Saturday, September 14, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Dmitry Medvedev ni nani?

Dmitry  Medvedev

Septemba 14, 1965 alizaliwa Rais wa zamani wa Russia Dmitry  Medvedev ambaye ni mwanasiasa aliyehudumu kama waziri mkuu wa Russia tangu mwaka 2012. 

Medvedev alihudumu kama Rais wa taifa hilo kubwa ulimwenguni  mwaka 2008 hadi 2012. Kiongozi huyo amekuwa akichukuliwa kama mpenda uhuru na usawa katika jamii kuliko Rais wa sasa wa taifa hilo Vladmir Putin. Wawili hawa wamekuwa wakichukuliwa kama waendeshaji wa demokrasia ya Tandem kwani wakati wa utawala wa Medvedev, Putin alikuwa Waziri Mkuu na sasa Rais ni Putin na Medvedev ndiye Waziri Mkuu. Medvedev alizaliwa Leningrad, USSR. Baba yake aliyefahamika kwa jina la Anatoly Afanasyevich Medvedev (1926 – 2004), alikuwa mhandisi wa masuala ya Kemia katika Taasisi ya Teknolojia ya Leningrad. Mama yake anayefahamika kwa jina la Yulia Veniaminovna Medvedeva (Novemba 21, 1939) mwalimu katika chuo kikuu cha Herzen ambapo baadaye alifanya kazi kama muongozaji wa watalii. Wazazi wake walijaliwa kupata mtoto mmoja ambaye ni Dmitry Medvedev. Akiwa mtoto Medvedev alikuwa akipenda kujisomea na kusoma vitabu. Mwalimu wake wa kwanza aliyefahamika kwa jina la Vera Smirnova alimweleza Medvedev  kuwa ni mtoto mwenye akili aliyependa kuuliza kile asichokijua. Baada ya muda wa masomo kumalizika alikuwa akitumia muda kucheza na wenzake  kabla hajaenda kumalizia kazi alizopewa na mwalimu. Hata hivyo Medevedev aliwahi kukaririwa akisema hakuna mwaka aliuona mgumu katika masomo kama mwaka 1982 wakati wa mitihani yake ya mwisho. Tukiangazia upande wake wa kisiasa alipokuwa Rais wa Russia alikuwa akijitahidi kuipeleka Russia katika ukisasa ili kuufanya uchumi wa taifa hilo kukua huku akijikita katika masuala ya mafuta na gesi. Enzi za utawala wake ndipo kuliposhuhudiwa mkataba baina ya Russia na Marekani kuhusu kupunguza matumizi ya nyuklia uliposainiwa. Pia Russia iliibuka mshindi wakati wa vita yake na Georgia na uchumi ulirudi mahali pake huku akipambana vikali dhidi ya rushwa.

0 Comments:

Post a Comment