Tuesday, January 21, 2020

Mwaka mmoja tangu kifo cha Emiliano Sala (1990-2019)


Ni mwaka mmoja sasa tangu alipofariki nyota wa kandanda raia wa Argentina Emiliano Sala kwa ajali ya ndege, familia yake imekaririwa ikizungumza kwa uchungu mwingi tangu ilipompoteza kijana huyo alikuwa chipukizi katika soka Januari 21, 2019.

Emiliano Sala alikuwa akijiandaa kucheza ligi kuu ya England ili aweze kuitumikia timu yake ya taifa wakati mauti yalipomkuta kwa ajali ya ndege katika mwambao unaotenganisha England kwa Upande wa Kusini na Ufaransa kwa upande wa kaskazini.

Ilikuwa ni ndoto ya nyota huyo kuhudumu katika EPL. Cardiff City ilimtangaza Emiliano kuwa mchezaji wao Januari 19, 2019 na mauti yalimkuta wakati akiwa safarini kwenda Cardiff akitokea Nantes nchini Ufaransa  baada ya ndege aina ya Pipes Malibu ilipopoteza mwelekeo na kupotea.

Taarifa za kifo cha Emiliano zilithibitisha rasmi Februari 7, 2019 baada ya kupatikana kwa mabaki ya ndege na mwili wake. Nyota huyo alikuwa akicheza nafasi ya ushambuliaji.

Novemba mwaka 2017 alikuwa miongoni mwa ambao wangeweza kuvaa viatu vya Lionel Messi kwa taifa lake.

Kaka yake aliyefahamika kwa jina la Dario na watu wengi wa kitongoji cha Progreso nchini Argentina wanaamini hadi sasa Emiliano angeweza kuvaa viatu vya Messi kwani Messi hufunga bao kwa uwiano mzuri wa dakika 95 lakini Emiliano alikuwa akifunga kwa uwiano wa dakika 98.

Katika kitongoji cha Progreso picha ya mshambuliaji wa Ufaransa na klabu ya Paris Saint Germain Kylian Mbappe akimkumbatia Emiliano bado imehifadhiwa.
Kaka yake alikaririwa akisema Emiliano katika makuzi yake alikuwa akitamani kuwa kama washambuliaji mahiri na maarufu ulimwengu waliowahi kuvaa jezi ya Albiceleste Carlos Tevez na Gabriel Batistuta na alikuwa akiipenda klabu ya Independiente ya huko huko Argentina.

Emiliano alizaliwa Oktoba 31, 1990 ; alianza maisha yake ya soka akiwa na klabu ya Bordeaux ya Ufaransa  na mechi yake ya kwanza ilikuwa Februari 2012.

Hata hivyo alitolewa kwa mkopo katika klabu ya Championnat National iliyopo ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa na baadaye Niort kwa misimu miwili mfululizo.

Akiwa huko alifurahia kwani alifunga mabao 39 kabla ya kurudi Bordeaux. Aliporudi Caen wakamtaka kwa mkopo ikabidi aende. Mnamo mwaka 2015 klabu ya Nantes ilidaka saini yake baada ya Bordeaux kuamua kumuuza kwa makubaliano ya awali.

Alicheza mechi 120 akiwa na Nantes huku akifunga mabao 42 katika Ligue 1. Akiwa na miamba hiyo aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa klabu kwa misimu mitatu mfululizo.

Ndipo Januari 2019 Cardiff City ilipodaka saini yake kwa ada ya pauni milioni 15.

Ajali ilitokea Januari 21, 2019 huko Alderney huku akiwa ni abiria pekee katika ndege hiyo.

Siku tatu mfululizo ndege ilikuwa ikitafutwa. Mwili wa Emiliano ulipatikana Februari 3 na siku nne baadaye ulizikwa.

Mashabiki wa Cardiff walitoa rambirambi zao kutokana na kifo hicho nje ya dimba la Cardiff City wakimlilia kwa majonzi makubwa.

Imetayarishwa na Jabir Johnson......................XXI-I-MMXX

0 Comments:

Post a Comment