Wednesday, September 25, 2019

Kagame: Afrika yenyewe ndio chanzo cha suluhu ya matatizo yake


 Rais Paul Kagame wa Rwanda ameuambia mkutano wa Umoja wa wa Mataifa jijini New York kuwa Afrika imeonyesha uwezo wa maendeleo yake yenyewe licha ya changamoto kujitokeza. 

Kagame ameuelezea mtazamo wake kwa viongozi wenzake katika mkutano unaoendelea nchini Marekani kuwa Afrika imekubaliana na kuipa kipaumbele program ya kimataifa ya masuala ya Afya. 

Kiongozi huyo amesema nchini Rwanda zaidi ya asilimia 90 ya watu wa taifa lake wana bima za afya. Mpango huo wa Afya kwa ulimwengu umedhamiria ifikapo 2030 suala la Afya liwe siyo taarifa ya kustaajabisha. Kagame amesema malengo ya Umoja wa Mataifa ya 2030 yana maana kubwa kwa Afrika na ni wajibu wa mataifa ya Afrika kuwajibika katika malengo hayo. 

Kagame amesema hiyo ndiyo sababu inayoufanya Umoja wa Afrika (AU) kuendelea kuweka msisitizo wake katika malengo hayo. Kagame amesisitiza kuwa ukuaji wa uchumi katika mataifa ya Afrika utafanya pengo la usawa baina ya taifa moja na jingine kupungua. 

Mapema Kagame aliuambia mkutano huo kuwa ugunduzi  wa teknolojia mbalimbali usiwe kikwazo cha kukua kiuchumi kwa mataifa mbalimbali. Hata hivyo Kagame amewataka viongozi hao kuhakikisha usalama na utulivu kuwa kipaumbele ili kuhakikisha malengo hayo ya 2030 yanafikiwa kwa ukamilifu wake. 

Kagame hakusita kuonyesha hisia zake katika mshikamano baina ya taifa lake, Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR) na Umoja wa Afrika kuwa ni dalili nzuri ya roho ya mshikamano katika kufikia malengo hayo.  “Afrika yenyewe ndio chanzo cha suluhu ya matatizo yake,” ameongeza Kagame. Kagame ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wajumbe wa mkutano wa Kimataifa wa Jinsia ambao utafanyika jijini Kigali mwezi Novemba mwaka huu.

0 Comments:

Post a Comment