Thursday, July 4, 2019

Tembo wavamia waua, wajeruhi Same


Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Hansi Edensi (47), mkulima na mkazi wa kijiji cha Mheza kata ya Maore Wilayani  ya Same mkoani Kilimanjaro, amefariki dunia baada ya kujeruhiwa na Tembo akiwa shambani kwake.


Akithibitisha  kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi  Hamisi Issah, alisema mnamo  Julai  Mosi majira ya saa tatu asubuhi, marehemu alishambuliwa na wanyama pori hao wakati alipokuwa analinda shamba lake.

“Mnamo Julai Mosi mwaka huu, majira ya saa tatu asubuhi  marehemu akiwa shambani kwake, alivamiwa na tembo hao ambao walimshambulia na kumjeruhi ,"alisema.

Alifafanua kuwa "Kutokana na  tembo hao kuwa wanavamia shamba lake  na kula mazao yake na kufanya uharibifu, aliamua kuwa anakwenda kwa lengo la kulinda ndipo tembo hao walimvamia na kuanza kumshambulia hali iliyopelekea kifo chake,”alisema Issah.

Aidha katika maeneo ya Same mjini, waliweza kuoneka tembo wawili ambao walikuwa wakifukuzwa na wananchi ili kuweza kuwarudisha katika maeneo walikotoka ndipo walipomkuta mama mmoja ambaye alikuwa anakata maji kwa ajili ya kulisha ng’ombe  tembo mmoja aliweza kumshambulia na kumjeruhi  Mama huyo na kumjeruhi ambapo kwa sasa  amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Same kwa matibabu zaidi.

Kamanda Issah, alisema uongozi wa hifadhi ya Mkomazi kwa kushirikiana na maafisa wanyama pori wa wilaya ya Same wanaendelea kuwarudisha tembo hao kwenye maeneo yao.
Alisema wanyama hao kwa sasa hivi wamezagaa maeneo yote ya mji wa Same wakitokea katika hifadhi ya Taifa ya Mkoamazi kwa ajili ya kutafuta chakula na kutoa wito kwa wananchi wanapowaona wanyama hao kutoa taarifa ili waweze kudhibitiwa.

Mkazi wa Same mjini Josephat Mkwizu alisema wakazi hao wanaishi kwa hofu baada ya tembo hao kuonekana kila maeneo ya mji huo na kuwatishia maisha yao, ambapo amedai kwamba tembo hao wametokea katika hifadhi ya taifa Tsavo  na kuvamia maeneo yao.

“Tembo hawa tuliwaona kuanzia jana wakiwa makundi makundi, wakiwa wanafukuzwa na wananchi kurudishwa katika maeneo walikotoka, wananchi wamekuwa na hofu kubwa huku wengine wakishindwa kutoka ndani kwa ajili ya kwenda kujitafutia mahitaji yao ya  kila siku,”alisema Mkwizu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Sinyamule alikiri kutokea kwa makundi hayo na kuwataka wananchi hao kuwa watulivu wakati serikali ikilifanyia kazi suala la tembo hao kuwarejesha katika maeneo yao.

STORY BY: Kija Elias

0 Comments:

Post a Comment