Thursday, August 22, 2019

Afisa Utumishi adakwa na TAKUKURU akipokea rushwa ya laki moja

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Kilimanjaro, inamshikilia Afisa Utumishi Mwandamizi wa halmashauri ya Wilaya ya Moshi Julius Kimaro kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya shilingi 100,000.

Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro Holle Makungu alisema mtumishi huyo alitenda kitendo hicho kwa mfanyabiashara wa vinyago.

Makungu alisema alikamatwa na maafisa wa Takukuru Agosti 20 mwaka huu katika maeneo ya baa iitwayo Forest, Manispaa ya Moshi

“Afisa Utumishi huyo alipewa majukumu ya kusimamia makusanyo ya maduhuli katika halmashauri ya Moshi, alipokea rushwa ya shilingi laki moja kutoka kwa mfanyabishara wa vinyago ambaye baadaye alituletea taarifaza kuombwa rushwa,” alisema Makungu.

Awali ilielezwa kuwa Kimaro alimkadiria mfanyabiasharo huyo wa vinyago kuwa anatakiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni nne kwa mwezi.

Hata hivyo Afisa huyo, alimuahidi kuwa angempunguzia mfanyabishara huyo hadi kufikia kiasi cha shilingi milioni moja na laki mbili (TZS 1,200,000) endapo angempa kiasi cha shilingi laki moja.

“Baada ya mazungumzo na makubaliano ya wawili hao ndipo mfanyabiashara huyo alikuja na kutupatia taarifa iliyofanya tumkamate afisa huyo,” aliongeza Makungu.

Makungu alisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtumishi huyo baada ya uchnguzi kukamilika huku wananchi wakitakiwa kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi inapotokea kuna vitendo hivyo bila kujali wadhifa wa mtu au hadhi yake kwa jamii.


0 Comments:

Post a Comment