Mwandishi wa habari
na mtangazaji wa Redio Sauti ya Injili Samwel Shao amekuwa miongoni mwa
wanahabari wa kwanza mkoani Kilimanjaro kuongoza kura ya maoni ndani ya Chama
cha Mapinduzi (CCM) kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika
uchaguzi mkuu ujao kwenye ngazi ya udiwani.
Hayo yanajiri ikiwa
ni siku chache baada ya kauli ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania
(MCT) Kajubi Mkajanga kusema waandishi wa habari watapaswa kuacha kazi yao ya
habari endapo wataenda kuwania nafasi za kisiasa ili kutopoteza misingi ya
habari kwa ujumla.
Shao ameiongoza kura
za maoni katika Kata ya Mwika Kaskazini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro
akipata kura 26 kati ya 78 zilizofanyika Julai 25 mwaka huu na kutangazwa na
Msimamizi wa Kura za Maoni wa chama hicho Bariki Moses Kimaro.
Aliyemfuata
mwanahabari huyo ni Merry Shao aliyepata kura 17 akifungamana na Wilbard Shao
aliyepata kura 17. Nafasi ya Nne imeshikwa na Hubert Mariki aliyepata kura 7,
Harold Kimaro kura 6, Monyaichi Mlaki kura 5, Daniel Mgase kura 1 na Meja Jesse
Jeremia akiambulia patupu katika kura hizo za maoni. Mtia nia aliyefahamika kwa
jina la Nelson Eliya Massawe hakuonekana katika kura hizo za maoni.
Mwenyekiti wa kikao
hicho cha kata cha kura za maoni ndani ya CCM Wilbard William Shao ambaye ni
Mwenyekiti wa Tawi la Mlimbouwo alisimamia kikao hicho ambapo alisema watia nia
walikuwa 9 lakini waliothibitisha ushiriki wao ni 8.
Katibu Kata wa CCM
Mwika Kaskazini Leonard Mlaki alisema kumalizika kwa kura hiyo ya maoni
haimaanishi aliyeongoza ndiye ameshinda isipokuwa amewataka wajumbe wa mkutano
huo kusubiri uamuzi wa chama kama ilivyotangazwa mpaka jina litakaporudi ili
kupambana na vyama vingine katika uchaguzi wa mwaka huu.
Awali uchaguzi huo
ulianza na uandikishaji wa wajumbe wa mkutano huo ulitawaliwa na uwazi na
utulivu wa hali ya juu hadi akidi ilipotosha ndipo zoezi zima lilianza
kufanyika kwa watia nia kujinadi.
Wajumbe wa mkutano
huo walisimama kwa dakika moja kuomboleza kifo cha Rais wa awamu ya tatu wa
Tanzania Hayati Benjamini William Mkapa kilichotokea Julai 24, 2020 jijini Dar
es Salaam.
Kura ya maoni ya
kuchagua majina yatakayokwenda katika Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya kwa kata ya
Mwika Kaskazini ilifanyika kuanzia saa 4 asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa
Shule ya Sekondari ya Mwika ambapo Mkuu wa Shule hiyo Damian Petro alifungua mkutano huo kwa kuwakaribisha na
kuwatakia kila la kheri katika mchakato mzima wa kura ya maoni.
Wakati wa muda wa
Kampeni ulipofika kila mtia nia alipata nafasi ya kuzungumzia atawafanyia jambo
gani wakazi wa Mwika Kaskazini ambapo mwandishi wa habari Shao alisisitiza
ulazima wa kutetea shughuli za kimaendeleo ikiwamo suala la maji na barabara
katika kata hiyo.
Wanahabari wengine
mkoani Kilimanjaro walioingia katika kinyang’anyiro cha kura za maoni ndani ya
CCM ni Nakajumo James (Mabogini), Gift Mongi (Mwika Kusini) na Venance Maleli
(Rombo).