Baadhi ya wafanyabiashara mkoa wa Kilimanjaro, wamelalamikiwa na wananchi, kwa kuwalazimisha watu kununua mche wa sabuni, kibiriti au sabuni kama bidhaa ya ziada ndipo wauziwe sukari.
Mkazi wa Kata ya Majengo Manispaa ya Moshi Dorice Chuwa, ambaye anajishughulisha na biashara za kutembeza viatu, alisema kwa sasa ukienda dukani kununu sukari mfanyabiashara anakulazimisha ununue mche wa sabuni, dawa ya mswaki au kiberiti kama bidhaa ya ziada ndipo akuuzie sukari na ukikataa kununua bidhaa hizo huwezi kukuuzia sukari.
“Baadhi ya wafanyabiashara wa Manispaa ya Moshi, wanawalazimisha watu kununua mche wa sabuni, kibiriti au sabuni kama bidhaa ya ziada ndipo wakuuzie sukari, ukikataa kununua bidhaa hizo huwezi kuuziwa sukari, ” alisema Dorice.
Alisema “Changamoto hii imenikuta mimi juzi baada ya kutoka kwenye mihangaiko yangu jioni wakati nawaandalia watoto wangu chai kwa ajili ya kunywa kesho asubuhi waennde shuleni, ndani kwangu sukari ilikuwa imeisha nilimtuma mtoto kwenda dukani kununua sukari kilo moja, nilimpa Sh 4,000, lakini alirudi bila sukari.”alisema.
Alisema baada ya kumuuliza mtoto kwa nini hujanunua sukari alinijibu kuwa pale dukani wanataka kwanza ununue sabuni, kiberti au dawa ya mswaki ndipo wakuuzie sukari.
Akizungumza kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliwaagiza wafanyabiashara kuweka bayana bei ya sukari madukani mwao ili kukabiliana na changamoto ya kupandishwa kwa bei ya bidhaa hiyo.
“Yako malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na bei ya sukari kupandishwa kiholela kila siku, hali hii imekuwa kero kubwa kwa wananchi pamoja na juhudi zote zinazofanywa na serikali katika kukabiliana nayo”, alisema.
“Kuanzia sasa, wafanyabiashara wote wa jumla na rejareja watatakiwa kuweka tangazo kubwa lenye kuonyesha bei elekezi ya sukari kama ilivyoainishwa na serikali”.
Babu aliendelea kusema kuwa kutokana na mapenzi yake kwa wananchi, serikali yake imeagiza sukari ya ziada kutoka nje ili kufidia pengo la sukari lililoko hapa nchini.
“Ili kutoa unafuu kwa wananchi, serikali imeondoa kodi ya uagizaji sukari na ile ya ongezeko la thamani (VAT) ili iuzwe kwa bei ya nafuu kwa wananchi, hivyo serikali mkoani hapa haitawavumilia wafanyabiashara ambao watataka kutumia sukari hiyo kujinufaisha huku wakiwaumiza wananchi”, alisema na kuongeza, kwa kuweka bango lenye bei elekezi kutamuwezesha mnunuzi kuuziwa sukari kwa bei kama ilivyoainishwa kwenye bango hilo.
Aliongeza, “Serikali mkoani Kilimanjaro imejipanga kuhakikisha wananchi walioanza kufunga Kwaresma kwa Wakristo na Ramadhan kwa Waislamu sukari haitakuwa kikwazo kwao wakati wakitekeleza nguzo hizo muhimu za Kiimani”.
Pia mkuu huyo wa mkoa alitoa wito kwa uongozi wa kiwanda cha sukari cha TPC kuwasilisha orodha ya wafanyabashara wa jumla watakaopewa jukumu la kuuza sukari kwa uongozi wa Mkoa ili waweze kufuatiliwa lengo likiwa ni kuhakikisha wanauza bidhaa hiyo kwa mujibu wa bei elekezi.
Awali akitoa taarifa ya hali ya sukari ya kiwanda cha uzalishaji sukari ya TPC kilichoko Moshi, mkoani humo Jaffari Ally alisema kuwa kiwanda hicho kinaendelea na uzalishaji hadi mwezi Machi mwaka huu wakati wa mvua za masika zinapotarajiwa kunyesha.
“Kwa upande mwingine sukari iliyoagizwa na serikali kufidia pengo la sukari hapa nchini imeanza kuwasili hivyo hakuna sababu ya uwepo wa uhaba wa sukari”, alisema Ally.
Alisema serikali imeondoa asilimia 25 ya kodi ya kuingiza sukari nchini (Income Tax) na asilimia 18 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ili kumpa nafuu mlaji, ambapo alisema si vyema wafanyabiashara wakatumia mwanya huo kujinufaisha.
“Kufuatia uamuzi huo wa serikali, bei ya sukari inatakiwa kuwa kati ya Sh 2,650 na Sh 2,800/- kwa kilo kwa bei ya jumla na Sh 2,800/- na Sh 3,000/- kwa kilo kwa bei ya rejareja na hii ni kwa mujibu wa muongozo wa serikali kuhusu bei hizi uliotolewa Januari 23, 2024”, alisema Ally.
0 Comments:
Post a Comment