Januari 20, 1983 alifariki
dunia mwanamichezo wa Brazil maarufu katika mchezo wa soka Manuel Francisco dos
Santos ‘Garrincha’.
Nyota huyo wa Brazil
amekuwa akichukuliwa kuwa ni miongoni mwa wakokotaji bora wa mpira waliowahi
kutokea katika dunia.
Garrincha alipata mafanikio
makubwa katika soka lakini alikuwa akikabiliwa na changamoto ya ulevi katika
maisha yake ya soka.
Inaelezwa kuwa Garrincha
alikuwa akikumbwa na matukio ya ajali za kutisha mara kwa mara ikiwamo ya
Aprili 1969 iliyohusisha lori ambapo mama mkwe wake alipoteza maisha.
Pia kutokana na ulevi
uliopindukia Garrincha alikuwa akipata matatizo na familia yake.
Katika kuupigania uhai wake
Garrincha alifariki dunia kutokana na ini kushindwa kufanya kazi vizuri
kitaalamu hujulikana kama Cirrhosis ya Ini.
Garrincha alioa mara mbili
wa kwanza alikuwa Nair Marques ambaye alikuwa mfanyakazi katika kiwanda mkazi
wa Pau Grande mnamo mwaka 1952 ambapo mwaka 1965 walipeana talaka.
Garrincha alizaa naye
watoto wanane wa kike. Wa pili alikuwa Elza Soares ambaye alikuwa mwimbaji wa
muziki asili wa Brazil Samba.
Garrincha alimwoa mwanadada
huyo katika tukio ambalo halikuwa rasmi mnamo Machi mwaka 1966. Mwimbaji huyo
wakati akiingia kwa Garrincha naye alikuwa ameolewa hapo awali.
Waliachana na Garrincha
mnamo mwaka 1977 baada ya miaka 11. Waliachana na Garrincha kutokana na kuwa na
mahusiano na mwanadada mwingine Angelita Martinez ambaye alikuwa mwimbaji
katika majukwaa.
Garrincha anafahamika kwa
kuwa ni baba wa watoto wasiopungua 14.
Nyakati za mwisho za uhai
wake Garrincha alikuwa katika hali tete ya kiuchumi huku matatizo ya
kimahusiano yakiendelea kumsumbua.
Akiwa katika dimbwi la
ulevi alipelekwa hospitalini jijini Rio Janeiro akiwa hajitambui.
Mwaka mmoja kabla umauti
haujamkuta nyota huyo alilazwa mara nane.
Katika miaka yake ya mwisho
katika kuupigania uhai wake Garrincha alikuwa shujaa aliyesahaulika lakini
ibada ya mazishi ilianza kufanyika Uwanja wa Maracana hadi Pau Grande,
mamilioni ya mashabiki walijitokeza kwa wingi kumuaga Garrincha, miongoni mwa
maandishi kuhusu Garrincha yalisomeka, “Pumzika kwa Amani, Uliyekuwa Furaha ya
Watu-Mane Garrincha.”
Katika kuta za mitaa
mbalimbali watu waliandika maandishi, “Obrigado, Garrincha, por você ter vivido”
yaani Asante sana Garrincha, kwa kuishi duniani.”
Uwanja wa michezo katika
makao makuu ya taifa hilo jijini Brasilia, uliitwa kwa jina lake Estadio Mane Garrincha.
Pele na Garrincha enzi zao wakiwa dimbani, Brazil haikuwahi kupoteza mechi ilipokuwa na miamba hii. |
Kuhusu maisha yake ya soka
hususani mwaka 1962 wasanii wa filamu waliyaelezea katika Garrincha, Alegria do
Povo pia mnamo mwaka 2003 katika filamu Garrincha-Estrela Solitaria yaani
‘Lonely Star’ iliyochukua maelezo mengi kutoka katika kitabu kilichoandikwa na
Ruy Castro ambaye alielezea maisha ya Garrincha ndani na nje ya uwanja.
Garrincha alifahamika kwa
kukokota mpira dimbani, kumiliki, hisia na milazo ya kila aina akiwa katika
winga.
Pia Garrincha alikuwa
mahiri kutengeneza nafasi ya kufunga pasipotarajiwa.
Katika suala la mikwaju
mirefu hususani mashuti yenye ujazo alikuwa mahiri pia upigaji wa mipira
iliyokufa.
Garrincha alikuwa akisifika
kwa kupiga mipira iliyokufa hususani kona kwa kutumia upande wa nje wa mguu
wanasoka wa kitanzania hupenda kuita ‘Outer’.
Mwandishi wa habari Scott
Murray aliwahi kuandika katika gazeti la Guardian mnamo mwaka 2010 kuhusu
ukokotaji wa mpira wa nyota huyo, “the bottom line is uncontestable: Garrincha
was the greatest dribbler ever.”
Alikuwa kipenzi cha mashabiki
awapo dimbani hadi kupewa jina la ‘Furaha ya Watu’ kutokana kuwa mtaratibu,
mpole na uwezo wa kuwafanya wachezaji wa timu pinzani wapumbavu kutokana na
manjonjo akiwa na mpira.
Rafiki yake wa karibu
Djalma Santos aliwahi kukaririwa akimwelezea kuwa alikuwa na roho ya kitoto pia
alikuwa kama Charlie Chaplin.
Garrincha anakumbukwa sana,
mchango wake mkubwa aliutoa katika Kombe la Dunia mnamo mwaka 1958 na 1962.
Hata hivyo katika Kombe la
Dunia mnamo mwaka 1962 wakati Pele alipokuwa majeruhi Garrincha alionekana
kuziba pengo hilo ambapo aliiongoza Brazil kutwaa taji hilo.
Garrincha ndiye mchezaji wa
kwanza kutwaa tuzo tatu ndani ya mashindano akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa
mashindano pia Kiatu cha Dhahabu na Kombe la Dunia.
Garrincha alikuwa miongoni
mwa wachezaji waliotajwa katika kikosi cha dunia cha Kombe la Dunia mnamo mwaka
1958 na 1962.
Mnamo mwaka 1994 alitajwa
katika kikosi cha zama zote cha Kombe la Dunia.
Brazil haikuwahi kupoteza
mechi alipokuwapo Pele na Garrincha. Katika ngazi ya klabu aliitumikia
Botafogo. Garrincha alizaliwa Pau Grande katika wilaya ya Mage, Rio de Janeiro
Okotoba 28, 1933.
Wakati Garrincha akizaliwa
mguu wake wa kulia ulikuwa mfupi kuliko wa kushoto kwa sentimeta sita pia mguu
wake wa kushoto uliangalia nje na mguu wa kulia uliangalia ndani hali
iliyomfanya daktari kumwandikia kuwa ni mtoto mwenye ulemavu.
Baba yake alikuwa mlevi wa
kupindukia wa pombe kali maarufu nchini
humo ya Cachaca ambayo hutengenezwa kwa miwa.
Kutokana na kuwa na umbo
dogo kuliko watoto wenzake dada yake aliyefahamika kwa jina la Rosa alianza
kumwita Garrincha.
Jina ‘Garrincha’ ni ndege
mdogo wa rangi ya brauni anayepatikana Kaskazini-Mashariki mwa Brazil.
0 Comments:
Post a Comment