Malameni Rock at Mbaga, Same. |
Utamaduni ni jumla
ya mambo yote yaliyobuniwa na jamii ili kukidhi utashi na maendeleo yake.
Kwa maneno mengine
utamaduni ni mwenendo wa maisha ya jamii, mtazamo wao wa mambo na taratibu zao
za kuendesha maisha zinazowatofautisha wao na jamii nyingine.
Utamaduni ndicho
kitambulisho kikuu cha taifa na ni ikielelezo cha utashi na uhai wa watu wake.
Nguzo za Utamaduni ni pamoja na mila na desturi, lugha, michezo na historia.
Kwa mfano katika
baadhi ya mila na desturi za makabila mtoto akizaliwa hakuna mtu anayeruhusiwa
kumwona mtoto huyo.
Kwa kawaida, mtoto huwekwa ndani ya nyumba nao watu wasio
washiriki wa familia hawaruhusiwi kumwona mpaka baada ya sherehe ya kumpa jina.
WILAYA YA SAME,
KILIMANJARO
WILAYA ya Same ipo
Mkoa wa Kilimanjaro umbali wa kilometa 105 kutoka Moshi yalipo Makao Makuu ya
Mkoa.
Ni kati ya Wilaya 6
za Mkoa wa Kilimanjaro. Wilaya ya Same ilianzishwa mwaka 1962.
Kwa mujibu wa
makadirio ya mwaka 2017; Wilaya ya Same inakadiriwa kuwa na Wakazi wapatao
296,287 na idadi ya kaya zipatazo 65,842
Wilaya ya Same ipo
katikati ya Latitudo 040 04’006 Kaskazini hadi 040 04’456 Kusini na Longitudo
370 04’87 Mashariki hadi 380 04’897 Magharibi.
Hali ya hewa ya
wilaya ina kiwango kati ya nyuzi joto 15 hadi 30 na kiwango cha mvua cha
wastani wa kati ya lita za ujazo 500 hadi 2,000 kwa mwaka.
Kiikolojia Wilaya
imegawanyika katika kanda tatu nazo ni; ukanda wa juu ambao ni milimani.
Eneo linalofaa kwa
kilimo cha tangawizi, kahawa, ndizi, maharage, miwa, miti (kwa ajili ya mbao/
boriti/kuni) matunda mbalimbali kama mapapai, na maparachichi.
Ukanda wa kati na ukanda wa chini ambao ni tambarare. Ukanda
wa tambarare katika wilaya ya Same una hali ya kijangwa na makazi mtawanyiko
kwa wakazi wanaojishughulisha na ufugaji.
Hifadhi ya Mkomazi
Hifadhi ya Mkomazi ilianzishwa mwaka 1951 kama Pori la Akiba la Mkomazi –umba,
kutoka katika Pori Tengefu la Ruvu na lina ukubwa wa kilometa za mraba, 3600,
Pori hilo la Akiba lilipandishwa hadhi na kuwa hifadhi ya Taifa (National
Park).
Hifadhi iko ndani ya
mikoa ya Kilimanjaro katika Wilaya ya Same kwa asilimia 61 na Wilaya ya Lushoto
mkoani Tanga kwa asilimia 39 na ukubwa wa hifadhi nzima ni kilometa za mraba
3245.
HISTORIA YA KABILA
LA WAPARE
Wapare ni kabila
kutoka milima ya Pare, Mkoa wa Kilimanjaro, kaskazini mwa nchi ya Tanzania.
Kabla ya kuingia huko, inasemekana walikuwa Taveta, Kenya, kwa zaidi ya karne
moja iliyopita na wakati huo walikuwa wakijulikana kwa jina la Waasu.
Masimulizi yanasema
walipoingia Tanganyika, walitamani kufanya makao yao kwenye miteremko ya Mlima
Kilimanjaro, lakini wakavurumishwa na wenzao waliokuwepo kabla yao, yaani Wachagga.
Wachagga hao
hawakuwa radhi kuwaruhusu Wapare kuwa na makazi eneo hili, hivyo waliwafukuza
kwa kupigana kama ilivyokuwa tabia ya makabila mengi hapo zamani.
