protein, kuanzia chakula cha asubuhi!. Chai na chapati/maandazi/vitumbua/cutlets/mihogo/viazi/keki n.k achana navyo kabisa. Kila mlo lazima uwe na protein na mbogamboga. Mfano wa vyakula vyenye protini; Nyama: Ya ng’ombe, kuku, mbuzi n.k Samaki: Salmon, sato, sangara, prawns n.k Mayai: Ya kuku wa kienyeji ni mazuri zaidi; Mbegu na karanga: Mbegu za chia, karanga za almonds. Utajisikia kushiba kwa muda mrefu, hamu ya kula kula hovyo au kula usiku wa manane vitapungua sana hivyo kukufanya kula kwa kiasi.

FANYA MAZOEZI YA KUNYANYUA UZITO: Ukipunguza vyakula vya wanga ni muhimu kutopunguza mafuta aina hii, ukipunguza mafungu haya mawili ya chakula kwa wakati mmoja utapata tabu sana na hautafurahia healthy lifestyle yako. Utachoka na kukosa nguvu muda mwingi kwahiyo usisahau kutumia healthy fats kwenye milo yote. Kufanya mazoezi ya weight lifting matokeo yatakuwa makubwa zaidi. Kama hauwezi kunyanyua uzito basi unaweza kufanya mazoezi ya cardio kama jogging, kuendesha baiskeli, kuogelea, n.k Utaongezeka uzito kidogo tu ambao unasababishwa na maji kwasababu kula vyakula vya wanga kunafanya mwili ushikilie maji mengi, ukipunguza tena vyakula hivi figo itatoa hayo maji na huo uzito kidogo ulioongezeka utatoka. Kwa hiyo usiogope/usishtuke/usishangae! Ni kitu rahis tu. Jitahidi kujidhibiti (self control) usipitilize siku moja tu ya kula hivi vyakula vya wanga, na pia usifanye maajabu kwa kula hadi kupitiliza kama kulipizia. Ni muhimu kujifunza kuwa na kiasi. Kula kadri ya mahitaji usipitilize.

KULA TARATIBU: Hili huwa linawashinda wengi hususani jamii ya Watanzania kutokana na kushindwa kupangilia vizuri ratiba ya kula na hujikuta kazi zimembana na hatimaye kula haraka haraka. Imekuwa ni tabia ambayo imekuwa ikichukuliwa kama mtu huyu anajali sana muda kwa kulak wake haraka jambo ambalo sio kweli. Kula taratibu kunasaidia kumeng’enya chakula chako vizuri lakini pia kunafanya ule chakula kidogo na kushiba haraka.

PATA USINGIZI WA KUTOSHA: Kupata Usingizi wa kutosha kutakuepusha na kutaka kula chakula usiku sana, unapowahi kulala unawahi kula hii inasaidia mmeng’enyo wa chakula kufanya kazi yake vizuri.

KUNYWA MAJI: Mara nyingi wengi wamekuwa wavivu kunywa maji, lakini ukiwa unakunywa maji mengi/mara kwa mara kwa siku itakusaidia kutosikia njaa, hii itakufanya uwe mbali na vyakula hususani vyakula vya hapa na pale pia maji yanasaidia kufanya ngozi iwe nyororo. Unaweza kuongezea vitu kama limao, tango, tangawizi katika maji unayokunywa

Black Death: Janga kubwa kuitesa Ulaya

Black Death ni janga la pili kubwa kulikumba bara la Ulaya katika kipindi cha kati, janga la kwanza ilikuwa ni njaa. Black Death ilitokea kati ya mwaka 1346 hadi 1353.

Inakadiriwa kuwa ugonjwa huo uliua asilimia 30 hadi 60 ya watu barani Ulaya. Kwa ujumla ugonjwa huo wa tauni ulipunguza idadi ya watu hapa ulimwenguni wakati huo kutoka milioni 475 hadi milioni 350 katika karne hiyo ya 14. Watu wapatao milioni 75 hadi 200 walifariki dunia kutokana na ugonjwa huo wa tauni barani Ulaya.

