Thursday, September 26, 2019

Mgogoro wa ardhi Nyabiraba wazua hofu Burundi



Familia mbili zimesema zipo kwenye hofu ya kuuawa baada ya kundi la watu kukata migomba yao juzi jumatatu (Septemba 23, 2019) na kuwatishia kuwaua endapo watarudi katika ardhi hiyo. 

Familia hizo zinazoishi katika kitongoji cha Raro, Nyabiraba jijini Bujumbura zimetishiwa na watu kutoka Mutambu. 

Gazeti la Iwacu limesema ulinzi kuhusu maisha yao haujatolewa mpaka sasa  baada ya mashamba yao ya migomba na ndizi kufyekwa na hadi sasa hawalali katika nyumba zao. 

Aidha familia hizo zimesema licha ya kitisho cha uhai wao lakini pia kitisho cha njaa kinawakabili kwa sasa na baadhi ya wanafamilia wameshakimbia makazi hayo kwa kuhofia kupoteza maisha. 

Kikongwe aliyefahamika kwa jina la Angeline Bandyambona amesema siku ya tukio majira ya saa moja asubuhi watu ambao hawafahamu walikwenda katika shamba lake wakiwa na mapanga na kuanza kukata migomba yake na baada ya kufanya hivyo walisema watarudi kuwaua. 

Hata hivyo kikongwe huyo amedai kuwa watu hao wanatoka katika jamii ya Mutambu iliyopo katika kitongoji cha Raro. Aidha Bandyambona amesema awali kulikuwa na ugomvi wa ardhi na familia moja ya Mutambu. 

Alex Nahimana mwenye umri wa miaka 52 ni mtoto wa kiume wa kikongwe na baba wa watoto saba amesema wanachosubiri kwa sasa ni sheria ifuate mkondo wake. 

Mwanafamilia mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Rosalie Nahabandi ambaye ni mama wa watoto 8 amesema watu hao kutoka Mutambu walifika na kukata migomba na mbogamboga hali ambayo inawawia vigumu kupata chakula hadi sasa pia wana hofu ya kuuawa na watu hao. 

“Hatulali ndani ya nyumba zetu, tunashinda usiku mzima msituni,” amesema Rosalie. 

Uongozi wa Kitongoji cha Raro umesema utawala unalifahamu sakata hilo na kwamba taarifa walipata kuhusu familia kutoka Mutambu kufanya kitendo hicho na kwamba familia iliyokwenda kukata migomba katika ardhi ya familia nyingine ina nyaraka kutoka wizarani ambazo mamlaka za chini hazina uwezo wa kuingilia suala hilo. 

Imeelezwa mgogoro wa ardhi katika jamii hizo mbili ulianza mwaka 1984 na jalada la kesi hiyo lipo katika Wizara ya Sheria.

CHANZO: IWACU

0 Comments:

Post a Comment