Monday, August 19, 2019

Wananchi wamlilia DC Senyamule mikutano ya serikali ya Kijiji



Wananchi wa kijiji cha Mhero Kata ya Chome, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia kitendo cha kutoitishwa mikutano ya kijiji mara kwa mara pamoja na kusomewa taarifa za mapato na matumizi ni moja ya sababu kubwa inayokwamisha shughuli za maendeleo katika kijiji hicho.

Wakizungumza katika mkutano wa kijiji ambao uliitishwa na Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule kwa malengo ya kutatua kero za wananchi,  pamoja na kujadili changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za maendeleo, wananchi hao wamewatupia lawama  wenyeviti wa vijiji kwa kutoitisha mikutano ya serikali ya kijiji chao.

Kufuatia kuwepo kwa tuhuma hizo, Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka Wenyeviti wa Vijiji wilayani humo, kuhakikisha kwamba wanasoma taarifa ya mapato na matumizi kwa wananchi kabla ya Agosti 30 mwaka huu.

DC Senyamule alilazimika kutoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Mhero Kata ya Chome  ikiwa ni  ziara yake ya kutatua kero za wananchi ambapo baadhi ya wananchi walionyeshwa kukerwa na viongozi wa vijiji kwa kushindwa kutoa taarifa za mapato na matuzi kwa muda mrefu.

“Naomba kutoa maagizo ya serikali hapa, ifikapo Agosti 30 mwaka huu, nataka wenyeviti wa vijiji muwe mmeshasoma taarifa za mapatio na matumizi na tarifa hizo ziweke kwenye matangazo ili kila mwananchi aweze kuisoma taarifa hiyo,” alisema DC Senyamule.

Alisema Mwenyekiti yeyote wa serikali ya kijiji asiondoke madarakani kabla hajasoma taarifa za mapato na matumizi, ikiwemo michango ya wananchi walivyoshirika katika kuchangia shughuli za maendeleo katika eneo husika.

Aidha DC Senyamule alimwagiza Mkaguzi wa ndani ahakikishe ndani anafanya ukaguzi na kumpelekea taarifa hizo baada ya wiki mbili ofisini kwake.

Pia Mkuu huyo wa wilaya alitoa maelekezo kwa mganga mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha Kituo cha afya cha Shengena kinaanza kutoa huduma ifikapo Septemba mosi mwaka huu, hususani katika upande wa  wodi ya mama na mtoto.


0 Comments:

Post a Comment