Januari 2, 1995 alifariki
dunia mwanasiasa wa Somalia ambaye alikuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Somalia kutoka mwaka 1969 hadi 1991 Jenerali Siad Barre.
Alipokimbia taifa hilo
baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi kufanyika mjini Mogadishu Siad Barre
alijificha kusini magharibi mwa Somalia katika mkoa wa Gedo ambako ndiko
alikokulia.
Akiwa huko alifanya harakati za kutaka kurudi tena madarakani na
inaelezwa mara mbili alirudi katika makao makuu ya taifa hilo ili aweze
kuchukua tena lakini Mei 1991 alishindwa na majeshi ya Jenerali Mohamed Farrah
Aidid ambayo yalimfanya aishi uhamishoni.
Barre alikwenda zake Nairobi nchini
Kenya lakini makundi ya kiharakati nchini humo yalipinga ujio wake na kwamba huenda serikali ya Kenya ilikuwa
ikimuunga mkono. Kutokana na shinikizo hilo majuma mawili baadaye ilimbidi Siad
Barre akimbilie Nigeria. Taarifa zinasema aliariki dunia Januari 2, 1995 jijini
Lagos kwa shambulio la moyo na kuzikwa katika wilaya ya Garbahaareey katika mkoa wa Gedo nchini
Somalia.
Mohamed Siad Barre
alizaliwa mnamo oktoba 6 mwaka 1919 katika kijiji cha Shilavo jimbo la Ogaden
magharibi mwa Somalia akitokea kwenye kabila la Marehan, akiwa na umri wa miaka
10 Barre wazazi wake wote wawili walifariki hivyo alijikuta akiwa yatima katika
umri huo mdogo.
Mohamed Siad Barre alianza
elimu yake ya sekondari katika mji wa Liquu kusini mwa Somalia na baadaye mwaka
1940 alienda mjini Mogadishu kujiunga na elimu ya sekondari hata hivyo
utaratibu ulimtaka kupitia kwanza jeshini hivyo akajiunga na jeshi chini ya
ukoloni wa Italia, wakati huo ndiyo vita kuu ya pili ya dunia ilikuwa imelipuka
mwaka 1939 hivyo Barre na yeye akalazimishwa kwenda vitani ambapo alienda
nchini Kenya alipopigania kwenye jeshi la Italy na Ujerumani dhidi ya Uingereza
na ufaransa.
Mwaka 1952 Barre alipata
nafasi ya kuhudhuria mafunzo katika chuo cha kijeshi cha Carabinieri nchini
Italia kwa miaka miwili na baadaye aliporudi Somalia alizidi kupanda vyeo
kwenye jeshi, hadi kufikia mwaka 1960 Somalia ilipopata uhuru wake Barre
aliteuliwa kuwa mkuu wa kikosi cha anga huku pia akifanywa kuwa mkuu wa jeshi
msaidizi.
Muda wote huu akiwa jeshini
Barre hakuacha kuonyesha mapenzi yake makubwa kwa mfumo wa kisoshalisti wa
Urusi hali iliyochochea ukaribu wake na maofisa mbalimbali wa jeshi wa taifa
hilo ambalo lilikuwa kitovu cha ujamaa ulimwenguni kwa kipindi kile.
Kufuatia mgogoro wa katiba
nchini Somalia mwaka 1969 mwanajeshi wa cheo cha chini kabisa alimpiga risasi
rais wa pili wa Somalia Abdirashid Ali Shermarke, tukio hili lilikuwa ni bahati
ya mtende kwa Barre kwani kutokana na tabia yake ya kujiamini tena kuongea bila
woga mbele ya wenzake hali iliyomjengea ushawishi mkubwa hivyo siku ya mazishi
ya rais aliyeuawa Abdirashid Ali Shermarke oktoba 21 mwaka 1969 jeshi lilitwaa
nchi katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu na Mohamed Siad Barre akafanywa
rasmi kuwa rais wa tatu wa Jamhuri ya Somalia huku pia akifanywa kiongozi wa
baraza la mapinduzi "Supreme Revolutionary Council" SRC.
Kuingia kwa Barre katika
urais wa taifa kulibadili kabisa historia ya Somalia na pengine historia ya taifa
hilo lililopo katika Pembe ya Afrika kwani
kutokana na tabia yake ya kujiamini kupindukia alitangaza rasmi mkakati wake wa
kuijenga upya Somalia huku akidai kuwa anataka Somalia iwe taifa kubwa na
pengine iogopwe ndani na nje ya Afrika.
