Saturday, January 4, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Sheikh Maktoum bin Rashid Al Maktoum ni nani?


Jumatano ya Januari 4, 2006 ilikuwa siku ya huzuni katika ardhi ya U.A.E baada ya kuondokewa na mtawala wa Dubai, makamu wa rais na Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Maktoum bin Rashid al-Maktoum kwa shambulio la moyo. 

Sheikh Maktoum alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 62 nchini Australia katika Hotel ya Palazzo Versace huko Queensland nchini Australia. 

Desemba 28, 2005 aliwasili katika uwanja wa ndege akiwa na ndege yake ya Boeing 747-400 kwa ajili ya kuhudhuria kongamano la kibiashara ambalo hufanyika mwanzoni mwa mwezi Januari. 

Baada ya kutangazwa kwa kifo hicho nafasi yake ilichukuliwa na mdogo wake wa kiume Sheikh Mohammed bin Rashid al-Maktoum. 

Mamlaka za Dubai zilitangaza siku 40 za maombolezo. Ofisi za serikali zilifungwa kwa siku saba kwa ajili ya kuomboleza kifo cha mtawala huyo. Pia siku hiyo soko la hisa la Dubai halikufanya kazi pia maduka na sehemu za biashara zilifungwa katika mji wa Abu Dhabi. 

Wizara ya Elimu ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar ulitangaza kuahirisha mitihani iliyokuwa ifanyike  na hata Tamasha la Fartboy Slim lililokuwa lifanyike usiku huo liliahirishwa. 

Haikutosha mbio ndefu za Dubai maarufu Dubai Marathon hazikufanyika siku hiyo. Baada ya kufariki kwake maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Brisbane ambako ndege yake iliweka tangu alipowasili walifanya maandalizi ya kuurudisha mwili wake kwa kutumia ndege yake. Safari ya kuurudisha mwili Dubai ilichukua takribani saa 14 kutoka Australia. 

Enzi za uhai wake mbali na kuwa mtawala Sheikh Maktoum alikuwa akijihusisha na masuala ya ufugaji, uuzaji na michezo ya farasi. Sheikha Alia bint khalifa bin Saeed al Maktoum alikuwa mke wa Maktoum hadi mauti yalimpokuta. Walioana Machi 12, 1971. 

Sheikh Maktoum alizaliwa mnamo mwaka 1943 katika kitongoji cha Al Shindagha jijini Dubai katika familia ya Al Maktoum wa kabila la Al Bu Falasah. Alishika madaraka hayo baada ya kifo cha baba yake Rashid bin Saeed Al Maktoum. 

Sheikh Maktoum alikuwa waziri mkuu wa kwanza baada ya uhuru ambapo alishika wadhifa huo kuanzia Desemba 9, 1971 hadi Aprili 25, 1979. Pia alirudi katika nafasi hiyo baada ya kifo cha baba yake Oktoba 7, 1990. 

Sheikh Maktoum alikuwa akivitumikia vyeo vyote vitatu tangu wakati huo hadi kifo chake.  

0 Comments:

Post a Comment