Januari 15, 1981 alizaliwa
mshambuliaji wa zamani soka wa Kimataifa wa Senegal na klabu ya Liverpool na
Bolton El Hadji Diouf.
Nyota huyo wa kandanda
alizaliwa jijini Dakar. Katika maisha ya soka alikuwa akifahamika kama ni
mchezaji kipaji mtata.
Amezitumikia klabu nyingi
barani Ulaya katika mataifa ya Ufaransa, England na Uskochi.
Alianza maisha yake ya soka
katika klabu ya Sochaux ya nchini Ufaransa mnamo mwaka 1998 na msimu uliofuata
alitua katika klabu ya Rennes ambako alidumu kwa msimu mmoja.
Mnamo mwaka 2000 alisaini
kuhudumu na Lens hadi mwaka 2002. Akiwa na Lens alifunga mabao 18 katika mechi
54.
Hata hivyo alionyesha uwezo
mkubwa akiwa na timu ya taifa ya Senegal katika Kombe la Dunia mnamo mwaka 2002
alipokuwa miongoni mwa walioifikisha robo fainali ya mashindano hayo.
Kocha Gerard Houllier
wakati huo akinoa Liverpool alivutiwa sana na muundo wa uchezaji wa Diouf hivyo
akaidaka saini yake kwa pauni milioni 10.
Diouf alikuwa mshambuliaji
ambaye kocha Houllier aliamini kwamba atamsaidia kubeba taji la Ligi Kuu kutoka
mikononi mwa Manchester United.
Hata hivyo aliishia kushika
nafasi ya pili. Katika siku za mwanzo Diouf alikuwa akisifiwa sana na mashabiki
wa Liverpool kwani katika mchezo wake wa kwanza pale Anfield alifunga mabao
mawili katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Southampton hiyo ilikuwa Agosti 24,
2002.
Alianza msimu wa 2003
katika Fainali ya Football League ambapo Liverpool iliizabua Manchester United
kwa mabao 2-0.
Katika mchezo huo wa
fainali Diouf hakufumania nyavu hivyo mashabiki wa Liverpool walisubiri mpaka
Machi 2003 kwenye mchezo dhidi ya Bolton ambao Diouf alifunga kwenye ushindi wa
mabao 2-0.
Kwenye mchezo huo Diouf
alifunga na kutoa pasi ya mwisho. Katika mchezo mwingine ndani ya mwezi huo huo
ilikuwa ni dhidi ya Celtic katika dimba la Parkhead kwenye Ligi ya Europa
zamani ikijulikana kama UEFA Cup ambapo Liverpool ilitoka sare ya 1-1.
Katika mchezo huo sifa za
Diouf kuwa ni mchezaji mwenye utata zilidhihirika kunako dakika ya 87 alipomvaa
shabiki wa Celtic na kuzua tafrani uwanjani hapo na Polisi kumchukua Diouf kwa
mahojiano zaidi.
Houllier alimpa makavu kuwa
kitendo alichokifanya kitadidimiza maisha yake yote katika kandanda. Diouf
alifungiwa mechi mbili na kukatwa mshahara wa majuma mawili kwa ajili ya
kumpoza shabiki wa Celtic.
Msimu wa 2002-03 Diouf
hakufunga tena bao katika klabu ya Liverpool
huku msimu wa 2003-04 akionyeshwa kadi za njano 12 na moja nyekundu.
Kadi hiyo nyekundu
alionyeshwa Januari 7, 2004 alipomchezea vibaya Adrian Muttu katika mchezo
ambao Liverpool iliibuka na ushindi wa bao 1-0 hivyo hakuwa tena mchezaji wa
kuogopwa kutokana na kushindwa kufunga mabao.
Jamie Carragher aliwahi
kusema usajili wa Diouf huenda ndio ulikuwa mbaya katika historia ya Liverpool
kwani alimaliza msimu pasipo kufunga bao. Msimu wa 2004-05 walimtoa kwa mkopo
katika klabu ya Bolton ambapo alianza
kufunga tena akifunga mabao 21.
Baada ya misimu minne ya
kuishi Bolton alitua Sunderland ambako alikaa msimu mmoja 2008-09 na baadaye
Blackburn Rovers mnamo mwaka 2009 hadi 2011.
Nusu msimu wa 2010-11 Diouf
alitolewa kwa mkopo katika klabu ya Rangers. Akitokea Uskochi alirudi Doncaster
Rovers na mnamo mwaka 2012 alitua Leeds.
Kwa mara ya mwisho Diouf
alihudumu na klabu ya Sabah FA ya Malaysia kabla ya kustaafu mnamo mwaka 2015.
0 Comments:
Post a Comment