Wednesday, January 1, 2020

Ufahamu mwezi Januari



Januari ni mwezi wa kwanza katika kalenda ya Julian na ile ya Gregori. Pia ni mwezi wa kwanza kati ya saba ambao una siku 31. Siku ya kwanza ya mwezi huu inajulikana kama ni Mwaka Mpya.

Kwa wastani katika solistasi ni mwezi ambao upande wa kaskazini mwa mstari wa Ikweta huwa ni majira ya baridi.

Januari ni mwezi pili katika kipindi hicho cha baridi. Katika mzingo wa Kusini ni mwezi wa pili katika majira ya joto.

Rumi ya Kale walikuwa wakisherekea Januari 1, sikukuu ya Cervula ambayo kwa mujibu wa mwandishi wa vitabu wa Uskochi Robert Chambers (1864) anasema ilikuwa inaunganishwa na sikukuu ya Wakristo ya Punda ambayo ilikuwa inafanywa kuadhimisha namna Yusuf na mkewe Bikira Maria na mtoto Yesu walivyokimbilia nchini Misri baada ya kuambiwa na Malaika wa Mungu.

Pia mwezi Januari kwa Warumi walikuwa wakisherekea sikukuu ya Juvenalia ambayo ilianzishwa na Kaisari Nero mwaka 59 B.K ikiwa na maana ya kutoka katika ujana na kuingia utu uzima.

Sikukuu hii ya Juvenalia ilikuwa ikiadhimishwa kwa ajili ya tukio la Nero akiwa na umri wa miaka 21 kwa mara ya kwanza aliponyoa ndevu kuashiria ametoka katika ujana na kuingia utu uzima.

Aidha mwezi Januari Warumi wa Kale walikuwa wakisherekea sikukuu ya Carmenta kwa heshima ya mungu mke Carmenta ambapo katika kalenda ya Gregori matukio hayo hayakuingizwa.

Januari inatokana na neno la Kilatini Ianuarius.

Katika kalenda za zamani ya Kirumi jina kamili lilikuwa Mensis Ianuarius  ukiwa ni mwezi wa Janus.

Janus alikuwa ni mungu mwanzilishi na tafsiri kwa tamaduni za Warumi.

Mwezi huu wa Ianuarius ulikuwa na siku 29; siku mbili ziliongezwa katika kalenda mpya iliyoanzishwa na Julius Caesar mnamo mwaka 45 K.K

Kwa asili Kalenda ya Kirumi ilikuwa na miezi 10 ambayo ni sawa na siku 304 huku kipindi cha baridi kikichukuliwa kama ni cha giza.

Mnamo mwaka 713 K.K aliyerithi mikoba ya Romulus, Mfalme Numa Pompilius aliongeza miezi miwili Januari na Februari hivyo kufanya kalenda kuenda na siku za mwezi kwa mwaka ambazo ni 354.

Japokuwa mwezi Machi ndiyo ulikuwa mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kirumi ya Kale, Januari ikawa ndiyo mwezi wa kwanza.

Hata hivyo waandishi wa historia wa Rumi wanatofautiana katika uanzilishi huku wengine wakimtaja Decemvirs kuwa aliongeza miezi hiyo miwili mwaka 450 K.K

Hapo kabla ya mwaka 153 K.K mwanzo wa kalenda ulikuwa ukitambulika kwa Majaji wa Mahakama viongozi wa Kijeshi ya Jamhuri ya Rumi waliokuwa wakiingia kazini kati ya Mei 1 au Machi 15; hivyo baada ya kuongezwa miezi miwili Januari 1 ndiyo ikawa siku ya kwanza ya kuanza kuingia ofisini.

Kwa mujibu wa msomi, mwanahistoria, mwanasheria, mwandishi wa habari, mwanasiasa wa Kijerumani Theodor Mommsen aliandika kuwa Januari 1 katika kalenda ya Kale ya kirumi ilianza kutumika mwaka 600 ‘Ab urbe Condita’ ambao ni sawa na mwaka 153 K.K baada ya maafa yaliyotokea katika vita vya Lusitania au kwa kigiriki ikifahamika zaidi kama Pyrinos Polemos ambapo makabila ya Hispania yalipambana kupinga utawala wa Jamhuri ya Rumi.

Katika vita hivyo magavana wawili wa Kirumi na majeshi yao waliuawa na Chifu Punicus wa Lusitania ambaye alivamia eneo la Rumi. 

Sasa ilibidi wapelekwe majaji wenye kujua sheria huko Hispania na kupata msaada zaidi. Watalaamu wawili wa sheria na viongozi wa Kijeshi waliingia kazini miezi miwili na nusu kabla ya muda wa kisheria wa kuripoti kazini ambao ulikuwa ni Machi 15.

Vita ya Lusitania ilipiganwa kati ya mwaka 155 hadi 139 katika eneo ambalo kwa sasa ni Ureno na sehemu baadhi za Hispania hususani jimbo la Extremadura kati ya mto Tagus na Douro.

Mwanzoni mwa karne ya 16 baadhi ya nchi barani Ulaya zilianza kutumia  Januari 1, kama mwanzo wa mwaka ambayo walikuwa wakiita ‘Siku ya Kutahiri’ ambayo kwa kalenda ya Kiyahudi ilikuwa mtoto wa kiume anatahiriwa siku nane baada ya kuzaliwa kwake hivyo kuwa siku ya saba baada ya Desemba 25.

Imetayarishwa na Jabir Johnson...........................Januari 1, 2020

0 Comments:

Post a Comment