Januari 22, 1922 alifariki
dunia Papa Benedict wa XV wa Kanisa Katoliki dunia. Kiongozi huyo wa juu wa
kiroho katika kanisa hilo alifariki dunia kwa ugonjwa wa kichomi.
Alishika
nafasi ya Upapa wa kanisa hilo kuanzia Septemba 3, 1914 hadi mauti yalipomkuta.
Jina lake halisi ni Giacomo Paolo Giovanni Battista della Chiesa mzaliwa wa
kitongoji cha Pegli mjini Genoa katika nchi ya Italia.
Inaelezwa mapema Januari
ya mwaka 1922 Papa Benedict XV alikuwa akisheherekea sikukuu na wanawake
maskini wa kanisa hilo katika jengo la Domus Sanctae Marthae lililopo katika
Kanisa la Mtakatifu Petro wa Basillica jijini Vatican.
Wakati akisubiri dereva
wake ambapo siku hiyo kulikuwa na mvua alianza kuugua mafua ghafla ambayo
baadaye kichomi kilianza kumtesa. Januari 5, 1922 taarifa ziliztolewa kuwa Papa
Benedict XV anaumwa mafua yalitokana na baridi.
Januari 12, 1922 ilitolewa
taarifa kuwa Papa ana kikohozi kikali. Januari 18, 1922 ilitolewa taarifa
kwamba Papa hawezi hata kuinuka kitanda
na kuanzia Januari 19, 1922 hali yake ilizidi kuwa mbaya huku mapigo yake ya moyo yakionekana kuwa
hafifu kutokana na kusambaa kwa kichomi.
Hewa ya Oksijeni iliongezwa baada ya
kushuhudiwa kuwa hali yake inazidi kuwa mbaya.
Kardinali Oreste Giorgi
alikwenda kumsalimu Papa katika chumba chake
na kumfanyia maombi. Januari 20, 1922 ilionekana hali yake inaanza
kurudi hivyo Papa Benendict aliwataka
wahudumu wa kitabibu kuondoka kwani hali yake ilikuwa sio mbaya.
Hata hivyo
inaelezwa kuwa wakati akiwa hapo alipakwa mafuta ambayo hupakwa wagonjwa na
kwamba Papa Benedict XV alijua kwamba siku zake za kuishi zilikuwa ukingoni
hivyo alizungumza maneo yake ya mwisho na Kardinali Gasparri.
Kulikuwa na taarifa tofauti za muda
aliofariki hali ilizua tafrani ambapo magazeti ya Uingereza na Ufaransa
yalisema Papa Benedict XV alifariki Januari 21 saa 11:00 alfajiri hata hivyo Daktari
wa Makerubi alitangaza rasmi kuwa Papa alifariki dunia saa 12:00 asubuhi ya
Januari 22, 1922.
Bendera zilipepea nusu milingoti kuashiria heshima na kukumbuka
kwake na ibada ya mazishi ilifanyika kwa kufuata taratibu zote za kanisa hilo.
Miongoni mwa mambo anayokumbukwa Papa Benedict XV ni mchango wake katika
kumaliza vita vya kwanza vya dunia mnamo mwaka 1918.
Moyo aliokuwa nao Papa Benedict
XV ilipofika mwaka 2005 ulimshawishi Joseph Aloisius Ratzinger kuchagua kufuata
nyayo za mtangulizi wake wakati akitawazwa kuwa Papa wa kanisa hilo Papa
Benedict wa XVI kutokana na kuwa mfano katika masuala ya kiutu na kidiplomasia.
Papa Benedict wa XVI alisisitiza kuwa amechagua jina la Benedict kutokana na
mtangulizi wake kuwa mfano katika kutunza amani.
Papa Benedict wa XV
alichaguliwa kuwa kiongozi wa juu wa kanisa hilo akiwa na umri wa miaka 59 kipindi
ambacho dunia ilikuwa katika mwanzo wa vita vya kwanza vya dunia.
Della Chiesa
alizaliwa Novemba 21, 1854.
0 Comments:
Post a Comment