Mnamo Oktoba mwaka 1347 ugonjwa wa tauni ulifika barani Ulaya baada ya meli 12 kutoka Bahari Nyeusi zilipotia nanga katika bandari ya Messina huko Sicily nchini Italia. Watu walistaajabishwa na walichokiona siku hiyo kwani ilikuwa ni hali ya kuogofya.

Wengi wa manahodha na baadhi ya watu walikuwa wamefariki dunia na wachache wakiwa hai lakini wakiwa hoi.  Miili ya waliokufa ilikuwa ikivuja damu na usaha ikitoa halafu mbaya.

Mamlaka za Sicily ziliamuru meli hizo zitokea katika bandari hiyo lakini amri hiyo ilikuwa imechelewa. Miaka mitano baadaye watu wapatao milioni 20 barani Ulaya walipoteza maisha, ikiwa ni theluthi moja ya watu wa bara hilo.

Ugonjwa wa tauni unafikiriwa kuwa asili yake ni barani Asia ambako miaka zaidi ya 2000 ulianza na kusambaa kwake kulitokana na biashara ambayo ilikuwa ikifanyika kupitia njia ya Mashariki ya kati hadi Mashariki ya mbali kwa kutumia meli. 

Tafiti mbalimbali za miaka ya hivi karibuni zinaonyesha kuwa ugonjwa huu ulianza barani Ulaya mapema mwaka 3000 KK. Katika miaka ya mwanzoni ya 1340 tauni ilizikamata China, India, Uajemi, Syria na Misri.

Inaelezwa kuwa meli zile zilipotia nanga viroboto walionekana katika meli hiyo na kwamba walikuwa wakiishi kwenye panya weusi ambao walijificha kwenye meli za wafanyabiashara wa Genoa.

Pia tauni  hiyo ilizigusa baadhi ya sehemu barani Afrika hususani zilikuwapo katika mwambao wa bahari ya Mediterania. 

Saturday, June 27, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Joe Jackson ni nani?

Juni 27, 2018 alifariki meneja mwenye kipaji na mwangalizi wa familia ya Jackson ambayo ilikuwa na watoto vipaji katika muziki kama Michael na Janet raia wa Marekani Joe Jackson. 

Juni 22, 2018 iliripotiwa na mtandao wa TMZ kuwa Jackson amelazwa katika hospitali moja mjini Las Vegas kutokana na maradhi ya saratani ya kongosho. Hali yake ilikuwa mbaya kwani saratani hiyo ilikuwa imeshambulia kwa kiasi kikubwa.

Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 89 siku mbili tu baada ya kumbukizi ya tisa ya kifo cha mtoto wake Michael Jackson huku ikiwa ni siku 30 kabla ya kufikisha miaka 90.

Alifariki dunia kwa amani akiwa amezungukwa na mkewe na watoto wake. Jackson aliingizwa katika Jumba la Wakongwe wa muziki wa Rhythm na Blues mnamo mwaka 2014.

Jackson alikuwa na ndoto ya kuwa mpiganaji wa masumbwi  na baadaye alianza na kadhia hiyo na kuanza kupiga gitaa akiwa na kundi la The Falcons. Akiwa huko aligundua kwamba ana watoto ambao wana vipaji vya muziki huku akimwona kwa ukamilifu mwanaye Michael Jackson.

Baada ya hapo alipambana hadi kuunda miongoni mwa makundi makubwa ya pop ‘The Jackson Five’ ambalo liliweka wazi kipaji cha mwanaye huyo na binti yake Janet.  Mzee huyo aliwahi kunyoshewa kidole cha lawama na watetezi wa haki za watoto kwamba aliwatesa watoto wake, madai hayo aliwahi kuyasema pia Michael Jackson katika kitabu chake.

Hata hivyo Janet aliwahi kumtetea baba yake kuwa alikuwa akifanya hivyo kwani alikuwa anataka wawe bora zaidi. Janet alisema hata kama hakutumia wakati mwingine njia sahihi lakini ndiye anasalia kuwa msingi wa mafaniko yao.

