Sunday, September 22, 2019

Wakuu wa Mikoa, Wilaya wapewa kibarua kizito na Waziri Mkuu Majaliwa kuhusu Madini


Waziri Mkuu  Kasim Majaliwa, amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya, kwenye maeneo yao ambako yameanzishwa masoko ya madini kuhakikisha kwamba masoko hayo ya madini, yanalindwa kwa nguvu zote ili kudibiti utoroshwaji wa madini hayo.

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa, aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya pili ya Sekta ya Madini yaliyofanyika Mkoani Geita katika viwanja vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kalangalala katika mji wa Geita.

“Natoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya maeneo yote ambayo serikali imeweka masoko ya madini kuanzia ngazi za Mikoa na Wilaya, hakikisheni mnakwenda kila wakati kujiridhisha na yanawekewa ulinzi wa kutosha,”alisema Waziri Mkuu.

Aidha alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika maeneo ya uyeyushaji na uchachuaji , lengo likiwa ni kuona shughuli hizo zinafanyika hapa nchini ili kutengeneza ajira nyingi kwa Watanzania.

“Mpango wa serikalia ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha Watanzania wanapata ajira kwenye Sekta zote za ndani hata kama wawekezaji hao ni kutoka nje kwenye eneo la ajira linasimamiwa vizuri,”alisisitiza.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa, alisema hali ya uzalishaji wa madini hususan dhahabu imeendelea kuimarika vizuri hapa nchini.

Alisema katika kipindi cha kuanzia Machi 2019 hadi Septemba 7 mwaka huu jumla ya kilo 1573 zenye thamani ya takribani bilioni 145.46 zilishazalishwa na kuuuzwa katika soko la mji wa Geita.

Aidha alisema serikali  imeweza kukusanya kiasi cha Sh bilioni 10.18 kupitia kodi ambapo soko la Geita pekee linaongoza katika uzalishaji wa madini ya dhahabu  na kwamba linachangia wastani wa asilimia 43.1 ya dhahabu yote inayouzwa kwenye masoko yaliyopo hapa nchini.

STORY BY: Kija Elias, aliyepo Geita......Septemba 22, 2019

0 Comments:

Post a Comment