Saturday, July 20, 2019

Bilioni 45 zapelekwa Kilimanjaro sekta ya afya na elimu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya kukata utepe na kulipokea treni la mizigo mjini Moshi Julai 20, 2019


Imeelezwa kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 45 zimepelekwa katika mkoa wa Kilimanjaro ili kuimarisha sekta ya Afya na Elimu.


Akizungumza wakati wa kulipokea treni la mizigo mjini Moshi ambalo lilionekana mara ya mwisho miaka 17 iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema wamepeleka fedha hizo ili kuhakikisha sekta ya afya inaimarika.

“Tumeleta fedha Zaidi ya milioni 695 katika Manispaa ya Moshi, ili ziweze kujenga kituo cha afya pasua, pamoja na kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana wakati wote, katika jimbo la Vunjo shilingi bilioni tatu ili kuweza kujenga kituoa cha afya cha Uru Kyaseni na kununua dawa na kuhakikisha kwamba tunaimarisha sekta ya afya kwa wananchi wa wilaya ya Moshi,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa alifafanua kuhusu mgawanyo wa fedha hizo katika wilaya nyingine mkoani humo,

“Mwanga, Serikali imepeleka Shilingi Bilioni 1.245 katika sekta ya afya ili waweze kununua dawa, Siha Shilingi Bilioni 2.15 ili kujenga hospitali ya wilaya na kuimarisha vituo vya afya dawa na vitenganishi, Same, Shilingi Bilioni 2.122, ili kuweza kuboresha huduma za afya, Rombo Shilingi Bilioni 1.700 na Hai Shilingi Bilioni 1.567.9 kwa ajili ya kutoa huduma katika sekta ya afya mkoa wa Kilimanjaro,” alisema Waziri Mkuu.

Majaliwa alisisitiza kuwa serikali inataka kuona kila mtanzania anapata huduma bora za Afya na Elimu.

Katika sekta ya elimu Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 34.3

“Moshi Manispaa Shilingi Bilioni 4.5, Moshi Vijijini  Shilingi Bilioni 6.4, Mwanga Shilingi Bilioni 2.9, Siha Shilingi Bilioni 1.6 Same Shilingi Bilioni  5.8, Rombo Shilingi Bilioni 3.4,  Shilingi Bilioni Hai 3.8; tunataka elimu iendelee kukuzwa mkoani Kilimanjaro  serikali inatambua mkoa wa Kilimanjaro ni mkoa wa kwanza kwa kuwa na shule nyingi na sasa serikali inaendelea kuziboresha,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa. 

STORY BY: Jabir Johnson & Kija Elias, Moshi….Julai 20, 2019.

Treni iliyopokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Julai 20, 2019 mjini Moshi.


0 Comments:

Post a Comment