Mwanaye mwingine La Toya alikaririwa akisema, “Siku zote nitakupenda wewe! Ulitupa uimara, ulitufanya kuwa miongoni mwa familia maarufu sana hapa ulimwenguni. Hakika ninakukubali, sitasahau nyakati tulizokuwa pamoja na namna ulivyokuwa ukiniambia na kunijali.”

Jina lake halisi ni Joseph Walter Jackson. Alizaliwa huko Fountain Hill Arkansas Julai 26, 1928. Alikuwa mtoto mkubwa kati ya wanne wa Samuel Joseph Jackson (1893-1993) aliyekuwa mwalimu wa shule na mama Crystal Lee King (1907-1992).

Alipokuwa na miaka 12 wazazi wake walitengana na baba yake akaenda zake Oakland, California. Akiwa na umri wa miaka 18 alikwenda kuishi huko Indiana karibu na mahali alipokuwa akiishi mama yake East Chicago.

Joe Jackson alifanikiwa kuzaa watoto 11 miongoni mwa hao 10 ni kutoka kwa Katherine Scruse.  

Watoto hao ni Maureen Reillette "Rebbie" Jackson (Mei 29, 1950), Sigmund Esco "Jackie" Jackson (Mei 4, 1951), Toriano Adaryll "Tito" Jackson (Oktoba 15, 1953), Jermaine La Jaune Jackson (Desemba 11, 1954), LaToya Yvonne Jackson (Mei 29, 1956), Marlon David Jackson (Machi 12, 1957), Brandon David Jackson (Machi 12, 1957 - Machi 12, 1957), Michael Joseph Jackson (Agosti 29, 1958 – Juni 25, 2009), Steven Randall "Randy" Jackson (Oktoba 29, 1961), Janet Damita Jo Jackson (Mei 16, 1966) na Joh'Vonnie Jackson (Agosti 30, 1974). 

Friday, June 26, 2020

Mfahamu Zolile Hector Pietersen katika Mauaji ya Soweto 1976

Picha maarufu ya Mauaji wa Soweto ilipigwa na mwandishi wa habari Sam Nzima ambaye kwa sasa hatunaye ulimwenguni alifariki dunia mnamo Mei 12, 2018 katika Hospitali ya Rob Ferreira, Nelspruit, nchini Afrika Kusini akiwa na miaka 84. Picha hiyo imekuwa ikifahamika kwa jina la ‘Hector Pietersen’.

Story ya mtoto huyo inaanza hivi; Jina lake halisi mtoto huyo ni Zolile Hector Pietersen. Hata hivyo jina halisi la ukoo wake ni Pitso, lakini familia hiyo ililazimika kubadili na kuwa Pietersen ili kuendana na falsafa ya ubaguzi wa rangi nchini humo, na kujihisi kama wao ni makaburu ilhali wakiwa ni weusi. Familia hiyo iliamua kufanya hivyo ili kukwepa dhuluma za makaburu. Hata jina la Zolile lilifutwa kwa muda ili apate nafasi ya kusoma.

Zolile alizaliwa Agosti 19,1963 mjini Soweto nchini Afrika Kusini wakati falsafa ya ubaguzi wa rangi ikiwa imepamba moto. Falsafa ya ubaguzi wa rangi ilikuwa ikijulikana kama Apartheid, ambayo ilikuwa ikiendeshwa na makaburu waliokuwa wakitawala nchi ya Afrika Kusini.

Zolile alikuwa akihudhuria shuleni kwa taabu hasa alipokuwa akipita sehemu mbalimbali ili kuelekea shuleni. Alipita kwa wasiwasi mkubwa akiwa na hofu ya kufyatuliwa risasi. Baadae alizoea hali ya milio ya risasi mara kwa mara katika mji wa Soweto.

Alikuwa akienda shuleni mara nyingi akiambatana na dada yake Antoinete Sithole pamoja na rafiki yao kipenzi Mbuyisa Makhubo. Mbuyisa Makhubo alimtangulia Zolile Hector Pietersen miaka mitano kuzaliwa, hivyo alimchukulia kama kaka yake. Watatu hao walikuwa na furaha wanapokutana na kuzungumza pamoja na vilevile wakati wa shida hawakukosa kuwa pamoja ilipobidi.