Wakati wa kupambana
walikuwa wakiambiana, “Mpare… Mpare” wakimaanisha ‘Mpige…Mpige!’ Waasu hawa
wakatimka mbio na kuparamia milima ambayo sasa inaitwa milima ya Upare. Waasu
wakaanza kuitwa Wapare kwa maana ya "Wapige".
Hizi ni hadithi
zinazosimuliwa na baadhi ya Wachagga ambao ndio watani pekee wa Wapare, utani
uliozaliwa baada ya purukushani hizo za kuingia Tanganyika.
Hata hivyo, hakuna
hata Mpare mmoja anayeafiki maelezo hayo, isipokuwa wanakiri kuwa walitokea
Taveta: ndiyo maana hata baadhi ya maneno na lafudhi yao haiko mbali sana na
watu wa Taveta.
Zamani Wapare
walikuwa na sala tofauti kwa kila ukoo na eneo lao la tambiko.
Katika karne ya 19
hadi 20 wamisionari wa Ukristo waliingia maeneo mengi ya Upare.
Imani za Wapare kwa
sasa zinatofautiana kutokana na maeneo: walio kusini mwa wilaya ya Same katika
maeneo ya Ndungu, Kihurio, Bendera, Hedaru, Makanya, Suji, Chome, Tae, Gonja,
Mamba hadi Vunta kuna waumini wa kanisa la Sabato wengi sana.
Maeneo kama Chome,
Mbaga, Gonja, Vudee yana waumini wengi wa Kanisa la Kilutheri.
Katika Wilaya ya
Mwanga kuna idadi kubwa ya Walutheri na Waislamu.
Wakatoliki, japo ni
wachache, wanapatikana zaidi katika maeneo ya Kisangara Juu, Vumari na Mbaga.
MWAMBA WA
MALAMENI ULIVYO
Kimbwereza akitoa maelezo kuhusu Malameni Rock. |
Petrolojia ni tawi
la jiolojia ambalo linasoma miamba na masharti ambayo huyaunda. Petrolojia ina
sehemu ndogo tatu: igneous, metamorphic, na petrology sedimentary.
Hivyo basi muundo wa
Malameni Rock, ni mwamba mgando au mgumu au moto (igneous). Sifa za miamba hii
ambayo kipetrolojia ilitokana na kupoa na kuganda kwa magma.
Hadi mwaka 1930 mila
na desturi za Wapare katika kuwatoa watoto wenye ulemavu wakidai kuwa ni
kuondoa mapepo ambayo yangeweza kuwasababishia laana na mikosi katika familia
hizo zilikuwa zikiendelea kufanya. Hii ikiwa ni kabla ya Wamishionari wa
Kikristo kuanza kueneza neno la Mungu katika milima hiyo ya Upareni.
Miaka ya mwishoni
mwa 1800 ukristo ulianza kupenya katika milima hiyo. Mchungaji mmoja kutoka
Leipzig aliyefahamika kwa jina Jacob Jenson Dannholz alijenga kanisa katika
kijiji cha Mbaga ambako Malameni Rock inapatikana kati ya mwaka 1908 hadi 1917.
Hadi sasa unapofika
katika Vilima vya Mbaga ili uweze kwenda kujionea namna mwamba huo ulivyo, ni
sharti upewe maelekezo na historia kuhusu Malameni Rock.
Kwa kifupi ni kwamba
Malameni Rock haipo mbali na Mapango ya Mghimbi ambayo nayo ya historia yake.
USHUHUDA WA
MCHUNGAJI MARTIN KOSMALLA
Ushuhuda huu ni wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Mchungaji Martin Kosmalla ambao aliuhifadhi kwa
njia ya maandishi mnamo mwaka 1932.
"Jana nilikuwa
nikiitwa na mwanamke mara mbilimbili. Niliambiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa na
maumivu makali na kwamba asingeweza kuzaa mtoto," anaanza Mchungaji
Kosmalla katika ushuhuda wake.
"Mtoto wako ni
mzima, anaishi, yu hai hajafa. Ndipo nilipoliona tabasamu nilikionekana kwa
mwanamke yule aliyejawa na huzuni na maumivu makali na alikubaliana na maneno
yangu."
Mchungaji Kosmalla
anasema baada ya tukio lile kupita siku ile, usiku wake akiwa nyumbani kwake
aligongewa na alipotoka nje alikutana na baba wa familia ya yule mwanamke
aliambiwa kwamba mkewe amejifungua mtoto wa kiume na kinachovutia zaidi hali
yake ya afya ilikuwa nzuri na mkewe anaendelea vizuri.
