Shamrashamra
zilizidi kurindima kwa fujo katika ukumbi maarufu sana wa Wikechi mjini
Makambako, hakika maharusi walikuwa wamependeza na utakuwa mchoyo wa kuzaliwa
usingewapongeza waliotumia ubunifu wa hali ya juu kuupamba ukumbi ule nao
ukapambika.
Kila
mmoja alitabasamu bila kujalisha linatoka moyoni ama ni la kuzugia!!
Wanawake
walipiga vigelegele na wanaume walipiga mbinja kila muda ambapo msema chochote
aliamuru!!
Naam!!
Ilikuwa sherehe ya aina yake ya kuwaunganisha Gladness na Jackson kuwa mwili
mmoja!!!
Jack
ambavyo wengi tulizoea kumwita alikuwa mwenye furaha sana alipopewa nafasai ya
kusema chochote, alizishukuru pande mbili akianza na ule upande wa ukweni
akawashukuru kwa zawadi ya mke mwema…..kisha akageukia upande wa pili na
kuwashukuru wazazi wake waliomkuza na kumpa elimu dunia pamoja na ile ya
darasani!!!
Hatimaye
msema chochote akamkabidhi kipaza sauti Glad!!
Ukumbi
mzima ulitambua kuwa Maria hakuwa akitabasamu kutoka moyoni lakini bado hakuna
aliyejua kwanini alikuwa katika hali ile.
Maria
akashika kipaza sauti mbele ya umati na kuanza kuzungumza.
“Imekuwa
safari ndefu sana hadi kuifikia siku hii ya leo…nikimtoa mwenyezi Mungu katika
safari hii ninaye mtu mwingine muhimu katika dunia hii wa kumshukuru!! Ni mtu
mmoja tu nasisitiza pasipokuwa na unafiki wowote!!
Namshukuru
mama yangu…mama yangu wa Kambo” akasita kidogo ukumbi nao ukawa kimya!! Kimya
kikuu…Glad akaendelea.
“Asante
sana mama wa kambo kwa matusi yote uliyonitukana maana ulinifanya niyazoee,
awali nilikuwa nakasirika sana ukunitukana, ukimtukana marehemu mama yangu,
ukinitukania baba yangu. Naam ukaniimarisha zaidi hata nilipokuwa nafanya kazi
za ndani sikuhangaishwa na matusi kutoka kwa watoto wa bosi wangu!!
Niliyapuuzia tu!!!
Asante
kwa kunilaza nje asante sana kwa jambo lile, nikalizoea giza, mbu wakaizoea
damu yangu!! Ukaniimarisha na hata nilipokosa pa kulala nikiwa mtaani stendi
ilikuwa sehemu sahihi kwangu na nililala bila hofu. Mama wa kambo siwezi
kusahau kukushukuru kwa kunilisha chakula ambacho watoto wako walilalamika kuwa
ni kibaya ama kimeharibika.
Ulikuwa sahihi mama maana hata kule majalalani
sikuhangaika tena kila kinachoitwa chakula mimi nilikula. Unadhani ungenidekeza
ningeweza vipi?
Siku
uliyoamua rasmi kunifukuza ukinizushia kuwa nakujazia choo na kukumalizia
godoro bila sababu za msingi ni hivyo hivyo niliwahi kufukuzwa na mabwana wengi
walaghai. Lakini sauti zao na yako zilifanana hivyo sikuogopa chochote kitu!!
Nikabaki kuwa imara huku nikihesabu kuwa haya ni mapito tu!!
Kulala
bila kula kwa siku mbili hadi tatu katika nyumba yako lilikuwa jambo la kawaida
sana hivyo niliweza kumvumilia Jack wangu alipokuwa hana pesa. Alinishangaa
sana kwa uvumilivu wangu lakini leo atambue kuwa bila wewe nisingeweza
kumvumilia.
Ulininyima
elimu mama wa kambo!! Vyema sana ukanifanya niishi kwa kutumia nguvu zangu tu
na akili ya ziada lakini si vyeti!! Sikuwa mtu wa kuchagua kazi, nilibeba
kokoto, nikafanya ubaamedi, nikafua nguo za watu, nikafagia barabara na kazi
zote zile ambazo zilihitaji watu kama mimi nisiyekuwa na elimu!! Asante mama wa
kambo!!!