Serikali ya Makaburu nchini Afrika Kusini iliweka utaratibu wa 50/50 katika mitaala yote hasa katika elimu ya msingi na sekondari. Kulikuwa na masomo muhimu zaidi ambayo yalikuwa yakifundishwa kwa lugha ya kiingereza, na yale ambayo hayakuwa na umuhimu sana yalikuwa yakifundishwa katika lugha ya Kiafrikaan. Na mitihani ilikuwa ikitolewa kulingana na lugha husika inayotumika kufundishia katika somo husika.

Mnamo Juni 16, 1976, Zolile, Antoinete Sithole pamoja na rafiki yao kipenzi Mbuyisa o walipokuwa shuleni wakihudhuria masomo walifikwa na wakati mgumu walipoanza kugoma kufundishwa masomo kwa lugha ya Kiingereza badala ya lugha yao mama ya Kiafrikaan. Ndipo polisi wa makaburu walipoanza vurugu ya kuwashambulia wanafunzi pamoja na watu wengine.

Wanafunzi walikusanyika pamoja kwa amani na kueleza kile walichokuwa wakikipinga katika taaluma. Muda mfupi baadae, mkusanyiko wa wanafunzi hao wakiwemo Zolile, Antoinete na Mbuyisa, ulishambuliwa mara tu polisi walipowasili shuleni hapo. Ndipo wanafunzi hao walianza kuokota mawe na kuwarushia polisi wa makaburu waliofika kuwatawanya kwa risasi.

Mkusanyiko wa wanafunzi hao ulikuwa na wanafunzi yapata 13,000 pamoja na wafanyakazi weusi wa shule hiyo ambapo katika wafanyakazi wa shule hiyo, wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wa Makaburu. Kwa ghadhabu, wanafunzi waliongeza fujo ili kutetea haki ya kitaaluma waliyokuwa wakiidai na vilevile kulinda utu wao. Walichoma magari kadhaa moto na majengo. Pia walilishambulia jengo la kiengo cha Elimu mkoa wa Transvaal.

Wanafunzi 30 walikusanyika nje ya shule ya sekondari ya Phefeni wakiwa wanaimba wimbo mkuu wa Kisotho. Polisi walipowasili katika shule hiyo, mkusanyiko huo nao ulishambuliwa na polisi hao ambapo wanafunzi nao walikuwa wakiwarushia mawe polisi.

Polisi walifyatua mabomu ya gesi inayoumiza macho na kutoa machozi kwa wanafunzi hao. Haijulikani nani alitoa amri ya kutumika kwa risasi za moto kuwafyatulia mkusanyiko ule wa wanafunzi. Wanafunzi hao walianza kukimbia na kutawanyika ovyo ili kuokoa maisha yao. Wengine walikuwa wakigaragara barabarani wakilalamika maumivu baada ya kupigwa risasi.

Zolile aliripotiwa kuwa mwanafunzi wa kwanza kufariki baada ya kuwasili katika zahanati akiwa na majeraha ya risasi.

Lakini pia mwanafunzi Hasting Ndlovu aliripotiwa kufariki kutokana na majeraha ya risasi alizopigwa na polisi wa Makaburu. Lakini kutokana na kutokuwepo kwa picha iliyopigwa ya Hastings Ndlovu, imehesabiwa kuwa mwanafunzi aliyewapa simanzi watu wengi nchini Afrika kusini ni Zolile.

Zolile alipigwa risasi akiwa na dada yake pamoja na rafiki yao kipenzi Mbuyisa Makhubo, alidondokea katika kona ya nyumba moja mpakani mwa mtaa wa Moema na mataa wa Vilakazi; Mbuyisa Makhubo alimnyanyua Zolile akiwa na dada yake Antoinete Sithole.

