Januari 6, 2012 klabu ya Arsenal ilithibitisha kumrudisha mshambuliaji wao Thierry Henry kwa mkopo.
Thierry Henry anaendelea kushikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa zama zote tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mnamo mwaka 1886.
Henry alihudumu na Arsenal kutoka mwaka 1999 hadi 2007 akicheza mechi 369 na kufunga mabao 226.
Pia nyota huyo wa Ufaransa alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na miamba hiyo ya kaskazini mwa London likiwamo la msimu wa 2003-2004 ambalo walilitwaa pasipo kupoteza mchezo hata mmoja.
Aidha Thierry Henry alitwaa mataji matatu ya Kombe la FA kabla ya kutimua mbio kwenda Barcelona kwa ada ya euro milioni 24.
Akiwa nchini Hispania aliendelea kukusanya mataji akichukua mara sita katika mashindano matatu Ligi Kuu nchini Hispania La liga, Kombe la Mfalme na Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Baada ya kuondoka kwa nyota huyo Arsenal haijatwaa taji la Ligi Kuu ambapo msimu wa 2011-12 walimwangazia nyota huyo kwa ajili ya kuwasaidia.
Hata juhudi za kumbakisha katika viunga vya London zilishindikana kwani alitimkia New York Red Bulls katika Ligi Kuu nchini Marekani (MLS). Mnamo Januari katika majira ya baridi walifanikiwa kumpata kwa mkopo wa miezi miwili, ambapo Januari 9 alicheza mchezo wake wa kwanza.
Katika mchezo huo Henry alifunga bao pekee la ushindi dhidi ya Leeds United kwenye Kombe la FA. Alicheza tena mechi sita baadaye ambapo alifunga katika mechi yake ya mwisho kwenye mchezo dhidi ya Sunderland kabla hajaenda zake jijini New York.
Mnamo Desemba 2012 kulikuwa na tetesi kwamba huenda wakamrudisha tena Thierry Henry katika EPL lakini tetesi hizo hazikutimia kwani alikaririwa kwamba angependa zaidi kurudi Arsenal kama kocha baada ya kustaafu kucheza soka la kimataifa.
0 Comments:
Post a Comment