Angela Merkel |
Jina lake halisi ni Angela
Dorothea Merkel. Huyu ni Kansela wa Ujerumani. Alizaliwa Julai 17, 1954, mjini
Hamburg ni mwanasiasa wa Ujerumani ni Kansela wa Ujerumani tangu Novemba 22,
2005.
Licha ya kuzaliwa Hamburg, alikulia katika iliyokuwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Ujerumani maarufu kama Ujerumani ya Mashariki, kabla ya
Ujerumani zote mbili kuungana na kuwa moja.
Aliishi mashariki mwa Ulaya hadi
muungano Ujerumani ulipofanyika mwaka 1990. Angela Merkel kwa sasa ni
mwenyekiti wa chama cha Chama cha Kikristo cha Kidemokrasia cha Ujerumani
(CDU).
Mwaka 2009 alitangaza ya kuwa ataachana na Chama cha SPD akitafuta
ushirikiano na kile cha FDP. Uchaguzi wa Bunge wa Septemba 2009 ulirudisha
chama chake cha CDU kwa wingi wa viti Bungeni akaendelea kuunda serikali mpya
pamoja na FDP.
Tukiachana na hayo, kuna mambo kadhaa ambavyo huenda ukawa
huvijui kumhusu ikiwamo kutokuwa na watoto wa kuzaa. Angela ni binti wa Horst Kasner
na familia ya baba yake kwa kiasi fulani wana asili ya Poland.
Merkel ni jina
la mumewe wa kwanza aliyekuwa mwanafunzi mwenzake wa Fizikia ambaye waliooana
mwaka 1977 na kuachana miaka minne baadaye. Baba yake Merkel alikuwa mfanyakazi
katika Kanisa la Kilutheri.
Alihama na familia yake kutoka Ujerumani Magharibi
kwenda Mashariki iliyokuwa ikidhibitiwa na Urusi ya Kisovieti baada ya Angela
kuzaliwa huku maelfu wengine wakikimbia.
Angela Merkel |
Nidhamu, uangalifu na umakini wa
Merkel katika siasa mara nyingi unaelezwa ulitokana na makuzi yake ya Ujerumani
Mashariki. Alipokuwa na umri wa miaka tisa akiwa katika darasa la gym, aliwahi
kupooza kwa dakika 45 akiwa juu ya meza ya kujiandaa kurukia katika bwawa la
kuogelea.
Mwishowe aliamka na kuruka majini kabla ya darasa kumalizika. Ana
shahada ya fizikia na uzamivu katika kemia na baadhi ya mafanikio yake kama
mwanasiasa yanatokana na utaalamu wake wa siasa na uchambuzi wa hali halisi.
Alienda
kufanya kazi kama mwanasayansi mtafiti akiwa mwanamke pekee katika kitengo cha
nadharia ya kemia katika Chuo cha Sayansi cha Ujerumani Mashariki. Kufikia
mwishoni mwa 1970, Merkel aliomba kazi ya profesa msaidizi katika shule ya
uhandisi na alitakiwa kujiunga na Stasi, yaani polisi wa siri wa Ujerumani
Mashariki.
Hata hivyo, alikataa kujiunga
na kikosi hicho kilichoogopewa, akidai atakuwa mpelelezi mbaya kwa vile ana
mdomo kama kasuku. Hivyo, akakosa kazi lakini pia iwapo angejiunga na polisi
hao, asingefikia hapo alipo kisiasa. Yaani iwapo angejiunga nacho, hatima ya
baadaye ya kisiasa ingekuwa ngumu, kwa vile wanasiasa wa Ujerumani iliyoungana
waliokuwa na uhusiano ya nyuma na Stasi walihesabiwa sumu kali na wengi
walilazimika kujiuzulu baada ya kubainika uhusiano wao nao wa nyuma.
Baada ya
Merkel kutengana na mumewe wa kwanza, akaishi kama mtu asiye na makao maalumu
akijikunyata katika makazi haramu karibu na stesheni ya reli ya
Friedrichstrasse. Wakati wa siku yake ya 30 kuzaliwa akionekana kana kwamba
anaelekea kupotea, baba yake alimtembelea na kumwambia ‘hujachelewa bado
kujirudi.”
Usiku mmoja ukuta wa Berlin ukaangushwa ile Novemba 1989, akiwa na
umri wa miaka 35 alitembelea sauna.
Baada ya kuranda randa mpakani na wengine
akipoza koo kwa chupa moja ya bia mara moja alirudi nyumbani ili asijichokee
kwa kazi ya siku iliyofuata.
Karibu kila Mjerumani alikuwa mtaani usiku mwingi
kusherehekea tukio hilo. Mumewe wa sasa Joachim Sauer, profesa wa chuo Kikuu
cha Berlin anachukia kumulikwa hadharani na hivyo huwa hajitokezi katika
matukio mengi ikiwamo wakati wa alipoapishwa kwa mara ya kwanza ukansela mara
ya kwanza mwaka 2005.
Mumewe huyo anajulikana kwa kubana matumizi ikiwamo
kupanda ndege za gharama nafuu hata kama anaruhusiwa kusafiri na mkewe katika
ndege rasmi. Merkel ameripotiwa kuwa mpishi mzuri na mtaalamu wa kutengeneza
kesi na amekuwa akionwa akinunua katika groceries katika maduka makubwa ambako
hulipa pesa taslimu. Na alimwambia Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan
kuwa humwandalia mumewe kifungua kinywa kila asubuhi.
Ni mwoga wa mbwa baada ya
kuwahi kung’atwa mwaka 1995, kitu kinachodaiwa kumfanya Rais wa Urusi Vladimir
Putin mara kwa mara kutumia mbwa wake kujaribu kumwongopesha. Mara kwa mara
huingia katika vyumba vya kubadilisha nguo vya timu za soka na kupongeza
wachezaji na aliwahi kumshuhudia nyota wa Ujerumani Bastian Schweinsteiger
akiwa mtupu kama aliovyozaliwa.
Merkel aliingia katika
siasa na kuwa kama msemaji wa waziri mkuu wa mwisho katika iliyokuwa Ujerumani
Mashariki, Lothar de Maiziere, wakati huo akiwa na umri wa miaka 35. Ni mchapa
kazi katika chama chama cha CDU.
Chini ya Kansela Helmut Kohl mwaka 1994
alikuwa waziri wa mazingira na usalama wa nyuklia, wizara muhimu kabisa kwa mtu
anayeshikilia shahada ya uzamifu katika fizikia.
Baada ya kushindwa Helmut Kohl
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1998, chama cha CDU kilipata mshtuko mkubwa
lakini sio kwa Merkel, ambaye aliitumia nafasi yake barabara na mwaka 2000
akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho. Mwaka 2005 katika uchaguzi mkuu
akatokeza kuwa mgombea mkuu wa chama hicho wa ukansela.
Merkel alipata ushindi
lakini ilimbidi kuunda serikali ya pamoja na chama cha SPD. Merkel anakiongoza
chama hicho cha CDU kwa mwaka wa 19 sasa na amekuwa kansela kwa miaka 14.
0 Comments:
Post a Comment