Monday, August 19, 2019

Dkt. Mghwira atoa mifuko 100 ya saruji Same

Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule akikabidhi mifuko ya saruji kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kiimanjaro Dkt. Anna Mghwira.


Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira, ametoa msaada wa mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Mtii na ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Magulunde iliyopo wilaya ya Same mkoani hapa.

Dkt. Mghwira alisema, ameamua kutoa msaada huo wa saruji, ili kuwaunga mkono wananchi wa kata hiyo, waliojitolea kuanza ujenzi wa madarasa  katika shule hiyo pamoja na kituo cha afya ili waweze kukamilisha ujenzi huo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, kwa niaba ya Mkuu wa mkoa, Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule, amewapongeza wananchi kwa kata hiyo kwa hatua waliyoifikia ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya na ujenzi wa madarasa.

Dc Senyamule pia alitoa rai kwa kamati ya ujenzi kuhakikisha kwamba  saruji iliyotolewa  wanaitumia kwa lengo yaliyokusudiwa na endapo atabainika mtu yeyote kujihusisha na uchakachuaji wa saruji hiyo hata sita kumchukulia hatua kali za kisheria.

“Msaada huu wa mifuko 100 ya saruji ambayo nimewakabidhi hivi punde kwenu leo  ni kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kituo cha afya Mtii na ujenzi wa madarasa katika sule ya msingi Magulunde, nawaomba saruji hii itumike kwa kujenga kituo cha afya na madarasa, sitaki kusikia imebadilishiwa matumizi wala kusikia kwamba imeibiwa,”alisema DC Senyamule.

Dc Senyamule  alisema hakuna taifa lolote duniani ambalo linaweza kuendelea bila kuwekeza katika sekta ya elimu, hivyo ninatoa wito kwa wazazi na walezi kuwekeza kwa watoto wao kwa kuwapatia elimu ambayo itakuwa msingi wa maisha yao ya baadae.

Aliongeza kusema kuwa “Napenda kuona watoto wanasoma katika mazingira mazuri ili watimize ndoto zao  hatimaye baadae wawe viongozi wazuri wa taifa hili, walimu wakikaa katika ofisi zilizo bora hata moyo wa kufundisha wanakuwa nao,”alisema Dc Senyamule.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Same Isaya Mngulu, ameipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mwenyekiti wa (CCM)  taifa Dkt John Magufuli,  kwa kazi kubwa ya kuwapelekea wananchi maendeleo katika kila nyanja.

Nao baadhi ya wakazi wa kata hiyo wamemshukuru Mkuu wa mkoa Dkt. Mghwira kwa  kuwaletea saruji hiyo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa yao pamoja na kituo cha afya,  jambo ambalo walikuwa wanalilia kupata huduma hizo kwa karibu zaidi ili kuwapunguzia adha wanayoipata wananchi ya kutafuta huduma umbali mrefu.

“Tunampongeza  Mkuu wa mkoa Mama Mghwira, kwa kuweza kutusaidia mifuko hii ya saruji, tunawaomba na wadau wengine waone umuhimu wa kuweza kutusaidia kwani jengo hili la kituo cha afya hadi kukamilika kwake linahitaji zaidi ya Sh. 35/= milioni,”alisema  msoma risala.

STORY BY: Kija Elias….Agosti 2019

0 Comments:

Post a Comment