Saturday, January 25, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Mamadou Dia ni nani?



Januari 25, 2009 alifariki dunia Waziri Mkuu wa kwanza wa taifa la Senegal aliyefahamika kwa jina la Mamadou Dia. 

Mwanasiasa huyo wa Senegal alihudumu katika nafasi hiyo kutoka mwaka 1957 hadi mwaka 1962. Alishika wadhifa huo hadi alipolazimishwa kujiuzulu na pia mashtaka yake ya kutaka kuipindua serikali ya Rais wa wakati huo Leopold Sedar Senghor. Dia alianza harakati zake za kisiasa mnamo mwaka 1949 kama kiongozi wa baraza kuu wa AOF na katibu mkuu wa chama cha Senegalese Democratic Bloc (BDS) mnamo mwaka 1950. Alihudumu katika bunge la seneti la Ufaransa kutoka mwaka 1948 hadi mwaka 1956 na pia kama naibu spika wa bunge la Ufaransa kutoka mwaka 1956 hadi mwaka 1958. Akiwa na Senghor, walifanikiwa kuanzisha chama cha African Convention (PCA) Januari mwaka 1957 kutoka BDS. Baada ya rais wa zamani wa Ufaransa Charles de Gaulle kuanzisha utaratibu mwingine wa kisiasa katika jamii nzima ya Ufaransa na makoloni yake mnamo mwaka 1958 wawili hayo yaani Senghor na Dia walikuwa wapinzani katika sera zao. Dia alikuwa akipendelea kujiondoa katika muungano na Ufaransa wakati Senghor alipendelea kusalia mikononi mwa wakoloni hao. Dia alifanya kazi ya ziada katika mikataba mbalimbali kwenye taifa hilo dhidi ya wakoloni kutoka barani Ulaya, ambao walikuwa na nia ya kuinyonya zaidi Senegal. Baada ya miaka miwili ya kuwamo katika bunge, Mamadou Dia alikuwa mhimili mkuu wa ukosefu wa utulivu baada ya uhuru wa mwaka 1962 pale ambapo alishindwa kutekeleza jaribio lake la kuipindua katibu ili amzidi kete mtu wake wa karibu Senghor hapo ndipo maisha yake ya kisiasa yalipoingia doa na kujikuta akizuiliwa katika jela kwa kitendo hicho. Licha ya maisha yake ya kisiasa kwa maana ya nguvu kuporwa lakini maisha yake ya ndani hayakuharibika kwani mnamo miaka ya 1980 alitaka kurudi tena katika ulingo wa kisiasa baada ya mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa na Abdou Diouf. Hata hivyo chama kidogo cha The People Democratic Movement hakikupata uungwaji mkono wa kutosha. Baada ya hapo hakurudi tena katika medani ya siasa ya taifa hilo na alisalia kuwa nembo ya siasa za Senegal. Hadi leo Mamadou Dia anakumbukwa kwa mchango wake wa kuitengeneza Senegal ya sasa. Pia anakumbukwa kwa kuwa mpinzani wa Rais wa sasa wa Senegal Abdoulaye Wade ambaye aliwahi kuwa wakili wake miaka ile ya 1963.
Mamadou alizaliwa Julai 18, 1910  katika mji wa Khombole, mkoani Thies  na kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 98 jijini Dakar. Siku aliyofariki magazeti yaliandika mengi ya kumsifia kiongozi huyo kwamba alikuwa mtu aliyefuata kanuni na utaratibu ili kuijenga Senegal.

0 Comments:

Post a Comment