Januari 18, 2001 alifariki
dunia Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) Laurent-Desire Kabila.
Mwanasiasa huyo aliyeingia kwa mtutu wa bunduki kuchukua madaraka hayo baada ya
kuuangusha utawala wa Mobutu Sese Seko. Aliuawa akiwa ofisini hali ambayo
ilitaka kuliingiza taifa hilo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mamlaka za
usalama nchini humo zilijitahidi kuweka utulivu licha ya mauaji hayo.
Kwa
mujibu wa Waziri wa Afya wakati huo Leonard Mashako Mamba alisema Kabila
aliuawa na kupoteza maisha papo hapo.
Waziri huyo aliongeza kuwa wakati akiuawa
yeye alikuwa mlango wa pili na kwamba aliposikia kishindo alikimbia haraka
kwenda kwenye tukio. Awali ilielezwa kuwa aliwahishwa hospitalini nchini
Zimbabwe.
Serikali ya DRC ilitangaza Januari 18, 2001 kuwa Kabila alifariki kwa
majeraha ya risasi mwilini mwake. Wiki moja mwili wake ulirudishwa nchini humo
kwa ajili ya maziko na siku 10 baadaye mtoto wake Joseph Kabila alikuwa Rais wa
taifa hilo.
Uamuzi huo ulifikiwa baada ya ushuhuda wa mdomo uliotolewa na
Waziri wa Sheria na Haki wakati huo Mwenze Kongolo kuwa Laurent-Desire Kabila
aliwahi kuwaambia kwa mdomo maafisa wake kuwa endapo atauawa akiwa ofisini basi
mtoto wake Joseph atachukua mahali pake.
Hivyo walitimiza matakwa ya marehemu
na Joseph akawa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Uchunguzi kuhusu
mauaji wa mwanasiasa huyo uliwapandisha kizimbani watu 135 wakiwamo watoto
wanne.
Kanali Eddy Kapend ambaye alikuwa miongoni mwa mabinamu wa Kabila na
wengine 25 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa Januari 2003 lakini hawakunyongwa.
Wengine 64 walitupwa jela kuanzia miezi sita hadi kifungo cha maisha na wengine
akali ya 45 waliachiwa huru.
Pia kutokana na mauaji hayo wengine walikumbana na
mkono wa sheria kwamba walitaka kumuua mtoto wake ili asiweze kukalia kiti
hicho, miongoni mwa hao alikuwa mshauri wa karibu na muhimu wa Kabila
aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Dungia ambaye aliwahi kuwa balozi wa zamani
nchini Afrika Kusini.
Walio wengi wanaamini hadi leo kwamba wengi wa
waliohukumiwa ni wasio na hatia. Kabila aliingia madarakani mnamo mwaka 1997.
Enzi
za utawala wake alikuwa mfuatiliaji wa siasa za Marx lakini sera zake
alizichanganya na Ubepari na Ujamaa.
Kabila aliwahi kutangaza kwamba uchaguzi
hautafanyika nchini humo kwa miaka miwili ili aweze kupata muda wa kupanga
vizuri utaratibu nchini humo. Sera za Kabila zilitofautiana na mtangulizi
wake kwani zilijawa na ubabe, rushwa na
ukiukwaji wa haki za binadamu.
Miaka ya mwanzoni wakati wa utawala wake alianza
kufahamika kwa jina la ‘Mobutu mwingine’.
Mnamo mwaka 1998 waliokuwa washirika
wake nchini Uganda na Rwanda walimgeuka na kutaka mapinduzi kwa tiketi ya Rally
for Congolese Democracy (RCD) ambayo ilileta vita ya pili ya Kongo. Hata hivyo
Kabila alipata washirika wapya Angola, Namibia na Zimbabwe.
Kupata kwake washirika wapya kulimsaidia sana
Kabila kushikilia upande wa Kusini na Magharibi mwa DR Congo. Mnamo Julai 1999
mazungumzo ya amani yalifanyika ambayo yaliondoa majeshi mengi ya kigeni nchini
humo.
Harakati za kutaka kiti hicho zilianza tangu miaka ya 1960 hadi
alipofanikia miongo mitatu baadaye. Laurent-Desire Kabila alizaliwa Novemba 27,
1939 mjini Baudouinville katika jimbo la Katanga ambapo kwa sasa kunafahamika
kwa jina la Moba katika Jimbo la Tanganyika. Kabila ni mtu wa jamii ya Waluba.
Baba yake alikuwa Mluba na mama yake alikuwa wa jamii ya Walunda.
Kabila aliwahi
kusema kuwa alisoma Falsafa ya Siasa jijini Paris, PhD yake aliipata Tashkent,
Belgrade na Dar es Salaam; lakini hakuna uthibitisho kuwa alipita huko.
0 Comments:
Post a Comment