Septemba 23, 1940 alizaliwa
mwanasheria na mwanasiasa wa Brazili Michel Temer ambaye baadaye alikuja kuwa
Rais wa taifa hilo kubwa katika bara la Amerika ya Kusini.
Jina lake halisi ni
Michel Miguel Elias Temer Lulia. Alizaliwa katika kitongoji cha Tiete kilichopo
Sao Paulo nchini Brazil. Alikuwa Rais wa Brazil baada ya kuong’olewa madarakani
kwa mwanamama Dilma Rousef kwa kura ya wabunge ya kutokuwa na imani naye. Temer alikuwa wa nane na wa mwisho katika
familia yao ya wahamiaji kutoka Lebanon waliofika nchini humo mwaka 1925. Temer
alisomea masomo ya sharia katika Chuo Kikuu cha Sao Paulo na baadaye katika
Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Pontifical
cha Sao Paulo. Baadaye alitunukiwa shahada ya uzamivu ambayo ilimfanya
apande hadhi na kuwa Profesa wa Sheria hususani masuala ya Katiba. Mnamo mwaka
1964 alijiunga na Idara ya Elimu ya Jimbo la Sao Paulo na mwaka 1970 alikuwa
mwendesha mashtaka wa jimbo hilo. Mnamo mwaka 1983 aliteuliwa rasmi kuwa
mwanasheria mkuu na mwaka uliofuata Temer alikuwa Katibu Mkuu wa Masuala ya
Usalama wa Raia wa Sao Paulo. Alijunga na chama cha mrengo wa kati-kulia cha
PMDB (Partido do Movimento Democrático Brasileiro) na mnamo mwaka 1986 alikuwa
miongoni mwa wajumbe wa bunge la Katiba ambako walitengeneza upya katiba ya
taifa hilo mwaka 1987. Pia Temer aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Brazil katika
vipindi vitatu tofauti 1997–99, 1999–2001 na 2009–10. Mnamo mwaka 2001
alichaguliwa kuwa Rais wa Kamati ya Chama cha PMDB. Mwaka 2009 alitajwa kuwa
miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi nchini humo. Kabla hajachukua wadhifa wa
kuliongoza taifa hilo alikuwa makamu wa Rais
wa Dilma Rousseff ambaye alikuwa wa chama cha PT aliyeweka rekodi ya
kuwa Rais mwanamke kuliongoza taifa hilo. Hata hivyo Temer anakumbukwa kwa
tukio la kuoa mwanamke mrembo mwenye umri mdogo ukilinganisha na Temer akimpita
miaka takribani 43. Tukio hilo alilifanya mnamo mwaka 2003. Temer alikuwa Rais
wa 37 wa Brazil aliingia madarakani Agosti 31, 2016 hadi Desemba 31, 2018.
0 Comments:
Post a Comment