Friday, August 30, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Warren Buffett ni nani?


Agosti 30, 1930 Alizaliwa mwekezaji bilionea Warren Buffet, Omaha Nebraska nchini Marekani.

Katika kitabu cha “The Warren Buffet Way” kutoka kwa mwandishi Robert G. Hagstrom kinaelezea maisha ya bilionea Warren Buffett. Mwandishi anatumia kitabu hiki kushirikisha jamii mbinu ambazo mwekezaji bilionea Warren Buffet amekuwa akizitumia kukuza utajiri wake. Bilionea huyu ni mwekezaji ambaye amewahi kuwa tajiri namba moja wa dunia kwa kipindi kirefu na amekuwa kati ya matajiri watano wanaoongoza kwa muda sasa.

Warren Buffet amekuwa tajiri kupitia uwekezaji katika kampuni yake ya Berkshire Hathaway ambayo inajihusisha na uwekezaji kwenye biashara tofauti. Kwa ufupi Warren Buffet amekuwa ni mtu ambaye anachukua hatua mapema kama tahadhari dhidi ya nyakati zinazokuja na hivyo nyakati hizo (mbaya au nzuri) zinapowadia zinamkuta ameshajiandaa kiuwekezaji.

Alianza kupenda kilichomleta hapa duniani akiwa na umri wa miaka sita . Akiwa na umri wa miaka sita, alinunua paketi sita za Coca Cola kutoka dukani kwa babu yake na kwenda kuziuza ampapo alipata faida ya senti 5 kila paketi.

Akiwa na umri wa miaka 11 alikuwa tayari amenunua hisa, wakati huo watoto wenzie walikuwa wakiruka kamba, si jambo baya lakini hata yeye alikuwa akiruka, yaani kucheza, lakini alichokuwa akikiona siyo fedha, bali biashara. Suala la elimu kwake lilikuwa siyo la kipaumbele sana.

Mwaka 1947, akiwa na umri wa miaka 17, Buffet alimaliza kidato cha sita. Hakutaka kuendelea na masomo ya chuo, ingawa alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Tayari wakati huo alikuwa na fedha kiasi kama milioni 40, kiwango cha sasa cha Tanzania.

Hata hivyo Buffet alisoma na kumaliza elimu ya chuo kikuu. Sehemu kubwa baba yake ndiye aliyemshawishi hasa kusoma masuala ya biashara.

Akiwa na miaka 14 aliweza kununua shamba kutokana na kuweka akiba ya kugawa magazeti.

Wakati hajagundulika na kujulikana kuwa yeye ni tajiri, Warren Buffet hakujenga nyumba ya ghorofa ili watu wamjue yeye ni nani.

Alikuwa anaishi kwenye nyumba ndogo ya kawaida ya vyumba vitatu- Omaha. Ndani ya nyumba yake hiyo kuna kila kitu anachokihitaji yaani jiko, kitanda, meza, bafu, viti vya kukalia na television

Nyumba yake hiyo haikuwa na uzio. Huyu mzee hakuwa na dereva wala mlinzi. Alikuwa anaendesha mwenyewe na likiharibika, anaingia uvunguni mwenyewe kulitengeneza mwenyewe.

Warren Buffet haamini kuwa kuna bilionea duniani, bali anaamini kuwa kuna watu wanaotafuta ndoto zao ili zitimie.

Mfanyabiashara huyu wa Marekani anajulikana hasa kwa ajili ya falsafa yake ya ukarimu.

0 Comments:

Post a Comment