Zolile alibebwa na Mbuyisa Makhubo mpaka kwenye gari la mwandishi wa habari mweusi Sam Nzima na kumwingiza garini bila hata kuomba. Sam Nzima alipoona ujasiri wa Mbuyisa Makhubo akiwa na dada yake Zolie, alitoa kamera yake na kuwapiga picha walipokuwa wakisogea kwenye gari lake na kuamua kuwasaidia. Ndipo Zolile alipokimbizwa katika Zahanati ya Phenfeni. 

Gari lilikuwa likiendeshwa na mwandishi wa habari Sophie Tema ambaye aliambatana na Sam Nzima. Muda mfupi baada ya kumkabidhi Zolile kwa wahudumu wa afya ilitangazwa kwamba amefariki. 

MAKTABA YA JAIZMELA: Nasir al-Din al-Tusi ni nani?

Juni 26, 1274 alifariki dunia msomi na mwanazuoni wa Kiajemi Nasir al-Din Al-Tusi. Jina lake halisi ni Khawaja Muhammad ibn Muhammad ibn Hasan Tūsī.

Amekuwa akichukuliwa kuwa ni msanifu, mwanafalsafa, mwanafizikia, mwanasayansi na mwanatheolojia wa Kiajemi.

Nasir al-Din alikuwa miongoni mwa wanasayansi wakubwa katika kipindi cha kati cha Uislam. Na amekuwa akichukuliwa kuwa ndiye mvumbuzi wa Trigonometriki katika masuala ya Hisabati.  

Nasir al-Din alifanya kazi 150, miongoni mwa hizo zipatazo 25 aliziandika kwa lugha ya kiajemi na zilizobaki ziliandikwa kwa lugha ya Kiarabu.

Pia kuna moja ambaye iliandikwa kwa lugha tatu ya Kiajemi, Kiarabu na Kituruki. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 huko Al Yassin Mosque, Baghdad, Iraq. Nasir al-Din alipendelea pia kutunga mashairi miongoni mwa mistari katika mashairi yake ni “Yeyote ambaye hajui, na kwamba hajui kuwa hajui ni wazi kwamba milele yote atakwama kwenye ujinga mara mbili.”

Mara kadhaa mchango wake umetambuliwa na wasomi mbalimbali ambapo katika mbalamwezi upande wa kusini kuna crater ambayo ina kipenyo cha kilometa 60, kwa heshima ya Nasir al-Din eneo hilo limetajwa kwa jina lake kama ‘Nasireddin’. 

Chuo kikuu cha Teknolojia cha K. N. Toosi nchini Iran kimetajwa kwa heshima yake.

Pia Observatory of Shamakhy huko Jamhuri ya Azerbaijan imetajwa kwa heshima yake. Nchini Iran kumbukizi ya kuzaliwa kwake imekuwa ikisheherekewa na kama Siku ya Mhandisi. Nasir al-Din alizaliwa Februari 18, 1201 huko Tus, katika jimbo la Khorasan karibu na Mashhad.

Huko Mashhad kuna sanamu ya Nasir al-Din kutokana na mchango wake katika sayansi, unajimu, kemia, fizikia na hisabati.

Alizaliwa katika familia ya Kishia, akiwa bado mdogo alimpoteza baba yake.  Kwa ajili ya kutimiza kile ambacho baba yake alimtaka afanye Nasir al-Din alianza kujifunza kwa bidii. Alisafiri maeneo mbalimbali akifuatilia masomo ya walimu na kujipatia maarifa.

Alikuwa akifanya kwa bidii zote huku akitiwa moyo na imani yake katika Uislamu. Akiwa na umri mdogo alienda zake kaskazini Mashariki ya Iran katika mji wa Nishapur, ambako alijifunza falsafa chini ya uangalizi wa Farid al-Din Damad na Hisabati chini ya mwalimu Muhammad Hasib.

Akiwa Nishapur alikutana na mkongwe wa Kisufi Abū Ḥamīd bin Abū Bakr Ibrāhīm maarufu Attar wa Nishapur ambaye alikuja kuuawa na Wamongolia waliovamia mji  huo. Akiwa hapo alihudhuria masomo ya Qutb al-Din al-Misri.

