Thursday, September 26, 2019

Ntahorwamiye: Burundi ni nchi ya Kidemokrasia

Msemaji wa Serikali ya Burundi Prosper Ntahorwamiye

Msemaji wa Rais Pierre Nkurunziza Jean Claude Karerwa amesema kauli za Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini humo kuelekea uchaguzi mkuu 2020 ni utaratibu wao wa kila siku. 

Katika mkutano na waandishi wa habari  ambao umefanyika jana katika Jimbo la Rumonge amesema watazungumza tena kabla ya uchaguzi mkuu wa 2020.

Karerwa amesema serikali ya Burundi inaheshima mchango na maendeleo makubwa ya Kanisa Katoliki nchini humo kutokana na kuchangia pakubwa katika sekta ya elimu na miundombinu. 

Katika hotuba ya maoskofu hao Jumapili iliyopita walisema kinachoendelea katika taifa hilo kwa sasa ni kukosekana kwa uvumilivu wa kisiasa ambao umesababisha mauaji na kushikiliwa na vyombo vya dola kwa wapinzani wa serikali iliyoko madarakani hasa ikizingatiwa taifa hilo linatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu mwaka ujao. 

Aidha maaskofu hao waliinyoshea kidole cha lawama mahakama nchini humo kwa kuchelewa kutoa hukumu kwa wahusika wanaopatikana na makosa. Pia maaskofu hao walitoa maoni yao kuhusu mwingiliano ambao umejitokeza usio na afya kwa siasa ya taifa hilo kwa chama kinachotawala na utawala. 

Msemaji wa serikali Prosper Ntahorwamiye amesema kilichofanywa na maaskofu hao ni jambo muhimu na la kawaida kwani Burundi ni nchi ya kidemokrasia na kwamba watu mbalimbali wanatoa maoni yao.
Msemaji wa Rais wa Pierre Nkurunziza Jean Claude Karerwa.
    

0 Comments:

Post a Comment