Tuesday, July 30, 2019

Viongozi wa vyama vya ushirika waonywa kuhusu mikataba

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kilimanjaro Joseph Henjewele (mwenye kipaza sauti) akitambulisha wajumbe wa mkutano wa 35 wa KNCU uliofanyika Julai 30, 2019 mjini Moshi. 

Viongozi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kuacha mara moja kuingia mikataba pasipo kufuata kanuni, taratibu na sheria zinazotakiwa ili kuepusha migongano ya kimaslahi ndani ya vyama hivyo.


Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 35 wa KNCU uliofanyika mjini Moshi mkoani humo, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kilimanjaro Joseph Henjewele alisema vyama vya Ushirika vimekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya Tanzania na Serikali inauona ushirika kuwa ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo.

“Inapotokea viongozi wanaingia mikataba isiyo na tija kwa vyama vya ushirika inaleta kero na matatizo yanazidi badala ya kuwaletea watu maendeleo,” alisema Henjewele.

Henjewele alisema mikataba ya jinsi hiyo haipaswi kupewa nafasi katika vyama vya ushirika na kwamba hakutakuwa na uvumilivu kwa viongozi watakaofanya hivyo.

“Mkataba kabla haujasainiwa unatakiwa ufike kwa mrajisi ili aweze kuupitia ikishindikana unapelekwa katika ngazi za juu ili kuondoa mikataba isiyo na tija,” aliongeza Henjewele.

Aidha Henjewele aliwataka viongozi kuacha kupitia vichochoroni kupitisha mikataba hiyo na badala yake wapitie kwenye mkutano mkuu wa chama husika cha ushirika hatua ambayo itamwondolea usumbufu na kumweka huru.

“Watu wanaofanya kazi pamoja wanaweza kutatua matatizo ambayo hayawezi kutatuliwa na mtu mmoja mmoja. Kupitia kwenye mkutano mkuu kutakuweka huru,” alisisitiza Henjewele.
Wajumbe wa Mkutano wa 35 wa KNCU, Julai 30, 2019 mjini Moshi, Kilimanjaro.
STORY BY: Jabir Johnson, Moshi…..Julai 30, 2019; PHOTO BY: Joseph Tesha

0 Comments:

Post a Comment