Tuesday, February 27, 2024

Vijana watakiwa kuchangamkia ujuzi VETA

Zoezi la hiari la uchangiaji damu limefanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mjini Moshi Kilimanjaro Februari 27, 2024 ambapo wanachuo zaidi ya 300 walijitolea damu zao. (Picha Na: JAIZMELA)


Vijana wametakiwa kuwa imara kiuchumi kwa kuwa na ujuzi ili kujikwamua na changamoto mbalimbali za kimaisha badala ya kwa na vilio vya ukosefu wa ajira huku wakijikita katika ushabiki wa mambo ambayo hayana faida na kuziba fursa za maendeleo.


Akizungumza  wakati wa zoezi la Uchangiaji wa Damu ulioendesha na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Kilimanjaro; Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Moshi mkoani Kilimanjaro Ramadhani Matara amesema vijana wengi wamekuwa wakiamka asubuhi na kwenda kwenye michezo ya pool na ushabiki wa soka katika vijiwe huku wakiwa hawana kazi ya kufanya hatua ambayo imekuwa mwiba kwa maendeleo ya Taifa.


Aidha Matara amewataka vijana kuwa na ujuzi ambao wanaweza kuupa katika vyuo vya mafunzo ya ufundi kwa kozi za muda mfupi au mrefu ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuwa na uwezo wa kuzishangilia klabu hizo wakiwa vizuri.


Katika suala la uchangiaji wa damu Mkuu huyo wa Chuo amewataka vijana wa chuo chake kuendelea kuwa mabalozi wa utoaji wa damu hata baada ya kumaliza masomo yao chuoni hapo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Kilimanjaro Askofu Jones Mollah amesisitiza ulazima wa watanzania kuwa na utaratibu wa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine.


Mtaalamu wa Damu Salama Kanda ya Kaskazini Joseph Kessy, amesema bado mwitikio wa jamii kujitokeza kuchangia damu ni mdogo.


Naye Afisa Mhamasishaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi Renalda Kibona, amesema bado kundi la vijana wa kike wamekuwa waoga kujitokeza kuchangia damu tofauti na kundi la vijana wa kiume huku akisema kuwa elimu zaidi inahitajika kutolewa ili na wanawake waweze kujitokeza zaidi kuchangia damu.


Baadhi ya wanachuo walioshiriki katika zoezi hilo wamesema wamehamasika kujitolea damu licha ya dhana kwa walio wengi kuwa ukijitolea damu kuna matatizo yatajitokeza katika miili yao.


Zoezi la uchangiaji wa damu limefanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Moshi ikiwa ni wiki ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani ambayo kitaifa kilele itakuwa ni Machi 6 mwaka ju jijini Mbeya, ambapo wanachuo hao wamesaidia kupatikana kwa uniti zaidi ya 300.
















0 Comments:

Post a Comment