Septemba 27, 1954 alizaliwa
Mhubiri wa Neno la Mungu, Mwandishi wa vitabu vya Kikristo, Mfanyabiashara, Mhandisi
wa ujenzi na mwanzilishi wa Kanisa la Faith Tabernacle lililopo Ota katika
jimbo la Ogun nchini Nigeria na mwanzilishi wa Huduma ya Living Faith Worldwide
maarufu Winners Chapel International Bishop David Oyedepo.
Alizaliwa mjini Osogbo nchini Nigeria. Jina
lake halisi ni David Olaniyi Oyedepo. Oyedepo alikulia katika familia ya
kidini. Baba yake alikuwa mwislamu, mama yake aliyefahamika Dorcas alikuwa
muumini wa kanisa la Holy Order of Cherubim and Seraphim Movement tawi la
Aladura huko nchini Nigeria. Oyedepo alikulia kwa bibi yake mjini Osogbo ambaye
alimfundisha mambo mengi kuhusu Mungu. Oyedepo aliokoka mwaka 1969 wakati huo
akiwa na miaka 15 kutokana na msukumo alioupata kutoka kwa mwalimu wake aliyefahamika
kwa jina la Betty Lasher. Alisomea masomo ya Usanifu wa Majengo katika Chuo cha
Kwara State Polytechnic. Pia aliwahi kufanya kazi katika Wizara ya Nyumba mjini
Ilorin kabla ya kuacha na kuendelea na wito wake wa kimisheni. Alipata shahada
ya uzamivu nchini Marekani katika Chuo Kikuu cha Honolulu, Hawaii. Oyedepo
aliwahi kusema alipokea upako na maono kutoka kwa Mungu ambaye alizungumza naye
kwa saa 18 mnamo Mei 1981. Maono hayo yalikuwa kwa ajili ya watu wanaokandamizwa
na Ibilisi. Maono hayo ndiyo yaliyosababisha kuanzishwa kwa huduma ya Winners
Chapels International. Mnamo mwaka 2011 Jarida la Forbes lilimtaja Oyedepo kuwa
ni Mchungaji mwenye Utajiri mkubwa nchini Nigeria. Oyedepo amekuwa akitoa
huduma kupitia Winners Chapel zaidi ya miji 300 duniani kote ambapo barani
Afrika yupo katika nchi 45. Pia ameenda hadi Dubai, Uingereza na Marekani.
Mbali ya kuwa ni mtumishi wa Bwana kwa sasa ni Kansela katika Chuo Kikuu cha
Covenant na Landmark vilivyopo nchini Nigeria.
0 Comments:
Post a Comment