Thursday, February 8, 2024

Kuteketea Soko la Mbuyuni kutoa fursa taasisi binafsi kudhibiti majanga ya moto?

 


MOSHI, KILIMANJARO


SOKO la Mbuyuni lililopo Manispaa ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa masoko maarufu makubwa nchini ambayo yameingia katika orodha ya kuteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa kwa Wafanyabiashara, ndugu jamaa na marafiki kuathirika kisaikolojia na wengine kupoteza maisha kutokana na mshtuko

 

Masoko mengine ni kama vile Soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya, Soko la Mandela lililopo Sumbawanga mkoani Rukwa, Soko Kuu la Mpanda mkoani Katavi na Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam yamewahi kukutana na changamoto ya majanga ya moto

 

Usiku wa Februari 5 mwaka huu, moto uliteketeza Soko Kuu la Mbuyuni, lililokuwa na vibanda vya Wafanyabiashara 2,500 janga ambalo linadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme

 

Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba hakuna madhara kwa watu yaliyotokana na maafa hayo, japokuwa mali na pengine fedha, vitu vilivyotafutwa kwa jasho jingi na muda mrefu vilitokea dakika chache

 

Pamoja na msemo wa waswahili unaosema kwamba ajali haina kinga, tunaamini kwamba majanga ya aina hii ambayo aghalabu husababisha uharibifu mkubwa wa mali au hata kugharimu maisha ya watu yanaweza kuzuilika kwa kiwango kikubwa ikiwa tu hatua za tahadhari zitachukuliwa

 

Wakizungumza na Tanzania Leo kwa nyakati tofauti wakazi wa Manispaa ya Moshi wamesema kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu imewafungua na kuitaka serikali kuruhusu taasisi nyingine kudhibiti majanga ya moto.

 

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo akiwa na Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini katika eneo la Soko la Mbuyuni lililoteketea kwa moto mnamo usiku wa manane wa Februari 6, 2024.

Mkazi wa Kata ya Miembeni Manispaa ya Moshi Isack Kireti, ameishauri serikali kuzipa fursa taasisi nyingine imara zinazoweza kupambana na majanga ya moto yanapotokea nchini  badala ya kutegemea Jeshi la Zimamoto pekee kufanya shughuli hiyo kutokana na idadi ya watu kuongezeka kila mwaka huku vifaa vya Jeshi hilo vikishindwa kwenda na kasi ya mabadiliko

 

“Baada ya zimamoto kurudishwa Wizara ya Mambo ya Ndani ndio mambo yalipoharibika, ni vema ikarudishwa iweze kujitegemea kabisa au kuleta washindani nje ya mfumo ikiwamo kuziruhusu taasisi nyingine kusaidia kudhibiti majanga ya moto,” alisema Kireti.

 

Mkazi wa Kata ya Majengo Gadson Mdee, alisema elimu duni, uelewa ndogo juu ya namna ya kujikinga na majanga ya moto ambayo anaamini kwaba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likijipanga na kuweka mkakati balaa hilo linaweza kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

 

“Wananchi wanahitaji kuelimishwa kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya umeme kwenye nyumba na maeneo ya biashara majanga mengine yamekuwa yakisababishwa na ujivu wa masuala ya umeme na kufikia hata kuhamisha nyaya  bila ya kuzingatia wachache na vifaa stahiki.”alisema Mdee.

 

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO NURDIN BABU ANENA;

 

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akizungumza jambo kuhusu kuteketea kwa Soko la Mbuyuni ofisi kwake.

Serikali mkoani Kilimanjaro inafanya tathmini ya kujua chanzo cha moto ulioteketeza Soko Kuu la Mbuyuni usiku wa Februari 5 mwaka huu.

 

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliyabainisha hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuati tukio la hilo, lililoteketeza bidhaa za Wafanyabiashara zaidi ya 2,000.

 

Babu alisema jambo lolote linapotokea halipangwi na kwamba gari la zima moto kutokufika kwa wakati katika eneo la tukio ni kutokana na hitilafu kwa takribani mwezi mmoja sasa.

