Monday, September 30, 2019

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni nchi ya namna gani?


Taifa hili limekuwa likifahamika kama Congo Kinshasa baada ya kubadilishwa kutoka Zaire jina ambalo lilitumika kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1997; wakati wa utawala wa Mobutu Sese Seko. 

Ni miongoni mwa nchi kubwa katika bara la Afrika ikiwa ya kwanza iliyopo china ya Jangwa la Sahara. Ina idadi ya watu takribani milioni 80 na kuwa nchi ya kwanza yenye watu wengi katika ukanda wa nchi zinazongumza Kifaransa na nchi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya watu barani Afrika. 

Kwa kiwango hicho Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inashika nafasi ya 16 duniani. Katika eneo la mashariki mwa taifa hilo limekuwa na matukio yasiyoisha ya migogoro ya kijeshi katika Kivu tangu mwaka 2015. Lugha zinazotumika katika taifa hilo ni Kifaransa, Kikongo, Kiswahili na Tshiluba. 

Nchi imepakana na Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Uganda, Rwanda, Burundi, Tanzania, Zambia na Angola. Ina sehemu ndogo ya pwani kwenye Bahari ya Atlantiki. 

Sehemu hiyo inatenganisha eneo la Cabinda kutoka maeneo mengine ya Jamhuri ya Angola. Eneo lote ni la kilometa mraba 2,345,409 na linafanya Kongo iwe nchi ya 11 duniani kwa ukubwa wa eneo. 

Taifa hilo lina mikoa 26 na wananchi wengi (zaidi ya 80%) wanajihesabu Wakristo wa madhehebu mbalimbali; kati yao asilimia 36.8 ni Wakatoliki. Waislamu ni asilimia 10-12. Wafuasi wa dini asilia za Kiafrika ni 3%. 

Januari mwaka huu taifa hilo liliingia katika zama mpya baada ya kumpata rais katika sanduku la kura ambapo Felix Tshisekedi alipokea kijiti kutoka kwa Joseph Kabila. Uchaguzi wa kumpata Tshisekedi ulifanyika Desemba 30, 2018. 

Tume ya taifa ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, CENI, ilitangaza ushindi wa Tshisekedi  Alhamisi, alfajiri ya Januari 10 mwaka huu. 

Ushindi huo uliwashtua wengi ambao walishuku huenda matokeo yangebadilishwa ili mgombea wa muungano wa vyama tawala, Emmanuel Ramazani Shadary awe ndiye mshindi. Baada ya kutangazwa mshindi, Felix Tshisekedi alisema anatoa heshima zake kwa Rais Joseph Kabila, ambaye amesema anamchukulia kama mshirika muhimu kisiasa. 

Mpaka sasa licha ya changamoto za taifa hilo lakini Tshisekedi ameendelea kuwa mtulivu katika kusuluhisha na kuweka sawa mambo mbalimbali hali inayoashiria zama mpya.

Imetayarishwa na Jabir Johnson…….Septemba 30, 2019.


0 Comments:

Post a Comment