Tuesday, September 3, 2019

Uzinduzi wa Mradi wa Maji: MUWSA yatimiza ndoto ya Rais Magufuli



Maji ni kimiminika ambacho ni kiini cha uhai wowote duniani na pia kiini cha utamaduni wa binadamu.

Hakuna mtu anayeweza kuishi bila maji kwa sababu asilimia 50 hadi 65 za mwili wa mwanadamu ni maji.

Hata miili ya mimea na wanyama kwa kiasi kikubwa ni maji. Pia katika dunia maji yamechukua karibu robo tatu ya eneo lake lote (71.11%). Kwa hiyo maji ni kitu cha msingi sana.

Maji yana matumizi mengi nyumbani na katika uchumi: nyumbani maji hutumika katika kunywa, kuogea, kuoshea vitu na vyombo mbalimbali; kiuchumi maji yanatumika viwandani, kwa mfano kupoozea au kuoshea mashine, pia maji hutumika katika usafiri, kama vile meli za mizigo, za abiria na vinginevyo.

Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo inategemea maji katika kuendesha shughuli zake za kila kisu hasa ikizingatiwa ifikapo 2025 Tanzania itakuwa imefikia uchumi wa kati.

Tanzania ya Viwanda haiwezi kwenda bila kuwa na maji kwa wananchi wake. Usimamizi mbovu wa maji nchini umesababisha kupungua kwa maji na kuzuka kwa migogoro ambayo dhahiri inakwamisha vita dhidi ya umaskini na kuwa kikwazo dhidi ya uwekezaji.

Lakini usimamizi unapokuwa mzuri na juhudi mbalimbali kufanyika kuhakikisha maji yanapatikana hakika Tanzania ya Viwanda inakuwa ndoto ya kweli kama ambavyo Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyoaahidi wakati akiingia madarakani.

Hata hivyo viongozi na mamlaka mbalimbali zimekuwa zikitajihidi kuhakikisha ndoto ya Rais Magufuli inafikiwa, kama ambavyo Naibu Waziri Maji Jumaa Aweso alivyofanya kwa kutembelea mkoa wa Kilimanjaro na kuzindua Mradi wa Maji katika chanzo cha Kyaronga.

Naibu Waziri Aweso aliupongeza uongozi wote na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  mjini Moshi (MUWSA) kwa utendaji wao mzuri uliopelekea taasisi hiyo kukabidhiwa na Serikali majukumu ya kutekeleza miradi ya maji nje ya mipaka yake ya kazi ikiwemo nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Anasema Serikali imejiwekea lengo la kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2020 huduma ya Maji Safi na Salama  inawafikia asilimia 85 ya wananchi waishio maeneo ya  vijijini, na asilimia 95 ya wananchi wanaoishi mjini.

“Wananchi wa Mwika Kusini mnayo bahati kubwa ya kuwa kati ya maeneo ya vijijini yaliyopata huduma ya maji safi na salama hata kabla ya mwaka 2020 wakazi wa Mwika Kusini mmekuwa miongoni mwa watu wa kwanza hongereni sana,”anasema Naibu Waziri.

Anafafanua kwamba Serikali inampongeza sana Mkurugenzi wa MUWSA kwa kazi kubwa ambazo anazifanya,  ikiwa ni pamoja na Mamlaka hiyo kutumia rasilimali zake kutoa huduma za maji kwenye maeneo ya vijijini, hivyo Wizara inaiamini na itaendelea kuiwezesha MUWSA ili ifanikishe kuwapelekea wananchi wengi zaidi huduma za maji.

Anafafanua kuwa serikali ya Awamu ya tano imedhamiria kuongeza ufanisi katika kuwafikishia wananchi huduma ya maji kwa kufanya mabadiliko katika muundo wa Wizara ya maji. “Kwa sasa shughuli zote za usambazaji huduma ya maji nchini zinasimamiwa na Wizara ya Maji, hii imeondoa utaratibu wa awali ambao jukumu hilo lilikuwa linasimamiwa na halmashauri.

Owesso anasema kuwa tathimini ya EWURA inaonyesha MUWSA ni Mamlaka bora Tanzania  na taarifa zenu zinaonyesha mradi huu tuliouzindua ni mradi wa tisa  kuzinduliwa ndani ya miaka mitatu.

Niwapongeza kwa jinsi mnavyotumia Wataalamu wenu wa ndani katika kutekeleza miradi hii, ni jambo la kujivunia na kuigwa na Mamlaka nyingine  mfumo huu unawaongezea uwezo na unaokoa gharama za utekelezaji miradi.

Mkurugenzi mkuu wa MUWSA Joyce Msiru, anasema Mamlaka hiyo kwa sasa inatekeleza miradi yake nje ya mipaka yake ya kikazi kisheria ambayo ni Moshi Mjini.