Mwanaume wa kabila
la Wapare anaweza akawa tajiri wa mifugo na mali nyingi lakini pasipokuwa na
watoto basi huonekana kama mtu maskini.
Hali hiyo huwekwa
msisitizo na methali mbalimbali, kwamba mwanaume tajiri bila watoto sifa zake ni bure na utajiri wake
ni nani atakayeulinda.
Mchungaji Kosmalla
anasema licha ya kuzaliwa kwa watoto lakini kwa kabila la Wapare kitu kingine
cha ziada huangaliwa ambacho ni afya ya mtoto huyo.
"Endapo
kutakuwa na hitilafu katika mwili wa mtoto, hofu huikumba familia yote na kifo
itakuwa ndio zawadi pekee mtoto huyo itamfaa," anasema Mchungaji Kosmalla.
Malameni Rock au
Mwamba wa Malameni uliopo katika kijiji cha Mbaga-Manka ndio mahali ambapo
watoto wasio na hatia walikuwa wakiuliwa kwa kuweka juu nyakati za usiku na
mama zao ambao huwanyonyesha na kuwabembeleza hadi usingizi utakapowashika
kisha kuwalaza hapo ili watakapozinduka wataviringika kutoka juu hadi chini na
ndio hadithi yao huishi palepale.
Mama zao baada ya
kuwabembeleza kuondoka hapo kwa machozi makubwa kwani hawatakuja kuwaona tena,
lakini yote hayo ni kwasababu ya ulemavu waliozaliwa nao.
Mchungaji huyo
anasimulia siku moja wakati akiendelea na huduma yake katika milima ya Pare
aliamua kuondoka na waamini wake kwenda katika mwamba ambao ulikuwa ukiangamiza
watoto wengi waliozaliwa wakiwa na ulemavu.
Mchungaji Kosmalla
anasema wakati wa kupanda kwenda katika mwamba huo walikuwa wakipanda taratibu
na kwa uangalifu mkubwa kutokana na mwinuko wake kuwa mkali ili waweze kufika
katika kilele cha mwamba huo na alisimama huko na kuwaambiwa waumini wake.
"Hapa ndio
mahali ambapo watoto wenye ulemavu, wasio na hatia walihukumiwa na mama mwenye
mtoto alikuwa akimbusu mtoto wake kwa mara mwisho na kumwacha hapa asimwone
tena kwani atakapozinduka katika usingizi ataviringika kutoka juu hadi chini na
kupoteza maisha."
DHANA YA ULEMAVU KWA
WATOTO ILIVYOJENGEKA
Muongozaji wa watalii kujionea vivutio Eliakunda akizungumza kuhusu Malameni Rock. |
Kwa mujibu wa kamusi
ya mtandaoni Wikipedia; Ulemavu ni hali ya kuwa na hitilafu ya kudumu mwilini
au akilini inayomzuia mtu kutekeleza shughuli zilizo kawaida katika maisha ya
jamii.
Unamwekea mtu mipaka
asiweze kutekeleza shughuli fulani katika maisha yake, tofauti na watu wengine.
Kuna nchi nyingi
walemavu wana klabu za michezo au kuendesha michezo katika vitengo vya pekee
vya klabu za kawaida.
Kwa kawaida
wanatekeleza michezo ya kawaida lakini kufuatana na kanuni zinazolingana na
hitilafu zao.
Je, Malameni Rock
iliwahi kufikiria kuwa kuna siku nchi mbalimbali zitakuja kuwa na maendeleo ya
juu ambayo yangemthamini mtoto mwenye ulemavu badala ya kuwaza kuwa anailetea
jamii husika laana na mikosi?
Hivyo basi Malameni
Rock inasalia kuwa ni mwamba wa kihistoria ambao unafaa kuenziwa ili kuendelea
kutoa msisitizo kwa jamii mbalimbali Tanzania na ulimwenguni kote umuhimu wa
kutowatenga watoto wenye ulemavu na wakati mwingine kuwaua kwa kudhani ni mikosi
na laana.
STORY & PHOTO BY: Kija
EDITED BY: Jabir Johnson
0 Comments:
Post a Comment