Mnamo mwaka 1242 alienda zake kaskazini mwa Iraq katika mji wa Mosul uliopo kaskazini ya Baghdad yapata kilometa 400 ambako alisomea Unajimu na Hesabu pamoja na Kamal al-Din Yunus, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Sharaf al-Dīn al-Muẓaffar. Baadaye alijumuika na mwanafalsafa wa Kisufi Sadr al-Din al-Qunawi.

Wakati huo wote jamii yao ilikuwa ikivamia sana na Wamongolia kutoka Mongolia na China.

Hata hivyo Nasir al-Din alifanikiwa kuweka mizizi yake na kuwa miongoni ya watu waliochangia pakubwa katika medani ya sayansi na falsafa.

Thursday, June 25, 2020

Chanzo cha Sera za Ubaguzi wa Rangi (Apartheid) Afrika Kusini

Chanzo cha Afrika Kusini kama nchi ni Rasi iliyoundwa na Waholanzi katika eneo la Cape Town. Huko kabila jipya la Makaburu lilijitokeza kati ya walowezi Wazungu kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani. Lugha yao ilikuwa Kiholanzi iliyoanza kuchukua maneno ya Kifaransa, Kiafrika na Kiingereza na kuendelea kuwa lugha ya pekee Kiafrikaans.

Karne za kwanza za koloni la Kiholanzi ziliona pia kufika kwa watumwa kutoka Indonesia walioletwa kama wafanyakazi wa Waholanzi na Makaburu. Hao Waindonesia walikuwa chanzo cha jumuiya ya Uislamu kwenye rasi hiyo.

Pia machotara walitokea kutokana na kuzaliana kati ya Makaburu na wanawake Waafrika na Waindonesia. Sehemu ya machotara hao wameingia katika jumuiya ya Makaburu na wengi wao wanapimwa kuwa na mababu Waafrika.

Katika miaka iliyofuatia ubaguzi wa rangi uliongezeka na watoto machotara wa Wazungu na Waafrika mara nyingi hawakukubalika; walianza kuishi kama kundi la pekee kati ya Waafrika na Wazungu, nao ni chanzo cha hao walioitwa baadaye "Cape Coloreds".

Mwaka 1814 Rasi ya Tumaini Jema (Good Hope) ilitwaliwa na Waingereza na kuwa sehemu ya Milki ya Uingereza. Utawala wa Waingereza ulisababisha uhamisho wa nje wa sehemu ya Makaburu waliotokana na Wazungu kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani; Makaburu hao walihama kwenda kaskazini wakaanzisha jamhuri ndogo kati ya maeneo ya Waafrika ama kwa njia ya mapatano au kwa njia ya vita.

Kati ya miaka 1840 na 1850 Waingereza waliwafuata Makaburu kwa kuenea kutoka maeneo yao hadi mto Oranje; waliteka Jamhuri ya Kikaburu ya Natalia na kuanzisha koloni jipya la Natal.

Jamhuri mbili za Makaburu ziliweza kustawi kwa miaka kadhaa ambazo zilikuwa jamhuri ya Dola Huru la Oranje upande wa kaskazini wa mto Oranje na Jamhuri ya Transvaal (ilijiita pia Jamhuri ya Kiafrika ya Kusini) upande wa kaskazini wa mto Vaal.

Milki za Kiafrika zilitafuta njia zao kati ya himaya hizi za Wazungu ambao walikuwa na nguvu kutokana na silaha za kisasa. Wengine walitafuta uhusiano mzuri na Makaburu na kushikamana nao; wengine waliona Makaburu kama hatari wakatafuta uhusiano wa ulinzi na Waingereza.

Mikataba kati ya Waingereza na milki za Kiafrika iliunda nchi lindwa zinazoendelea hadi leo kama nchi huru kama vile Botswana (Bechuanaland), Lesotho (Basutoland) na Uswazi (Swaziland).