“Kwa sasa tunatekeleza miradi mitatu Moshi Vijijini na mmoja wilaya ya Hai, pamoja na mwingine katika wilaya ya Same na hii ni kutokana na maombi ambayo tunayapata kutoka kwa Wananchi wa maeneo husika, tukiidhinishiwa na Serikali kupitia Mamlaka zake husika huwa tunatekeleza miradi hiyo”, anasema.

Anasema hatua hiyo imefikia Mamlaka hiyo kupewa dhamana ya kutekeleza miradi ya maji nje ya Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo anasema tayari MUWSA inatekeleza mradi wa maji huko Kakonko, mkoani Kigoma.

Kuhusu mradi wa maji wa Mwika Kusini, Msiru anasema umekamilika kwa asilimia 100, ambapo anasema awamu ya kwanza uligharimu shilingi milioni 430.6 na awamu ya pili gharama yake ni shilingi milioni 310.1.

“Mafanikio haya tumeyapata kutokana na ushirikiano mzuri tulioupata kutoa kwa Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maji, Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Serikali ya wilayani Moshi, pamoja na Wananchi walioko eneo la mradi huu, pamoja na kata za jirani”, afafanua.

Anasema Mamlaka ilipewa jukumu la kutoa huduma ya maji eneo la mji mdogo wa Himo yenye kata mbili ya Makuyuni na Njia Panda kwa GN namba 113 ya mwaka 2016. Hadi sasa Mamlaka inatoa huduma kwenye kata moja ya Makuyuni kwa asilimia 100, yenye wakazi wapatao 22,442.

Anasema mara baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo Mamlaka inakusidia kuanza kuweka mtandao wa usambazaji maji katika vijiji vitatu na kata ya Holili wilayani Rombo.

Akizungumzia utekelerzaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 220, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM) mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi, ameunga mkono juhudi zinazo fanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi MUWSA, na kuhimiza kuendelea kuunga mkono kwa kulinda mazingira na vyanzo vya maji.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba, anawataka wananchi kuwa walinzi katika vyanzo vya maji pamoja na miundombinu ya maji, uharibifu wa mradi huu utapelekea kuleta magomvi na uongozi wa serikali lakini pia utachochea ukosefu wa amani miongoni mwetu , tusimamie na kulinda miundombinu hii na mradi huu kwa ujumla.

Awali akisoma risala kwa niaba ya Wananchi wa kata ya Mwika Kusini, Mtendaji wa kata hiyo Amros Kimathi, anasema kuwa kukamilika kwa mradi huo utarajiwa kunufaisha vijiji vitano katika kata hiyo yenye wakazi 19,645.

Agosti 9, 2017 akiwa mkoani Kilimanjaro, kwenye uzinduzi wa tenki la maji katika eneo la Shabaha, kijiji cha Newland, Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Mkumbo, Anasema Wizara ya Maji inajukumu la kutafuta maji na kujenga miundombinu ya maji na hatimaye kuisambaza kwa wananchi.
Suala la utoaji wa huduma ya maji tunasimamia Wizara ya Maji , ikiwemo Usafi wa mazingira  kwa maana ya uondoaji wa maji taka mjini na vijijini.

Anasema upatikanaji wa maji safi na salama kwa Moshi ni asilimia 95 hadi 97,  Tanga wanapata kwa asilimia 90, Iringa asilimia 93 kwa maeneo ya mjini. Upatikanaji wa maji kwa nchi nzima ni asilimia 71 na kwa maeneo ya vijijini ni asilimia 53 wanapata maji.

Profesa Mkumbo anawasisitizia Wananchi na sekta mbalimbali wanaotumia maji kuwa waaminifu kwa kutekeleza wajibu wao wa kulipa bili za maji ili kuiwezesha Mamlaka zinazosimamia huduma za maji nchini kuendelea kutoa huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.

Katika kampeni za mwaka 2015 Rais Dkt. Magufuli aliwaahidi kwa wananchi katika maeneo mbalimbali alikotembelea kuwa tatizo la upatikanaji wa Maji Safi na Salama lililokuwepo kwa muda mrefu atalipatia ufumbuzi wa kudumu.

Rais Dkt Magufuli aliendelea kuweka msisitizo huo wakati pia akifungua Bunge la mwaka 2015 huku akiwaasa Watendaji atakaowateua katika serikali yake kuwa wahakikishe wanatatua kikamilifu na kwa wakati changamoto ya upatikanaji wa Maji Safi na Salama nchini.

Aidha Rais Dkt. Magufuli  alisema atakamilisha miradi iliyokwisha anza na kuanzisha miradi mipya mikubwa na midogo kutoka katika mito, maziwa na katika vyanzo vingine mbalimbali ambavyo vitakuwa na uhakika wa maji,  ikiwa ni pamoja na kuvuna maji ya mvua. Kwani “Tunataka Tuwatue akina Mama ndoo Kichwani,”.

FEATURED BY: Kija Elias, Moshi…..Agosti 27, 2019
EDITED BY:  Jabir Johnson


0 Comments:

Post a Comment