Tuesday, September 24, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Zitto Kabwe ni nani?


Septemba 24, 1976 alizaliwa mwanasiasa wa Tanzania Zitto Zuberi Kabwe Ruyagwa. Kwa sasa ni mlezi wa chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo).

Elimu ya msingi alianza 1984 na kuhitimu mwaka 1990 katika Shule ya Msingi Kigoma. Kisha akaenda sekondari ya Kigoma ambayo alianza 1991 hadi 1994 na baadaye katika shule ya sekondari Kibohehe ya Mkoani Kilimanjaro mwaka 1994 hadi 1995.

Mnamo mwaka 1996 alitua kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Galanos iliyopo mkoani Tanga, hata hivyo hakufanikiwa kumalizia hapo, kidato cha sita alimalizia katika Sekondari ya Tosamaganga mnamo mwaka 1998.

Aliingia kuchukua masomo ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mnamo mwaka 1999 na kuhitimu mwaka 2003.

Mnamo mwaka 2003 alitua nchini Ujerumani ambako alikwenda kusomea Stashahada ya Juu ya Masoko ya Kimataifa huko Inwent –IHK mjini Bonn. Masomo hayo alihitimu mwaka 2004.

Zitto Kabwe hakurudi Tanzania alisalia nchini Ujerumani ambako alisomea shahada ya uzamili katika masuala ya sheria katika Shule ya Sheria ya Bucerius iliyopo Hamburg ambako alihitimu masomo hayo mwaka 2010.

Aliingia tena darasani kuchukua uzamivu katika chuo Otto Beisheim kilichopo Vallendar na Dusseldorf huko huko nchini Ujerumani.

Katika masuala ya siasa Zitto Kabwe akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwahi kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) mwaka 2002 hadi 2003.

Mnamo mwaka 2004 aliingia rasmi katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mwaka uliofuata aliwania ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya chama hicho na kusalia hadi leo.

Licha ya kubadili chama Zitto Kabwe amekuwa na ushawishi mkubwa awapo bungeni na Tanzania kwa ujumla.

Alipokuwa mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Mandeleo (Chadema) pia alipokuwa Chadema aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Ofisi ya Masuala ya Kimataifa.

Mwaka 2015 alijiuzulu bungeni, akatoka katika Chadema na kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo). Katika uchaguzi wa 2015 alichaguliwa upya bungeni kama mgombea wa chama hiki.

0 Comments:

Post a Comment