Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya watu wote wakiwemo
wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao wanajihusisha na utoroshaji wa
madini, waache mara moja, Serikali ipo makini imejidhatiti vya kutosha na
kwamba haitokuwa na huruma dhidi yao.
Serikali imefuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT-18%) na
kodi ya zuio (withholding tax-5%) kwa wachimbaji watakaouza madini kwenye
masoko yalioanzishwa nchini ikiwa ni mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji
wadogo ili waweze kuongeza uzalishaji na hivyo kujiongezea tija na kuchangia
katika pato la Taifa.
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo Jumapili, Septemba 22,
2019, wakati akifungua maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta
ya Madini yanayofanyika kwenye uwanja wa CCM Kahangalala mjini Geita. Amesema
kwa wale wasiotaka kuelewa na kuacha kutorosha madini Serikali itashughulika
nao.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto
wanazokutana nazo wachimbaji wadogo ikiwemo matumizi ya teknolojia duni katika
uchimbaji na uchenjuaji madini. “Nitoe wito kwa wadau kuitumia fursa ya
uwekezaji kwa kuanzisha biashara ya vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji
nchini.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wadau wa
madini kuwa katika mkutano wa 16, wa Bunge la 11 lilijadili na kuridhia Azimio
la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu kupunguza kwa kadiri iwezekanavyo
matumizi ya zebaki ifikapo 2030.
Amesema lengo la mkataba huo ni kuanza kupunguza na hatimaye
kuacha matumizi ya zebaki kwenye uchenjuaji wa dhahabu hususan kwa wachimbaji
wadogo. Kwa mantiki hiyo, amewasihi wachimbaji wadogo kuepuka matumizi ya
zebaki katika uchenjuaji na kuanza kutumia njia nyingine zilizopo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kwa kipindi
kirefu kumekuwepo na changamoto ya wachimbaji wadogo kufanya shughuli za
uchimbaji bila kuwa na taarifa sahihi za kijiolojia, hivyo
kusababisha wachimbaji wengi wadogo kuchimba kwa kubahatisha na hata
wengine kutumia imani za kimila katika kuchagua maeneo ya uchimbaji.
0 Comments:
Post a Comment