Edward Ngoyayi Lowassa ni
mwanasiasa nchini Tanzania. Alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa 10 wa Tanzania Desemba 30, 2005 na akajiuzulu Februari 7, 2008
kwa kashifa ya Richmond.
Mwaka 2015 alikuwa mgombea urais kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Alizaliwa Monduli mkoani Arusha Agosti 26,
1953. Alisoma shahada ya kwanza katika tamthilia kwenye Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, halafu shahada ya pili katika Sayansi ya Maendeleo ya Jamii Chuo Kikuu
cha Hull nchini Uingereza.
Lowassa ni mwanasiasa mkongwe mwenye uzoefu
mbalimbali katika siasa za nchini Tanzania, kwa kuwa aliwahi kushika vyeo mbalimbali
katika serikali kama vile Waziri mdogo wa Mazingira na Mapambano dhidi ya Umaskini
katika ofisi ya Makamu wa Rais (1988-2000), Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa
cha Mikutano (1989-1990) na Waziri Mdogo wa Haki na Mambo ya Bunge katika Ofisi
ya Makamu wa Rais (1990-1993). Alikuwa mbunge wa Monduli tangu mwaka 1990.
Mwaka
1995 Edward Lowassa aliamua kuingia katika mchakato wa kumpata mgombea urais
kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wakati huo Lowassa aliombwa na Umoja
wa Vijana kupitia kikao cha baraza kuu la Taifa achukue fomu akiwa miongoni mwa
wana CCM wanne ambao vijana waliamini wataweza kulisaidia Taifa kupiga hatua za
haraka kuelekea maendeleo endelevu, wengine waliokuwa wametajwa na Umoja wa vijana
ni Salim Ahmed Salim, Laurence Gama na Jaji mstaafu Mark Bomani. Katika hatua
ya kuchagua majina 3 kati ya majina 11 yaliyoomba nafasi hiyo, Lowassa akawa
hakupendekezwa. Vijana wa CCM walihoji kwa nini ameenguliwa, na yeye kwa utii
mkubwa kwa CCM aliwataka vijana na viongozi wengine waheshimu maamuzi ya chama
na kumuunga mkono atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya chama. Ikumbukwe kuwa
mwana-CCM mwingine aliyekuwa anakubalika kwa umma Augustino Lyatonga Mrema
aliondoka mapema CCM kwa sababu ndogo tu ya kubadilishiwa wizara na kuamua
kwenda chama cha NCCR Mageuzi ambako aligombea uraisi kwa chama hicho na kuleta
upinzani mkubwa. Yapo maneno ya baadhi ya wanasiasa kwamba kutoteuliwa kugombea
kwa Lowassa kulitokana na kuonekana anamiliki fedha nyingi akiwa na muda mfupi
kwenye utumishi wa umma, lakini pia inasemekana kuwa wale waliohoji kukatwa kwa
jina lake kwenye kikao cha Halmashauri kuu ya Taifa, majibu yalikuwa, CCM
iliamua kupeleka majina matatu kwenye mkutano mkuu ili wachague moja katika
uwakilishi huo wa majina: walipenda apatikane mtu mzima mmoja, mwenye umri wa
kati mmoja na kijana mmoja, watu hao ni mzee David Msuya ambae ni mtu mzima,
Benjamini Mkapa ambae umri wake ulikuwa wa kati na kijana ambae ni Jakaya
Kikwete. Lakini maneno hayo ya baadhi ya wanasiasa hayakuishia hapo: wakadai
baada ya Rais Mkapa kuchaguliwa, hakumteua Lowassa kwa kuwa aliagizwa na
Mwalimu Nyerere asimteue mpaka achunguzwe kama uwezo kiasi wa fedha alionao
unatokana na mapato halali, kama siyo halali asimteue. Mwaka 1997 Rais Mkapa
akamteua Lowassa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais mazingira.
Februari
7, 2008 Lowassa alijiuzulu baada ya kushtakiwa kuwa ameshiriki katika kashfa ya
Richmond. Kamati ya bunge iliwahi kuchungulia mkataba baina ya kampuni ya
TANESCO na kampuni ya Richmond Development Company LLC kutoka Houston, Texas.
Kamati ya wabunge watano chini ya mwenyekiti Dkt. Harrison Mwakyembe ikaona
mkataba huu ilikuwa kidanganyifu. Richmond ilipewa kazi ya kutengeneza megawati
100 za umeme kila siku baada ya ukame wa mwaka 2006 uliopunguza uwezo wa TANESCO
kutoa umeme nchini kutokana na mitambo yake ya umememaji. Lakini mitambo ya
dharura ya Richmond ilichelewa kufika nchini pia haikufanya kazi jinsi
ilivyotakiwa. Hata hivyo serikali ikaendelea kulipa zaidi ya dolar za Marekani
100,000 kila siku.
Mwaka 2014 Lowassa alisimamishwa na kamati kuu ya CCM baada
ya kushtakiwa ya kwamba aliwahi kuanzisha kampeni ya kuwa mgombea wa urais
kabla ya kipindi kilichokubaliwa na chama hiki.
Lowassa aliondoka katika CCM na
Julai 28, 2015 alijunga rasmi na chama cha upinzani cha CHADEMA. Lowassa alikaririwa
akisema,“Nitakuwa mnafiki nikisema bado nina imani na CCM.'' Pia mwanasiasa
huyo alisema, ''CCM niliyoiona Dodoma si CCM niliyokulia” na kuongeza “Kama Watanzania
hawapati maendeleo kupitia CCM basi wakayatafute nje ya CCM.”
Siku chache
baadaye aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CHADEMA mnamo Oktoba 2015.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) alishindwa kwa
kupata asilimia 39.97 za kura zote na mgombea wa CCM John Pombe Magufuli alipata
58.46 Lowassa aliendelea kuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema.
Mwaka 2016
alitangaza ya kwamba hawezi kurudi kamwe CCM. Mnamo Januari 2018 aliwahi kuwa
na mazungumzo marefu na Rais Magufuli. Machi 1, 2019 Lowassa alirudi kwenye
chama chake cha awali Chama Cha Mapinduzi.
0 Comments:
Post a Comment