Friday, September 27, 2019

Rwanda yapokea kundi la kwanza la wakimbizi kutoka Libya


Kundi la kwanza la wakimbizi wa Libya limewasili jijini Kigali. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema raia 66 wa Libya wanaotafuta makazi limewasili nchini Rwanda na litawekwa kaskazini mwa taifa hilo katika mpango mpya wa kuwahifadhi wakimbizi. 

Programu hiyo mpya inakuja baada ya Rais Kagame mnamo mwaka 2017 kutoa ruhusa kwa wakimbizi wa Afrika wanaotafuta makazi kuja nchini mwake badala ya kukimbilia barani Ulaya. 

Mwanzoni mwa mwezi huu Rwanda ilisaini mkataba mpya na Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Wakimbizi la Kimataifa (UNHCR) wa kupokea wakimbizi wa Afrika kutoka nchini Libya. Serikali ya Rwanda imejiandaa kupokea wakimbizi 30,000 japokuwa mpango huo utakwenda kwa awamu 500 ili kuondoa taswira ya raia wake kuonekana kama wanaonewa. Katika akaunti ya twitter ya UNHCR imeandikwa kundi la kwanza wanawake wenye watoto na baadhi ya familia zimewasili katika jiji la Kigali. 

Aidha katika taarifa hilo iliwekwa bayana kuhusu mkimbizi mmoja ambaye ametua Kigali akiwa na mtoto wa miezi miwili aliyezaliwa kwa wazazi wenye asili ya Somalia waliokuwa wakiishi Libya. 

Hata hivyo kuna taaifa nyingine kuwa kutakuwa na ndege nyingine ambaye itabeba watu 125 itakayotua kati ya Oktoba 10-12 mwaka huu. 

Pia wakimbizi hao watawekwa katika makazi maalumu kabla ya kuwaachia huru mpaka wakubali kurudi katika mataifa yao. Katibu Mkuu wa Wizara ya Usimamizi wa Dharura Olivier Kayumba Rugina amesema wakimbizi hao watapewa malazi, chakula, elimu na huduma za kifya na UNHCR. 

Rugina ameongeza baada ya taratibu kukamilika za kuwapokea watapewa vitambulisho kama wakimbizi wengine wanavyofanyiwa. Wakimbizi hao watakaa katika Kambi ya Gashora iliyopo Wilaya Bugesera ikiwa ni kilometa 60 kutoka jijini Kigali. 

Kambi hiyo ilianzishwa mwaka 2015 kwa madhumuni ya kuwahifadhi wakimbizi kutoka Burundi waliokimbia vurugu na machafuko nchini mwao. 

Akali ya wakimbizi 30,000 walihifadhi katika kambi hiyo ya Gashora. Wakimbizi waliopokelewa nchini Rwanda kutoka Libya wamefika hapo kutokana na machafuko yaliyojitokeza baada ya kuondolewa kwa Muammar Gaddafi katika mapinduzi yaliyofanyika mwaka 2011. Hadi sasa Umoja wa Mataifa umesema wakimbizi 42,000 wapo nchini Libya.

Rais Kagame amechukua majukumu hayo baada ya kituo cha televisheni cha CNN kuripoti kuwa wakimbizi walioko Libya ni kama watumwa katika ardhi yao. 

Itakumbukwa Julai mwaka huu zaidi ya watu 40 waliuawa kutokana na shambulio la anga lililofanywa katika kituo cha wahamiaji kwenye mji wa Tajoura nchini Libya. Mnamo 2017 Umoja wa mataifa ulipinga mpango wa wakimbizi kuwaweka upande nchini Niger. Aidha Maofisa nchini Rwanda wamesema wamejifunza kutoka Niger. 

Jumuiya ya Afrika Mashariki imepongezwa kwa kuwa na uwazi katika suala la wakimbizi. Uganda inawahifadhi wakimbizi 800,000 kutoka Sudan Kusini na nchini nyingine katika ukanda huo zimekuwa zikiwahifadhi kutoka Burundi, Somalia na kwingineko. 

Hadi mwishoni mwa mwaka 2018 nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zilikuwa zikiwahifadhi wakimbizi akali ya milioni nne.

0 Comments:

Post a Comment