Kikongwe mwenye umri
wa miaka 73 na binti yake mwenye umri wa miaka 47 wamekutwa wamekufa huku miili
yao ikiwa kwenye vyumba tofauti.
Maofisa wa Polisi wa Nairobi wamesema tukio
hilo la kikatili limetokea katika South B Estate jijini Nairobi.
Kikongwe
ametambuliwa kwa jina la Judy Wanjiku Mwai na binti yake Catherine Nyaguthi
Mwai na kwamba mauaji hayo yalitokea siku ya Jumapili katika nyumba waliyokuwa
wakiishi peke yao iliyopo katika viunga vya Golden Gate.
Miili ya marehemu hao
imegunduliwa jana jioni baada ya ndugu yao mmoja kwenda katika nyumba hiyo
akiwa na madhumuni ya kuwasalimia. Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kwa mara ya
mwisho marehemu hao waliwaona siku ya Jumapili mchana wakati wanashushwa na
gari jeusi.
Marehemu wote walikuwa waajiriwa wastaafu ambapo kikongwe alikuwa
mhasibu na bintiye alikuwa mfanyakazi wa benki. Imeelezwa kuwa wakati ndugu yao
alipofika katika nyumba hiyo alibisha hodi bila kuitikiwa hivyo ilimbidi aingie
ndani ambako alikutana na miili ya ndugu zake ikiwa katika vyumba viwili tofauti
na ndipo aliporipoti polisi.
Maofisa wa Polisi wamesema mwili kikongwe huyo
ulikutwa na kamba ya katani shingoni na kwamba mwili ulilazwa kwenye kitanda
ukiwa na kamba shingoni ambayo ilikuwa imefungwa kwenye tendegu la kitanda. Pia
imeelezwa damu zilikuwa zikitoka mdomoni.
Mwili wa Nyaguthi ulikuwa katika
sakafu ya chumba chake ukiwa na majeraha katika shingo hali iliyoonyesha
kulikuwa na purukushani.
Majirani wamesema hawakuwapo katika eneo hilo wakati
wa tukio. Hata hivyo Polisi imesema upelelezi wa awali unaonyesha katika tukio
hilo watu zaidi ya wawili wamehusika katika ukatili huo.
Hakuna kitu chochote
ambacho kimeibiwa katika nyumba hiyo kwani simu za marehemu walikutwa nazo.
Mkuu wa Polisi wa Nairobi Phillip Ndolo amesema hadi sasa hakuna mtu
aliyekamatwa kutokana na mauaji hayo na kwamba kwa sasa bado upelelezi
ukiendelea kujua chanzo cha mauaji hayo.
CHANZO: STANDARD
0 Comments:
Post a Comment