Mbaraka
Mwinshehe alikuwa ni mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi hapa nchini
Tanzania.
Alizaliwa katika mjini Morogoro; Juni 27, 1944. Mbaraka Mwinshehe
alikuwa mtoto wa pili kati ya watoto 12 wa Mzee Mwaruka. Baba yake Mzee
Mwinshehe Mwaruka alikuwa Mluguru msomi na karani katika mashamba ya katani, na
mama yake alikuwa Mngoni.
Kati ya hao kumi na mbili, ni yeye na wadogo zake
Zanda na Matata ndio walikuwa wanamuziki, Zanda alikuwa mwimbaji, akiimba pia
nyimbo za kizungu katika bendi ya Morogoro na Matata alikuwa mpiga drum pia
bendi hiyohiyo.
Kutokana maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa wa
kabila la Wadoe wa Bagamoyo na alipelekwa Mzenga (Kisarawe) akawe chifu wa huko
na wakoloni.
Huko akaoa wake tisa na kupata watoto zaidi ya hamsini akiwemo
baba yake Mbaraka, Mzee Mwaruka.
Mbaraka alisoma mpaka kidato cha tatu na
kuacha shule ili awe mwanamuziki.
Mbaraka Mwinshehe alianza kushiriki katika
maonyesho ya Morogoro Jazztangu akiwa shule, wakati huo alipenda kupiga sana
filimbi katika mtindo wa kwela kutoka Afrika ya Kusini ukiwa na wapulizaji
maarufu kama Spokes Mashiyan, na ulipendwa sana na vijana haswa wa shule na
makundi mengi ya jiving yalikuweko katika shule za sekondari.
Hivyo alishiriki
akiwa mpigaji wa filimbi wakati wa wikiendi. Siku moja kwenye mwaka 1965,
wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya klabu yao Mbaraka
alipita akiwa na begi kubwa walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa
kuwa shule, aliwaambia kuwa hataki tena shule anaenda Dar es Salaam kutafuta
maisha, walimsihi alale pale klabuni kwanza awaze hatima yake.
Kesho yake wanamuziki
walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa kwani walikuwa
wakimfahamu kama mpiga filimbi, kwa kuwa walikuwa na shida ya mpiga rhythm
walimsihi aache safari ya Dar na abaki kwenye bendi kama mpiga rhythm,
akakubali.
Wakati huo ni wapiga tarumbeta, saxaphone na gitaa la solo pekee
waliokuwa wanalipwa kwa mwezi, wengine wote walipata posho kidogo kila
lilipopigwa dansi. Siku ya Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania
ulitikiska kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha mwanamuziki huyo, mpiga gitaa
muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake
ilikuwa imepiga karibu kila wilaya ya nchini Tanzania.
Taarifa ziliingia jioni
ya siku ile kupitia redio ya Taifa kuwa nguli huyu alifia katika hospitali
katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya
gari.
Kwa maelezo ya Zebedee Japhet Kinoka au maarufu kama Super Zex ni
mwanamuziki mkongwe, Januari 12, 1979 alikuwa anatoka maeneo ya
Kisauni kumtembelea Mtanzania mwenzake aliyekuwa na hoteli huko, ambaye pia
walitoka kijiji kimoja Maramba huko Tanga.
Alisema alipofika karibu na Kongoya
Church aliona gari aina ya Peugot 404 nyeupe ikitoka upande wa Bush Bar na kwa
spidi kali ikaenda na kuligonga lori moja lililokuwa likitokea upande mwingine.
Mbaraka alifariki dunia siku hiyo ya Ijumaa ya Januari 12, 1979 akiwa na umri mdogo wa miaka 34 tu.
Kwa
kuwa mpaka wa Kenya na Tanzania ulikuwa umefungwa wakati huo kutokana na
mgogoro kati ya serikali za nchi hizi mbili, mwili wa Mbaraka alisafirishwa
mpaka mpakani na kupokelewa na ndugu marafiki na Maafisa wa Wizara ya
Utamaduni. Mbaraka Mwinshehe alizikwa Mzenga, Kisarawe.
0 Comments:
Post a Comment