Wednesday, January 8, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Akbar Hasheem Rafsanjani ni nani?


Januari 8, 2017 alifariki dunia mwanasiasa, mwandishi na miongoni mwa waanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyehudumu kama Rais wa nne taifa hilo Akbar Hashemi Rafsanjani.

Mwanasiasa huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika ardhi hiyo alihudumu katika madaraka hayo ya juu kutoka Agosti 3, 1989 hadi Agosti 3, 1997.

Pia alihudumu katika Bunge la Watalaamu kutoka mwaka 2007 hadi mwaka 2011 nafasi ambayo hakutaka iwe yake milele.

Rafsanjani alifariki dunia kwa shambulio la moyo ambapo hali ya afya yake ilianza kubadilika akiwa katika bwawa lake la kuogelea kabla ya mauti kumkuta.

Baada ya hapo alichukuliwa hadi hospitali ya Shohada-ye Tajrish iliyopo kaskazini mwa jijini la Tehran.

Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82 alizaliwa Agosti 25, 1934 katika jimbo la Kerman kwenye familia ya wakulima matajiri. Serikali ya Iran ilitangaza siku tatu za maombolezo na kwamba itakuwa siku ya kifo chake itakuwa siku mapumziko kutokana na mchango wake katika Jamhuri ya Iran.

Mabango ya rangi nyeusi yalifungwa kila pembe ya jiji la Tehran na miji mingine nchini humo yakionyesha na kumwelezea Rafsanjani alikuwa mtu wa namna gani huku picha kubwa za Rafsanjani zenye tabasamu zikipepea katika mabango hayo.

Katika jimbo la Kerman ambako alizaliwa kiongozi huyo siku tano za maombolezo zilitangazwa.

Miezi miwili baada kifo chake Ayatollah Rafsanjani alipewa mtaa jijini Tehran ambapo mtaa uliokuwa ukifahamika kwa jina la Sa’adat Abad ulibadilishwa kwa heshima yake na kupewa jina lake.

Mitaa mbalimbali katika miji mingine ilibadilishwa na kuitwa Hashemi Rafsanjani. Pia katikati ya Chuo Kikuu cha Azad jengo mojawapo lilibadilishwa na kupewa jina lake pia sanamu yake ilitengenezwa na kuwekwa humo.

Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kerman ulibadilishwa jina na sasa unafahamika kwa jina la Ayatollah Hashemi Rafsanjani.

Mwaka mmoja baada ya kifo chake familia ya Rafsanjani ilifungua upya jalada kuhusu kifo cha rais huyo wa zamani wa Jamhuri ya Iran kwa kile kilichodaiwa kulikuwa na kiwango kisichokuwa cha kawaida cha mionzi katika mwili wake.

Binti wa Ayattollah Rafsanjani Faezeh Hashemi alisema kuwa uchunguzi uliofanywa na baraza la usalama la nchi hiyo ulibaini kuwa mwili wa baba yake ulikuwa ni kiwango cha mionzo mara kumi ya inavyotakiwa.

Akiwa na miaka 40 Rafsanjani aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Iran, pia Amiri Jeshi wakati wa vita vya Iran na Iraki mnamo mwaka 1980 hadi 1988.

Kutokana na uimara wake katika siasa za Iran alipewa jina la Akbar Shah. Rafsanjani alikuwa rais wa taifa hilo baada ushindi wa uchaguzi wa mwaka 1989 pia akishinda katika uchaguzi wa mwaka 1993.

Mnamo mwaka 2005 alirudi tena akitaka kuhudumu kwa mara ya tatu lakini alishindwa katika duru ya pili kwa mpinzani wake Mahmoud Ahmadinejad.

Familia ya Rafsanjani ilikutana na upinzani mkali pale ilipoamua kuwaunga mkono wapinzani mnamo mwaka 2009. Rafsanjani aliingia katika mbio za kuwani urais mnamo mwaka 2013 lajkini alishindwa katika hatua za awali.

Ujio wa Hassan Rouhani katika siasa za Iran uliungwa mkono na Rafsanjani na hapo ndipo familia ya Rouhani iliporudisha hali nzuri ya kisiasa kwa familia ya Rafsanjani.

Katika masuala ya uchumi aliunga mkono soko huru la ndani na pia ubinafsishaji wa mashirika na viwanda vilivyokuwa mikononi mwa serikali.
Hata hivyo alikuwa makini sana kutoingia katika mgongano na Marekani na mataifa mengine ya magharibi.

Jarida la Forbes lilikadiria utajiri wake kuwa unazidi dola za Kimarekani bilioni moja.


0 Comments:

Post a Comment