Sijaisahau
ile siku uliyonimwagia maji ya moto na kuondoka na ngozi yangu usoni, tazama
ulinisaidia sana hakika, wanaume hawakunitamani!! Ndio…nani wa kumtamani na
kumthamini mwanamke asiyekuwa na mvuto.
Ulifanya
la maana sana mama maana maumivu niliyoyapata kuondokewa na wazazi wangu,
maumivu niliyoyapata kwa mateso yako, ni heri hayo yalitosha na ukaniepushia
maumivu ya kudanganywa na wanaume wakware kisa uzuri wangu kisha wanitelekeze
pasi na msaada. Ni heri waliidharau na kuichukia sura yangu hadi nilipokutana
na Jack. Hakujali sura akayajali maumivu yangu na akaamua kunipooza!!!
Hata
lile kovu uliloniachia kwa kunichoma na mkaa wa moto pajani, yeye hakujali pia.
Unadhani ni wanaume wangapi wanaweza kuwa na ujasiri wa Jack??
Nasema
nawe ewe mama uliyevaa nguo nyeupe pee!! Umeketi katika kiti cha tatu kutoka
kushoto, mama usiyekuwa na haya uliyenitukana huku ukisema kamwe kuwa
sitaolewa!!
Nimezisikia tetesi kuwa wale wanao wawili wa kike uliowabatiza cheo
cha umalikia walijazwa mimba na kuzaliwa nyumbani, sijui kama ni kweli kuwa
yule mwanao wa kiume alinibaka ukanitusi mimi kuwa namfunza tabia mbaya nasikia
na yeye ni teja na kila leo anakuibia vitu nyumbani!!
Natoa
shukrani kwako kwa mabaya yote uliyonitendea, natoa shukrani kwako kwa moyo
wako mgumu unaodhani kuwa niliyasahau yale yote na leo hii umeketi upande wa
ukoo wangu ukisubiri kunipa zawadi ya kunipongeza kwa sababu nimeolewa.
U
mnafiki ewe mama, u mkatili katika maana halisi ya kuitwa mkatili.
Nayasema
haya ili niwe na amani, nayasema haya bila unafiki wala tabasamu bandia la
kuigiza!!! Nilijua itafika siku ya kusema nd’o maana sikusema katika siku hizi
zote.
Ewe
mama wa kambo umenipa zawadi nyingi sana tena za kudunu, siihitaji zawadi yako
siku hii ya leo. Sihitaji chochote kitu katika maisha yangu kutoka kwako!!
Umenipa vingi na vinatosha sana!!!
Asante
sana mama wa kambo!! Mama mbaya unayesababisha hata wale mama wa kambo wenye
utu waonekane kuwa si lolote na si chochote kitu!!!”
Glad
alimaliza kuzungumza huku machozi yakiondoka na nuru yake asiweze kuona mbele
tena.
Mama
yule ambaye ukumbi mzima ulikuwa ukimtazama alibaki akiwa ameinama. Watu
walingoja sana anyanyuke waweze kuibaini walau sura yake. Lakini hakunyanyuka,
aliyeamua kumgusa bega mara kadhaa kwa kumsukuma ndo aliihitimisha safari yake
sakafuni. Mama yule hakuwa na fahamu zake!!!
Zikafuata
hekaheka za kumpepea lakini fahamu hazikurejea.
Glad
naye alifanya harakati hizo huku akiipuzia shela aliyokuwa ametinga. Hali
ilikuwa tete na ukumbi wa sherehe ukageuka kuwa ukumbi wa hekaheka!!
Wakati
mama yule anakimbizwa hospitali, Maria alipata fursa ya kukwapua bahasha ambayo
awali ilikuwa mikononi mwa mama wa kambo kabla hajaanguka!!
Akaifungua
na kukutana na kipande cha karatasi.
“Sina
zawadi yoyote ya kukupa Glad, japo ni wewe wa kunipa mimi zawadi kubwa ya
msamaha. Hakuna nikitegemeacho tena duniani zaidi ya msamaha wako!! Siwezi
kujieleza nikaeleweka kwa yote yaliyotokea miaka hiyo lakini waweza kunielewa!
Ninauhitaji msamaha wako kabla sijafa Glad.
CREDITED: Simulizi
hii fupi ya ‘Asante Mama wa Kambo’ ilitungwa na George Iron Mosenya, mwaka 2013.
JAIZMELA imeihariri kidogo kutoka kwa mtunzi ili kuleta maana iliyokusudiwa.
0 Comments:
Post a Comment