Thursday, January 9, 2020

Sintofahamu Marekani-Iran yapandisha mafuta ghafi


Gharama za mafuta zimepanda baada ya kambi mbili za majeshi ya Marekani nchini Iraq kushambuliwa na makombora.

Gharama za mafuta ghafi zimepanda kwa 1.4% kwa dola 69.21 za Marekani kwa pipa moja.

Wakati huo huo gharama za mafuta kwenye soko la dunia zilishuka kutokana na mzozo wa Mashariki ya kati.

Televisheni ya Taifa ya Iran ilisema kuwa shambulio lilikuwa ni kisasi baada ya kuuawa kwa kamanda wa juu wa jeshi la nchi hiyo Qasem Soleimani.

Shambulio lilitokea saa chache baada ya shughuli za mazishi ya Soleimani, aliyeuawa na shambulio la Marekani siku ya Ijumaa.

Kifo chake kilisababisha wasiwasi kuwa mzozo kati ya Marekani na Iran unaweza kuwa mkubwa zaidi.

Hali hii inaelezwa kuwa inaweza kuathiri usafirishaji wa mafuta kupitia lango la Hormuz linalotenganisha ghuba ya uajemi na ghuba ya Oman. Takribani moja ya tano ya mafuta duniani husafirishwa kupitia lango hilo linalounganisha eneo la ghuba na bahari ya Arabia.

Mlango wa Hormuz ni muhimu kwa wasafirishaji wakubwa wa mafuta katika eneo la ghuba - Saudi Arabia, Iraq, Umoja wa falme za kiarabu na Kuwait- ambao uchumi wao unajengwa kutokana na uzalishaji wa mafuta na gesi.

Iran pia inategemea kwa kiasi kikubwa njia hiyo kwa ajili ya kusafirisha mafuta.

Qatar, mzalishaji mkubwa duniani wa gesi, husafirisha karibu gesi yake yote kupitia lango hilo.

CHANZO: BBC Swahili

0 Comments:

Post a Comment