Monday, January 13, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Chiang Ching-Kuo ni nani?


Januari 13, 1988 alifariki dunia mwanasiasa wa China aliyefahamika kwa jina la Chiang Ching-Kuo.

Kiongozi huyo wa kisiasa ni mtoto wa Rais wa zamani wa taifa hilo Chiang Kai-Shek.

Ching-Kuo alishika madaraka hayo katika serikali ya Jamhuri ya China kutoka mwaka 1972 kifo chake. Ching-Kuo alifariki ghafla jijini Taipei huko Taiwan akiwa na umri wa miaka 77 kutokana na maradhi ya moyo.

Mtunzi wa nyimbo wa China Hwang Yau-tai alitunga wimbo wa kumbukumbu kwa ajili ya Ching-Kuo kufuatia kifo chake. Katika masuala ya kisiasa Ching-Kuo hakuwa na misimamo kama ya baba yake Chiang Kai-Shek, kwani alijijenga katika sera za upinzani wakati wa uchaguzi wa Taiwan.

Pia Ching-Kuo ataendelea kukumbuka kutokana na uwazi na juhudi zake katika maendeleo ya kiuchumi. Mwanasiasa huyo wakati akikua alipelekwa kusoma nchini Urusi mnamo mwaka 1925 wakati huo uhusiano wa kisiasa baina ya Chama cha Nationalist ambayo baba yake alikuwa mwenyekiti yalikuwa mazuri na Chama cha Kikomunisti cha Wachina.

Alisoma elimu ya chuo kikuu na mara baada ya wanachama wa Nationalist kuvunja mahusiano baina yao Joseph Stalin aliyekuwa kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti alimpeleka Ching-Kuo kufanya kazi katika kiwanda cha chuma huko katika Milima ya Ural.

Huko ndiko alikokutana na mwanadada Faina Vakhreva na kumuoa. Wakati wa vita baina ya China na Japan ilipokuwa kali mnamo mwaka 1937 Stalin aliwarudisha Ching-Kuo na mkewe nchini China.

Wakati wa vita baba yake ndipo alipoweza kumwamini Ching-Kuo na hivyo alimpa majukumu ya kufanya ikiwamo masuala ya utawala.

Baada ya Wajapan kusalimu amri; Ching-Kuo alipewa kazi ya kupambana na rushwa katika maeneo ya Shanghai, ambako alifanya kazi nzuri.

Ushindi wa Wakomunisti mnamo mwaka 1949 uliwafanya ukoo mzima wa kina Chiang na serikali yao kwenda zao Taiwan.

Ching-Kuo alikuwa wa kwanza kushika madaraka ya askari wa siri nafasi aliyokaa nayo hadi mwaka 1965. Baada ya hapo akawa Waziri wa Ulinzi kuanzia 1965 hadi 1969.

Baada ya kifo cha baba yake mnamo mwaka 1976 Ching-Kuo alichukua madaraka ya kukiongoza chama cha Nationalist akiwa mwenyekiti; hapo ndipo mwaka 1978 alichaguliwa kuwa Rais.  

Ching-Kuo mvumilivu katika masuala ya kisiasa pia aliruhusu watu wa kundi hasimu la Han katika siasa za China kupata nafasi za uongozi akiwamo Lee Teng-hui ambaye alikuja kuwa Rais wa Jamhuri ya China aliyezaliwa Taiwan.

Ching-Kuo alizaliwa Fenghua, huko Jiànfēng Aprili 27, 1910.


0 Comments:

Post a Comment