Monday, January 13, 2020

Derby della Mole yachezwa kwa mara ya kwanza



Januari 13, 1907 klabu za soka za jiji la Turin nchini Italia yaani Juventus na Torino zilicheza mchezo wa kwanza wa watani wa jadi maarufu Derby della Mole. 

Katika mchezo huo Torino ambao ni maarufu kwa jina la Granata walishinda mabao 2-1 dhidi ya Biaconneri. 

Klabu hizo mbili zina historia inayofanana kwani Torino ilianzishwa mwaka 1906 kutoka Juventus. Chanzo cha kuundwa kwa Torino ilikuwa ni wanachama wa klabu ya Juventus ilianzishwa mnamo mwaka 1897 walipotaka kuiondoa klabu hiyo jijini humo na kuihamishia sehemu nyingine. 

Baadhi ya wanachama walikataa ombi hilo akiwamo Alfredo Dick ambaye ndiye aliyeanzisha klabu hiyo mpya ili isalie jijini humo. Mechi hiyo ya watani wa jadi ilipewa jina la Derby della Mole kutokana na jengo maarufu sana jijini humo lililokuwa likifahamika kama Mole Antonelliana. 

Kwa mara ya kwanza zilikutana mnamo mwaka 1907 katika championship zikicheza mfumo wa mtoano wa nyumbani na ugenini. 

Kwa mara ya kwanza Torino ilicheza mchezo wa kwanza nyumbani Velodrome Umberto I na kushinda mabao 2-1 mabao ya Federico Ferrari Orsi na Hans Kempher. Bao pekee la Juve lilifungwa kwa mkwaju wa penati na Ernesto Borel. Baada ya hapo mzunguko wa pili Torino ilishinda kwa mabao 4-1 hivyo kusonga mbele kwa uwiano wa mabao 6-2. 

Hata hivyo Torino walipoteza dhidi ya Milan hivyo walishindwa kuchukua taji hilo. Miamba hiyo imekutana mara 242; Juventus ikishinda mara 104. Mechi hii ya mahasimu ni zamani katika soka la Italia inayoendelea kwa moto ule ule kutoka katika mji mmoja. 

Mfungaji bora katika mechi hii ya mahasimu wa Turin ni nyota wa Juventus Giampero Boniperti aliyecheza misimu 15 kutoka 1946 hadi 1961 akifunga mabao 14. Mara ya mwisho miamba hii ya Della Mole ilikutana Novemba 2, 2019 kukishuhudiwa Torino akizabuliwa kwa bao 1-0. 

Itakutana tena Aprili 5 mwaka huu. Mara ya mwisho Torino kuifunga Juventus ilikuwa ni Aprili 26, 2015 iliposhinda kwa mabao 2-1 katika Serie A.

0 Comments:

Post a Comment