Monday, September 30, 2019

Njaa iliyojificha inavyoitesa Jamii

Kuanza kumpa mtoto chakula kabla ya kufikisha miezi sita ni hatari kiafya


Wataalamu wa masuala ya lishe wanaeleza njaa iliojificha kuwa ni kula chakula na kushiba huku mwili ukiwa haujavuna vya kutosha madini, protini na hata vitamin, hali inayopelekea mwili kuzongwa na maradhi mbalimbali.

Mataifa yanayoendelea yamekuwa yakikabiliwa kwa kiasi kikubwa na matatizo ya lishe kutokana na wananchi wengi kutokuwa na elimu ya kutosha na sahihi juu ya lishe bora katika familia zao, hali inayoathiri kasi ya juhudi za kupambana na njaa iliojificha.

Tanzania  ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na tatizo hilo kwa watu wake hasa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wanawake walio katika rika la kuzaa.

Utafiti wa wa afya na viashiria vya malaria wa mwaka 2015/16 unaonesha kuwa upungufu wa damu kwa watoto walio na umri wa miezi 6 hadi 59 ni asilimia 58 huku asilimia 2 wakiwa na upungufu wa juu wa damu, asilimia 30 wakiwa na upungufu wa kati na asilimia 26 wakikabiliwa na upungufu wa damu wa kawaida.

Utafiti huo unaonyesha kuwa mkoa wa Shinyanga ndiyo umeathirika zaidi ambapo wastani wa asilimia 71 ya watoto wana tatizo la upungufu wa damu.

Taasisi ya Chakula na Lishe nchini Tanzania (TFNC) anasema mapambano dhidi ya udumavu laazima yaanze katika siku 1000 za kwanza za binadamu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema utapiamlo ambao matokeo yake ni udumavu hutokana na kutokuwa na usawa katika kiwango cha chakula kinachompa mtu virutubisho mwilini.

Hali hii hutokea kwenye makundi mawili; kwanza kutokuwa na lishe ya kutosha ambako kunajumuisha kudumaa, kuwa  na uzito mdogo usioendana na umri pamoja na kukosa virutubisho vya kutosha.

Pili ni kula vyakula vinavyoleta  unene uliopitiliza na magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha. Na hali hii huwapata zaidi watoto na watu wenye kipato kizuri waishio mjini.

Katika familia nyingi linalotazamwa ni kula na kila mwanafamilia ashibe kwa kiwango chake pamoja na urahisi wa upatikanaji wa chakula katika jamii husika, ndani ya familia nyingi wanawake walio katika umri wa kuzaa na watoto walio chini ya miaka mitano ndio wanaathirika zaidi na tatizo hili linalotajwa na wataalamu njaa ilio jificha.

Bado utafiti huo unaonyesha kuwa miongoni mwa wanawake walio katika rika la kuzaa la umri wa kuanzia miaka 15-49 asilimia 45 wana tatizo la upungufu wa damu ambapo asilimia 1 wana upungufu wa damu wa juu, asilimia 11 wana upungufu wa damu wa kati na asilimia 33 wakiwa na upungufu wa damu kawaida.

Kwa nchini Tanzania  utafiti uliofanywa na taasisi ya lishe (TFNC) kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya takwimu (NBS) kuhusu afya na viashiria vya malaria wa mwaka 2015-2016  unaonesha kuwa tatizo la udumavu linakabili zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa na watoto chini ya miaka mitano.

Utafiti huo unaonesha kuwa mkoa wa Rukwa unaongoza kuwa na watoto wengi wenye udumavu kwa kiwango cha asilimia 56 ukifuatiwa na mkoa wa Njombe kwa asilimia 49, Ruvuma asilimia 41, Iringa asilimia 42 na Kagera 42.

Kiuhalisia mikoa hii kwa nchini humo ndio inayoongoza kwa uzalisaji wa chakula hata hivyo ndio inayoonoza kuwa na kiwango cha juu kuwa na hali ya udumavu.

Matokeo ya utafiti huo yanadhihirisha bado kuna kazi kubwa ya kupambana na  changamoto ya lishe duni inayosababisha  udumavu, uzito pungufu, upungufu wa damu na ukondefu.

Katika gazeti la mtandao la wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia, wazee na watoto naibu waziri Dkt. Faustine Ndugulile alisema, "Zaidi ya asilimia 35 ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano nchini vinachangiwa na matatizo ya lishe duni na katika kipindi cha mwaka 1992 hadi 2015/16 vimepungua kutoka 149 hadi 67 kwa kila vizazi hai 1000.

Shabaha ya shirika la afya duniani WHO ifikapo mwaka 2025 ni kwa kupunuguza kwa idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano waliodumaa kwa nchini Tanzania kwa asilimia 40. Hivyo ni muhimu kwa jamii ya Watanzania kuzingatia lishe bora kwa watoto, wajawazito na  wanawake walio katika rika la kuzaa.

CHANZO: DW

0 Comments:

Post a Comment