Katika miaka ya 1880 almasi na dhahabu zilipatikana kwa wingi katika Jamhuri hizi na kusababisha kufika kwa wachimbamadini wengi, hasa Waingereza, waliotaka kutajirika; Makaburu walisita kuwapa haki za kiraia kwa sababu waliogopa wageni wengi. Tatizo hilo lilisababisha vita vya Makaburu dhidi ya Uingereza na Jamhuri za Makaburu zilitwaliwa na jeshi la Kiingereza hadi mwaka 1902 zikawa makoloni.

Jitihada za kupatanisha Wazungu wa Afrika Kusini (yaani Waingereza na Makaburu) zilisababisha kuundwa kwa Muungano wa Afrika Kusini kama nchi ya kujitawala ndani ya Milki ya Uingereza. Waafrika kwa jumla hawakuwa na haki za kiraia katika nchi hiyo isipokuwa katika Jimbo la Rasi kama walikuwa na elimu na mapato ya kulipa kodi za kutosha.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia Chama cha National kilichofuata itikadi kali kilipata kura nyingi na kuchukua serikali ya Afrika Kusini. Hapo kilianzisha mfumo wa ubaguzi wa rangi kwa jina la apartheid.

Haki za wasio Wazungu zilipunguzwa zaidi. Maeneo ya Kiafrika yalitangazwa kuwa nchi za pekee chini ya usimamizi wa serikali ya Kizungu ya Afrika Kusini; kwa hiyo wananchi kutoka maeneo hayo hawakuwa tena na haki za kukata rufaa mbele ya mahakama; walipewa vibali vya muda tu kukaa kwenye miji. Waafrika walipaswa kutembea muda wote na pasipoti na vibali; ndoa na mapenzi kati ya watu wa rangi tofauti zilipigwa marufuku. Shule na makazi zilitenganishwa.

Siasa hiyo ilisababisha mafarakano kati ya nchi nyingi za dunia na Afrika Kusini. Upinzani kutoka Uingereza na Jumuiya ya Madola ulisababisha kuondoka kwa Afrika Kusini katika jumuiya hiyo na kutangazwa kwa Jamhuri ya Afrika Kusini.

Wenyeji wa taifa hilo ambao hawakupewa haki zao walianzisha ghasia ikiwa ni sehemu ya kupaza sauti ya kutaka haki zao. Lakini ziliwagharimu wengi wao walipoteza maisha kwani mamlaka za serikali hazikuwaacha kirahisi. Wengine walitupwa jela na kutumikia vifungo mbalimbali.

Mauaji ya Sharpville ya Machi 21, 1960 ni miongoni mwa vuguvugu za kupinga sera hizo za kibauguzi nchini Afrika. Tukio hilo lilionyesha mwanzo wa upinzani wa silaha nchini Afrika Kusini, na kushawishi ulimwengu kupinga sera za ubaguzi wa Afrika Kusini.

Waafrika wapatao 180 walijeruhiwa (kuna madai kuwa walikuwa zaidi ya 180) na 69 waliuawa wakati polisi wa Afrika Kusini walitumia silaha kuwazuia waandamanaji wapatao 300, ambao walipinga sheria hizo, katika mji wa Sharpeville, karibu na Vereeniging huko Transvaal.

Katika maandamano kwenye kituo cha polisi huko Vanderbijlpark, mtu mwingine alipigwa risasi. Baadaye siku hiyo hiyo huko Langa, nje ya Cape Town, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji waliokusanyika, wakipiga risasi tatu na kujeruhi wengine kadhaa.

Mauaji ya Soweto ya Juni 16, 1976 ni miongoni kati ya harakati za kupinga sera za kibaguzi nchini Afrika kusini zilizopitishwa Juni 24, 1950.

Machafuko hayo yalisababisha kiasi ya watu 170 kuuawa, yalikuwa ni hatua muhimu ya mabadiliko katika harakati za kukabiliana na siasa za ubaguzi wa rangi, kuyaeleza mataifa juu ya utawala wa kikandamizaji, lakini pia yalifungua njia ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka 1994, ambapo Nelson Mandela, alichaguliwa Rais wa kwanza mwafrika kuongoza nchi hiyo.

MAKTABA YA JAIZMELA: Michael Jackson ni nani?



