Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere umeongeza idadi ya abiria watakaokuwa wakihudumiwa
na Uwanja huo kutoka abiria milioni 2 mpaka abiria milioni 8 kwa mwaka.
Ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa Jengo la Tatu la
Abiria katika Uwanja huo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka.
Hayo yameelezwa Alhamisi
ya Agosti 1, 2019 Jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akitoa hotuba wakati wa uzinduzi
wa jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius
Nyerere.
"Mradi huu
umekamilika na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 720. Kukamilika kwa mradi
huu kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya fedha za Serikali na nidhamu
ya kutumia fedha hizo," amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema asilimia 100 ya fedha za
ujenzi wa jengo hilo ni fedha za Watanzania ambapo asilimia 15 imelipwa fedha
taslimu na asilimia 85 imekopwa na itarejeshwa kupitia kodi.
"Watanzania
tunaweza, tunachotakiwa ni kujiamini na kuamua kufanya. Bila kuamua Tanzania
tutaendelea kuwa wategemezi katika miradi ya maendeleo ya nchi yetu,"
amesema Rais Magufuli.
Aidha, ameitaja
miradi mingine inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutumia fedha za
ndani kuwa ni mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji wenye thamani ya shilingi
trilioni 6.5, daraja la Selander lenye thamani ya shilingi bilioni 270, ujenzi
wa viwanja vya ndege 15 nchini vyenye thamani ya shilingi ya trilioni 1.868,
ujenzi wa vituo vya afya 352, zahanati 30, hospitali 67 na ukarabati wa
hospitali za zamani 21 wenye gharama ya shilingi bilioni 321.6 pamoja na ujenzi wa barabara wa nchi nzima wenye jumla
ya kilomita 2105 yenye gharama ya shilingi trilioni 5.37
Miradi mingine ni
ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi katika ziwa Victoria, barabara ya njia ya
nane kutoka Kimara Dar es Salaam hadi Kibaha, ununuzi wa rada, utanuzi wa
bandari ya Dar es Salaam, ununuzi wa vifaa vya hospitali pamoja ukarabati wa
shule kongwe.
Kwa upande wake,
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema
Jengo la pili la abiria nalo linahitaji kukarabatiwa na kuongezwa uwezo wa
kubeba abiria mara mbili ya sasa, ambapo kwa sasa lina uwezo wa kuhudumia
abiria milioni 1.5 kwa mwaka.
Naye Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama
amesema taasisi yake imeshahamishia shughuli za uendeshaji wa ndege katika
Jengo hilo kutoka Jengo la abiria la pili.
Vile vile amesema,
jumla ya vijana 130 kati ya vijana 241 waliokuwa wanahitajika wameajiriwa,
ambapo kwa sasa wapo katika mafunzo ya nafasi walizopangiwa kufanya kazi.
Vile vile Mtendaji
Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patric Mfugale amesema ujenzi wa jengo la abiria la
kwanza ulijengwa mwaka 1956 ambapo unauwezo wa kuhudumia abiria laki 5 kwa
mwaka.
Mwaka 1984 ilikamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria ambalo
linauwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka.
STORY BY: Lilian Lundo, Habari Maelezo….Agosti 1, 2019
0 Comments:
Post a Comment