Mwaka 1970 Barre
aliitangaza Somalia kuwa taifa la kijamaa huku mwenyewe akiipaachika jina la
"The Great Socialist Somali" ambapo aliamua kabisa kujiegemeza kwa Urusi
akipokea misaada mingi ya kijeshi na kijamii, pia alianzisha matumizi ya lugha
ya kisomali mashuleni na vyuoni huku akipinga lugha za kigeni hususani
kingereza na kiitaliano.
Huku akiwa anavalia gwanda la jeshi na miwani miyeusi
ya jua Barre alitamka kwa sauti kubwa "sikuja kuwagawa Wasomalia bali
kuwaunganisha , nitamheshimu kila msomali kwasababu anastahili heshima ila
yeyote atakayethubutu kupinga utawala wangu litakalompata asilalamike."
Mwaka 1973 Barre alifanywa
kuwa mwenyekiti wa OAU nafasi ambayo aliitumia vizuri kuimarisha jeshi lake kwa
kujipatia silaha za kisasa kutoka Urusi kwa kutumia kkigezo cha kuharakisha
ukombozi kwenye mataifa yaliyokuwa bado yakitawaliwa. Alianzisha vijiji vya
ujamaa, akajenga barabara na kupiga marufuku ukabila nchini humo kwa kile
alichodai wasomalia ni wamoja tu.
Mwaka 1976 Barre aliingia
kwenye mgogoro na maswahiba zake Warusi, ili kuwaonyesha yeye si mtu wa
kutishwa Barre aliwatimua wataalamu wote wa Kirusi waliokuwa nchini Somalia
huku akisisitiza kuwa hawezi kutishwa wala kuogopa mtu yeyote kwasababu
anaungwa mkono na wasomali wote.
Mwaka 1977 Barre alianza
vituko vyake pale alipotaka kuongeza eneo la jimbo la Ogaden hali iliyomfanya
kuvamia eneo la Ethiopia , hii ilichochea kile kilichoitwa vita ya Ogaden ambapo
Urusi waliamua kuisaidia Ethiopia ili kumkomoa Barre, mwanzoni vikosi vya Barre
vilipata ushindi hata hivyo mwaka 1978 Barre alizidiwa na kuamua kuliachia eneo
hilo. Kutoka hapo Barre aliamua kujiegemeza kwa Marekani hali iliyomfanya
kujiimarisha tena hata hivyo upinzani wa ndani ya nchi dhidi ya uongozi wake
ulizidi mno.
Mwaka 1986 Barre alipata
ajali kubwa ya gari mjini Mogadishu ambapo inaelezwa kuwa aligongwa na lori
kufuatia mvua kubwa hivyo dereva wake kulivaa lori, Barre alijeruhiwa vibaya
akapelekwa kulazwa nchini Saudi Arabia kwa miezi miwili huku makamu wake Luteni
jenerali Mohamed Ali Samatar.
Baada ya kurejea nchini
Somalia Barre alijitahidi kuonyesha kuwa bado anaweza kuendelea kuwatumikia
wasomalia hata hivyo tayari vuguvugu la nani atamrithi lilipamba moto nchini
humo huku wengi wakiamini hana uwezo tena wa kuendelea kuongoza taifa hilo.
Tangu kuondoka kwa Barre
Somalia imetawaliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe
Mwaka 1988 uasi uliongezeka
nchini Somalia hali iliyofanya maisha kuwa magumu mwishowe mwaka huohuo Barre
alianza kuua watu hovyo hali iliyokoleza chuki dhidi yake. Mnamo Januari 26
mwaka 1991 vikosi vya bwana wa vita aliyefahamika kama Mohamed Farrah Aidid
vilifanikiwa kumpindua Barre.
Mohamed Siad Barre
atakumbukwa zaidi kwa kauli yake maarufu aliyowahi kuitoa alipokuwa ukingoni
mwa utawala wake kabla ya kuangushwa ambapo alisema "nilipokuja Mogadishu
nilikuta waitalia wamejenga barabara moja mkinilazimisha kuachia madaraka basi
hali itarudi kama awali lakini pia kumbukeni kuwa mimi nimepata madaraka kwa
bunduki hivyo nitaondoka kwa bunduki pia".
Imetayarishwa
na Jabir Johnson........Januari 2, 2020.
0 Comments:
Post a Comment