Juni 25, 2009 alifariki mfalme wa Pop raia wa Marekani Michael Jackson. Jackson alifariki dunia mwaka 2009 akiwa na miaka 50 kutokana na kuzidisha madawa. Alizikwa huko Forest Lawn Memorial Park, Glendale jimboni California.

Michael Jackson alizaliwa Agosti 29, 1958, huko Gary katika Jimbo la Indiana. Jackson alikuwa ni mtoto wa nane kati ya kumi wa Mzee Joe Jackson na Catherine Jackson, alikuwa na dada zake watatu  ambao ni Rebbie, La Toya na Janet, pia kaka zake ni Jackie, Tito, Jermaine, Marlon, Randy, na ndugu yake mwingine anayeitwa Brandon alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Alianza kuimba akiwa umri wa miaka mitano akiwa na kundi la Jackson 5, kundi la kifamilia kwani waimbaji wote katika kundi hilo walikuwa ni ndugu zake wa damu, kundi hilo lilifanya vizuri sana nchini Marekani na dunia nzima kwa ujumla.

Jackson hakuwa na mahusiano mazuri na baba yake aliwahi kusema kuwa alikuwa na kawaida ya kumchapa Michael wakati akiwa mtoto, na Michael aliwahi kulalamika kuwa baba yake alikuwa akimnyanyasa kwa kumpiga hasa wakati wa mazoezi ingawa aliwahi kukiri kuwa baba yake alichangia kwa kiasi kikubwa yeye kupata mafanikio.

Mnamo mwaka 1968 Boby Taylor na The Vancouver waliligundua Kundi la Jackson 5 ambapo kundi hilo liliingia mkataba na Motown Records na walifanikiwa kurekodi nyimbo zilizotisha enzi hizo kama ABC, I Want u Back, I’ll be there na nyinginezo, walirekodi albamu 14 na Motown na Michael alirekodi albamu nne za solo.

Jackson 5 walikaa na Motown mpaka ilipofika mwaka 1976 ambapo walidai wanataka uhuru wa kisanii na baada ya hapo wakaenda kusign na Epic, na kundi hilo lilibadilisha jina kutoka The Jackson 5 na kujiita The Jacksons na walirekodi albamu sita kati ya mwaka 1976 hadi 1984.

Mnamo mwaka 1977 Michael Jackson alikutana na mtaarishaji wa muziki maarufu enzi hizo Quincy Jones chini ya Epic Records akarekodi albamu inayoitwa Off the Wall, ambayo ilifanya vizuri katika chart za nchi Marekani.

Mnamo 1982 Wacko Jacko aliachia albamu ambayo ambayo iliuza sana kuliko album yoyote duniani, inaitwa Thriller, ndani ya albamu hii kulikuwa na Single 7 ambazo ziligonga vichwa vya watu sana dunia nzima, zaidi ya copy milioni 50 ziliuzwa, alifanya kazi na waandaji bora na waongozaji wazuri kufanikiwa kutengeneza Music video ya Thriller ambayo mpaka leo bajeti ya kutengeneza music video hiyo bado ni gumzo.

Ilipofika 1984 Jackson alivunja rekodi kwa kutunukiwa tuzo 8 za grammy ndani ya usiku mmoja, tuzo hizo zilitokana na Albamu yake ya Thriller na kitabu cha “T story book.” Desemba 9, 1984 katika concert ya mwisho ya Jackson 5 iliyoitwa Jackson Victory Tour, Wacko Jacko akatangaza kuwa anajitoa kutoka kundi hilo na atakuwa anafanya kazi zake binafsi.

Mnamo mwaka 1987 Michael Jackson akaachia albamu yake iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wake album inaitwa BAD na kuvunja rekodi ya Tour za msanii mmoja mmoja yaani Solo, kwani show zake zilikuwa zikihudhuriwa na maelfu ya watu kila nchi aliyokanyaga.

Mwaka 1988 kwa mara ya kwanza aliandika Autobiography yaani kitabu ambacho alizungumzia maisha yake kutoka utotoni na kazi yake ya muziki, Autobiography hiyo iliitwa Moon Walk.