Monday, January 6, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Theodore Roosevelt ni nani?


Januari 5, 1919 alifariki dunia rais wa 26 wa Marekani Theodore Roosevelt. Huyo alikuwa mwanasiasa, na mwandishi wa vitabu. 

Alifariki dunia kutokana na matatizo ya kupumua ambayo yalikuwa yakimsumbua tangu akiwa mtoto. Baada ya kupata matibabu kutoka kwa daktari George W. Faller alionekana kupata nafuu hivyo akaenda zake kulala. 

Maneno yake ya mwisho kabla ya kifo chake alisema, “ Tafadhali zima taa James.” Alikuwa akimwambia mfanya kazi wake aliyefahamika kwa jina la James Amos. 

Kati ya saa 10:00 na saa 10:15 alfajiri Roosevelt alifariki dunia akiwa katika usingizi huko Sagamore Hill. 

Inaelezwa kwamba damu iliganda katika mojawapo ya misuli hali iliyosababisha apumue kwa shida  kutokana na damu kushindwa kwenda kwenye mapafu. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 60. 

Wakati taarifa zilipotolewa kuhusu kifo chake mtoto wake Archibald alisema, “ Simba wa Mzee amefariki dunia”. 

Makamu wa Rais wakati huo katika utawala wa Woodrow Wilson, Thomas R. Marshall alikaririwa akisema Roosevelt amefariki dunia akiwa usingizini na kama angeamka angeendelea kupigania uhai wake. 

Mazishi yake yalifanyika katika Kanisa la Christ Episcopal huko Oysterbay. Viongozi wa kisiasa wakiwamo Thomas R. Marshall, Charles Evans Hughes, Warren G. Harding, Henry Cabot Lodge, na William Howard Taft walikuwa miongoni mwa waombolezaji. 

Theodore Roosevelt alizikwa katika makaburi ya Youngs Memorial. Kiongozi huyo alizaliwa Oktoba 27, 1858 katika mtaa wa 20, 28 East huko Manhattan jijini New York akiwa ni mtoto wa pili kati ya wanne wa Martha Stewart Bulloch na Theodore Roosevelt Sr. 

Alikuwa na dada zake Anna, Corinne na mdogo wake wa kiume Elliott. Alikuwa rais wa Marekani kuanzia mwaka 1901 hadi 1909 kabla ya hapo alikuwa gavana wa Jimbo la New York kutoka mwaka 1899 hadi 1900 pia makamu wa rais wa 25 wa Marekani kutoka Machi hadi Septemba mwaka 1901.

0 Comments:

Post a Comment