 

“Kwanza nichukue fursa hii kuwapa pole sana wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo, moto huu ulianza kuwaka muda wa saa sita na nusu usiku wa Februari 5, 2024, mimi na Kamati yangu ya ulinzi na usalama ya mkoa;

 

Tulifika eneo la tukio muda wa saa saba usiku tulishirikiana na viongozi wengine waliokuwepo akiwemo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwajuma Nasombe na Mkuu wa Wilaya Kisare Makori, tulikuwa tuna hakikisha moto ule hauvuki kwenda kwenye makazi ya watu, jambo ambalo tulifanikiwa hadi ile asubuhi moto ukawa umezimika.”alisema RC Babu.

 

Awali mwenyekiti wa soko hilo Lameck Mziray, alisema soko hilo lina wafanyabiashara wasiopungua 2,500 na kwamba soko hilo limeungua lote na kuteketeza mali zote zilizokuwepo.

 

“Soko linawafanyabiashara wasiopungua 2500, mpaka sasa hivi, soko hili limeunmgua lote hakuna palilpo salia,” alisema.

 

MANISPAA KUANZA KULIJENGA UPYA SOKO LA MBUYUNI;

 

Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini Faraji Swai akizungumza na waathirika wa Janga la Moto soko la Mbuyuni mnamo Februari 7, 2024.

Ujenzi wa Soko Kuu la Mbuyuni mjini Moshi unatarajiwa kuanza Februari 9,2024 baada ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kuruhusu miradi ya Kata nyingine isiendelee kwa ajili ya dharura.

 

Akizungumza katika mkutano wake na Wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni kuwaeleza waliyoafikiana na Baraza la Madiwani kuhusu mustakabali wao baada ya soko kuteketea Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo, alisema Madiwani kwa pamoja wamekubali kuzuia fedha za miradi ambayo ilikuwa inakwenda kutekelezwa kwenye kata zao na fedha hizo ziweze kutumika kujenga soko hilo.

 

Alisema soko la Mbuyuni litarejea kama ambavyo lilikuwa awali, kwa sasa tuko katika hatua za kumtafuta mkandarasi ili aweze kuanza haraka ujenzi wa soko hili.

 

Mstahiki Meya Kidumo, alisema wako Wafanyabiashara  wengi katika soko hilo walikuwa  wamekopa fedha kwenye taasisi  za kifedha, aliwaomba wenye mabenki kutowasumbua kuhusu marejesho ya fedha hadi hapo soko hilo litakapokamilika, ndipo waendelee na urejeshaji wa mikopo hiyo.

 

“Ndugu zangu wafanyabiashara nafahamu wengi wenu mnamikopo kwenye mabenki, nataka niwahakikishie su=ala hili mkuu wetu wa Mkoa wa Kilimanjaro analifahamu, anafanya utaratibu wa kuongea na viongozi wa benki mlizokopo fedha ili waweze kuwa na subra kidogo kuhusu urejeshaji wa fedha hizo, pindi soko hili litakapokamilika na nyie mkaanza kufanya biashara hata mtaanza kuzirejesha fedha hizo lakini kwa sasa tumewaomba wawe na uvumilivu kidogo.”alisema Mhandisi Kidumo.

 

Katika hatua nyingine Mstahiki Meya Kidumo, alimtaka Meneja wa soko hilo, mfanyabiashara aliyekuwa anafanyabiashara eneo hilo, pindi soko hilo litakapokamilika aweze kupata sehemu yake ya kufanyia biashara na asiwepo mtu wa kuachwa.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mwajuma Nasombe alisema mkandarasi ataanza kazi hiyo Februari 9, 2024 na ili kuepuka usumbufu, eneo lote la soko litazungushiwa uzio wa mabati.

 

“Wakati ujenzi huu ukiendelea hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kufanya biashara  yake kwenye uzio wa eneo hilo, nawaomba sana wafanyabiashara mtu ushirikiano na tunataka zoezi hili liende mapama zaidi ili muweze kuendelea na biashara zenu,”alisema Nasombe.

 

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Moshi Mjini Faraji Swai, aliwapa pole wafanyabishara hao, ambao wamefikwa  na janga hilo la kuunguliwa na mali zao.


Aidha aliwaondoa wasiwasi  Wafanyabiashara hao kuwa hakuna mtu yeyote atakayeondolewa ambae alikuwa akifanya biashara yake katika eneo hilo.

#KijaElias_Moshi

0 Comments:

Post a Comment