Friday, September 27, 2019

Rwanda ni taifa la namna gani?


Rwanda ni miongoni mwa mataifa madogo kabisa katika bara la Afrika. Lipo nyuzi chache kusini mwa mstari wa Ikweta. 

Rwanda imepakana na Uganda, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC). Pia taifa hilo ambalo sasa linaongozwa na Paul Kagame lipo katika ukanda wa maziwa makuu barani Afrika. 

Katika suala la hali ya hewa, mvua hunyesha mara mbili kwa mwaka na vipindi viwili vya kiangazi. Rwanda ina makabila matatu Wahutu, Watusi na Wa Twa; ambapo makabila haya yote yapo katika kabila moja kubwa la Banyarwanda. 

Wa Twa huwa wanachukuliwa kuwa ndio wenyeji wa taifa hiyo kutokana na aina ya maisha yao katika ardhi hiyo. Hata hivyo kuna wasomi wengine wanapingana na hilo kwa sababu mbalimbali. 

Pia Rwanda ni taifa ambalo limejichotea sifa kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha rushwa ikilinganishwa na mataifa mengine barani Afrika. 

Kagame ambaye ameshika wadhifa wa kuliongoza taifa hilo tangu mwaka 2000 kwa tiketi ya Chama cha Rwanda  Patriotic Front (RPF) amekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa katika hilo. 

Katika utawala wake taasisi za kimataifa za haki za binadamu zimekuwa zikimnyoshea kidole cha lawama kiongozi huyo kwa kukandamiza makundi yanayompinga na pia uhuru wa kujieleza umekuwa finyu katika taifa hilo. Rwanda ina majimbo matano yaliyoanzishwa mwaka 2006. 

Hata hivyo katika suala la kuwapa kipaumbele wanawake Kagame amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani ni miongoni mwa nchi mbili barani Afrika zenye idadi kubwa ya uwakilishi wa wananwake katika bunge la taifa hilo. 

Taifa hilo lilipata uhuru wake Julai Mosi, 1962 na katiba mpya liliipata mwaka 2003 baada ya kuifanyia marekebisho ile ya mwaka 1962. 

Kwa makadirio ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2015 Rwanda ina takribani watu milioni 11.2 kwa takimu hizo inashikilia nafasi ya 76 kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ulimwenguni. 

Mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ni habari isiyotoka katika historia ya taifa hilo. Mauaji ya Kimbari ya Rwanda yalikuwa mauaji ya halaiki nchini Rwanda ambapo wananchi wa kundi la Watutsi pamoja na Wahutu waliotazamwa kuwa wapinzani wa serikali au mauaji waliuliwa na wanamgambo, polisi na wanajeshi wa serikali iliyosimamiwa na viongozi Wahutu. 

Katika kipindi cha takriban siku 100, kuanzia kuuliwa kwa marais Juvenal Habyarimana wa Rwanda na Cyprien Ntaryamira wa Burundi Aprili 6 hadi katikati mwa mwezi Julai, takribani watu 800,000 hadi milioni 1 waliuawa, au karibu asilimia 20 ya idadi ya watu nchini Rwanda wakati huo.

Imetayarishwa na Jabir Johnson…….Septemba 27, 2019.

0 Comments:

Post a Comment