Januari 21, 2012 nyota wa zamani wa kandanda wa Marekani na klabu ya Fulham
na Tottenham Clint Dempsey aliweka rekodi ya kuwa raia wa kwanza wa Marekani
kufunga mabao matatu yaani hat trick katika mchezo wa Ligi Kuu ya England.
Hat
trick hiyo aliifunga wakati akihudumu na Fulham katika ushindi wa mabao 5-2
kwenye mchezo dhidi ya Newcastle ulichezwa katika dimba la Craven Cottage.
Kiungo na mshambuliaji huyo ambaye alikuwa akifahamika kwa jina la Deuce ulikuwa
ni ni mwaka wake wa sita katika klabu hiyo ya jijini London tangu alipojiunga
Januari ya mwaka 2007 kwa ada ya pauni milioni mbili.
Alipotua katika viunga
vya jiji hilo alijiweka sawa katika kikosi cha kwanza akicheza zaidi ya mechi 40 kwa kila msimu.
Katikati ya msimu wa 2011-12 Fulham ilikuwa ikihaha kujinasua kutoka katika
mstari wa kushuka daraja kwenye msimamo wa ligi hiyo ambapo Newcastle wakiwa miongoni mwa klabu
ambazo zilikuwa katika wakati mzuri.
Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu
huo Fulham ilipotua katika dimba la St. James Park ilichezea kichapo cha mabao
2-1.
Siku ya mchezo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Fulham ilikuwa nyuma
kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo wao Danny Guthrie. Lakini wenyeji walirudi
katika kipindi cha pili na kurekebisha makosa kwa mkwaju wa penati katika
dakika ya 52 uliokwamishwa wavuni na Danny Murphy.
Dempsey aliliona lango la
The Magpies katika dakika ya 59 na 65
hivyo kufanya Fulham, kuwa mbele kwa mabao 3-1.
Bobby Zamora aliipa bao
Fulham katika dakika ya 68 hivyo kupanua zaidi pengo na kuwa mabao 4-1.
Hartem
Ben Arfa alirudisha matumaini ya The Magpies katika dakika ya 85 ili kupunguza
pengo hilo lakini Dempsey aliwavunja moyo kabisa alipotua bao lake la tatu na
ubao kusomeka mabao 5-2.
Dempsey msimu huo alifunga mabao 23 kabla Tottenham kudaka saini yake
mwezi Agosti 2012 kwa ada ya pauni milioni sita.
Dempsey alizaliwa Machi 9, 1983
huko Nacogdoches, katika jimbo la Texas.
Alianza maisha yake ya soka na klabu
ya New England Revoultion mnamo mwaka 2004 baada ya kumaliza chuo akiwa na
klabu ya Furman Paladins. Vyombo vya habari nchini Marekani humchukulia Dempsey
kuwa ni nyota mkubwa wa zama zote wa soka nchini humo.
Alianza kuitumikia timu
ya taifa mnamo mwaka 2004 hadi alipostaafu mwaka 2017 akiwa ameifungia mabao 57
katika mechi 141.
0 Comments:
Post a Comment